Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuwepo leo nikiwa hai. Pili, nakushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuweza kuongea katika kikao hiki cha leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwa ufinyu wa muda nianze kwa kuzingatia kanuni ya 175 katika Kanuni zetu za Kudumu. Pili, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri aliyeitoa. Kwa kweli ukiisoma ile hotuba, imelezea mambo mengi yaliyofanyika katika nchi hii na kwa kweli mambo yale yamefanywa na viongozi wetu wakubwa kwa Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba natoe ushauri mdogo sana kwa Serikali, lakini tukiufanyia kazi tutaweza kudhibiti uvujaji wa mapato katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kufuatilia miaka yote sioni forum ya kisheria inayompa nguvu Mkuu wa Wilaya aweze kusimamia mapato yanayopelekwa katika Halmashauri zetu kutoka Serikali Kuu. Serikali Kuu inapeleka kwenye Halmashauri zetu, zaidi ya asilimia 80 ya mapato zinaiendesha Halmashauri zetu. Mapato yale yanapofika kwenye Halmashauri zile basi Mkurugenzi anafanya yale anayoyataka bila kupata concern ya Mkuu wa Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri iundwe forum maalum ya kumfanya Mkuu wa Wilaya awe Mwenyekiti; Mkurugenzi awe Katibu; Wabunge wa Majimbo na Viti Maalum wawe Wajumbe wa forum hiyo. Forum hiyo nashauri iitwe Kamati ya Maendeleo, Nidhamu na Utawala. Kamati hiyo itatusaidia sana kudhibiti mapato katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme ya watu wa Jimbo la Mbagala. Sekta ya Afya katika Jimbo letu la Mbagala tunayo ile Hospitali ya Wilaya ya Zakiem. Nadhani ni hospitali pekee katika nchi yetu yenye level ya wilaya isiyokuwa na wodi za kulaza wagonjwa. Naiomba sana, Serikali tuipe hadhi hospitali ili tuweze kupata wodi za kulaza wagonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika Sekta ya Elimu, sote tunafahamu katika Jimbo la Mbagala, ndiyo jimbo lenye shule zenye wanafunzi wengi nchi nzima. Shule ya Maji Matitu ina wanafunzi zaidi ya 9,000. Naiomba sana Serikali ilisaidie Jimbo la Mbagala kulipatia shule za kutosha. Katika hili namwomba dada yangu Mheshimiwa Jenista, ndugu zetu wa NSSF wana maeneo mengi wasiyoyaendeleza. Tunaomba sana mtupe maeneo yale yaliyokuwa Tuangoma twende tukajenge shule.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie katika kuzungumza suala la TARURA. Barabara nyingi katika Jiji letu la Dar es Salaam zimekuwa na matatizo makubwa. Mheshimiwa Rais amesema, Halmashauri zetu huko nyuma zilikuwa zinatenga fedha zaidi ya shilingi bilioni nne kila Halmashauri katika ku-service barabara zile. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri utaratibu ule uendelee kurudiwa ili fedha zile zikiunganishwa na fedha zinazotoka kwenye Road Fund ziweze zikafanye kazi kubwa. Kuna Kata ya kama ya Kiburugwa na Kata ya Mianzini iko hoi katika suala nzima la barabara.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)