Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kushukuru kwa nafasi hii niliyoipata. Nichukue fursa hii pia kukishukuru Chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwanza kwa kuleta shukrani kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Kilolo. Wengi wameshukuru uongozi wa Rais wetu Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa mambo makubwa aliyoyafanya. Wananchi wa Kilolo wanamshukuru na watamkumbuka kupitia mambo mbalimbali ambayo waliyapata katika kipindi cha awamu iliyopita na wamenituma nishukuru kwa mambo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanashukuru kwamba Mji wa Ilula ambao haukuwa na maji kwa miaka mingi sasa una maji ya kutosha na ni kupitia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Wanashukuru sana Wizara ya Maji kwa kuwapatia maji watu wa Mji wa Ilula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Kilolo wanashukuru kwa mara ya kwanza kwenye vijiji wamepata barabara ya lami kilomita 18 kutoka Kidabaga - Boma la Ng’ombe. Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI ametembelea ameona barabara ile inaendelea kujengwa. Wanashukuru sana na watamkumbuka Hayati Dkt. John Joseph Magufuli kwa jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanashukuru kwa sababu wamejengewa hospitali ya wilaya. Wanaishukuru sana Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba kwa mara ya kwanza Wilaya ya Kilolo ina hospitali nzuri ya mfano ambayo itatibu watu wengi na watu wale wataondokana na kero waliyokuwa nayo ya maradhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya mengi yaliyofanyika ambayo wananchi wa Kilolo hawatamsahau Dkt. John Joseph Pombe Magufuli katika uongozi wake niliona nitaje hayo machache. Kwa niaba ya wananchi ambao wamenituma, hayo yamefanyika na yanaonekana na ndiyo ambayo ni kielelezo cha utendaji mzuri wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hao pia wamenituma nikumbushe mambo machache kwa Serikali hii sikivu. Jambo la kwanza wameniomba nikumbushe kwamba ile barabara ambayo ni ahadi ya kutoka Iringa Mjini kwenda Kilolo hadi Idete bado barabara ile inaendelea kujengwa lakini haijakamilika. Wanaamini Serikali hii sikivu itatekeleza hilo kwa sababu imo kwenye ahadi na kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wananchi hawa wa Kilolo wanakumbusha kwamba mara kwa mara viongozi waliotembelea pale Kilolo akiwepo Waziri wa TAMISEMI, Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda kwa kuona ukubwa wa Halmashauri ya Kilolo waliahidi kuigawa Halmashauri ile na kuwa Halmashauri mbili na pia kuelekea kugawa lile eneo kuwa Majimbo. Jambo hili lipo TAMISEMI hasa la halmashauri na wananchi wale wa Kilolo wanaomba kupata majibu ni lini sasa halmashauri ile itagawanywa ili kupata halmashauri mbili ili kurahisisha utekelezaji wa mambo mbalimbali hasa kuleta karibu huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wanakumbusha kwamba kuna ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara ambayo ni ya kituo cha afya pale katika Mji wa Ilula. Nayo pia wanaikumbusha kwamba Serikali iangalie na kwa kuwa hii ni bajeti ya Waziri Mkuu basi wanaomba kukumbusha hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa ujumla wake niendelee kukumbusha ajira kwa vijana hasa walioko katika shule za sekondari ambao wanajitolea; walimu wa kujitolea kwenye shule mbalimbali wa masomo ya sayansi. Wako wengi hata katika Jimbo la Kilolo lakini na katika maeneo mbalimbali, hilo pia tunakumbusha kwamba liendelee kuangaliwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye….

NAIBU SPIKA: Kengele imegonga Mheshimiwa.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukruu sana, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. (Makofi)