Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Nianze kwa kusema naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujielekeza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujikita zaidi katika Kamati ya Masuala ya UKIMWI. Sote hapa tutakubaliana kwa namna moja ama nyingine kila mmoja ameguswa na janga hili la UKIMWI, kama siyo yeye mwenye basi ndugu yake, jirani yake ama rafiki yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu nchini Tanzania zinaonesha kila siku iendayo kwa Mungu watu 200 wanaambukizwa UKIMWI na Virusi vya UKIMWI, watu 6,000 kwa mwezi na watu 72,000 ndani ya mwaka. Bado tukiziangazia takwimu, Mkoa wa Njombe ndiyo mkoa nchini Tanzania unaoongoza kwa maambukizi ya makubwa kwa asilimia 11.4, ukifuatiwa na Mkoa wa Iringa wenye asilimia 11.3, ukifuatiwa na Mkoa wa Mbeya wenye asilimia 9.3. Hii ndio mikoa top three nchini Tanzania inayoongoza kwa maambukizi ya UKIMWI na Virusi vya UKIMWI. Hivyo, ni kuonyesha ni kwa namna gani UKIMWI bado ni janga la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na takwimu hizo na hali ya maambukizi nchini, napenda kuipongeza Serikali kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI yaani TACAIDS kwa namna inavyopambana na kudhibiti UKIMWI na Virusi vya UKIMWI. Hili linadhihirishwa na survey iliyofanywa mwaka 2013, kiwango cha maambukizi kilikuwa asilimia 5.1 ukilinganisha na survey iliyofanywa mwaka 2017 kiwango hicho cha maambukizi kilishuka mpaka asilimia 4.7. Kwa hiyo, hii ni kusema kwamba maambukizi ya UKIMWI yamekuwa yakipungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hiyo ya kupungua kwa maambukizi ya UKIMWI na Virusi vya UKIMWI nchini, inachagizwa na jitihada nzuri zilizofanywa na Serikali kufikia zile 90, 90, 90. Sasa tunabakiwa na jukumu moja kubwa ya kufikia malengo tarajiwa ya mkakati wa Kitaifa kwamba mpaka kufikia mwaka 2025 tuhakikishe tumefika zile 95, 95, 95 kwa maana maana 95 ya kwanza asilimia 95 ya Watanzania tuwe tumepima virusi vya UKIMWI, lakini asilimia 95 ya Watanzania ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI wawe wanatumia dawa na asilimia 95 ambao wako kwenye kutumia dawa wahakikishe hawawi watoro kwenye kufuata dawa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaweza kuzifikia hizi 95 tatu ifikapo 2025 ama hizi sifuri tatu ifikapo mwaka 2030, endapo Serikali itaendelea kujidhatiti katika masuala mazima ya kuhakikisha tunatenga bajeti kwa kutumia fedha zetu ndani. Kwa kiasi kikubwa bajeti ya UKIMWI hususan kwenye upande wa miradi ya maendeleo tumekuwa tukitegemea wahisani. Kama tutaendelea kutegemea wahisani, siku wakijitoa au wafadhili wakiacha kutupatia fedha hizi ina maana lile lengo tulilolikusudia kama Taifa ifikapo 2030 tufike zile sifuri tatu itabaki kuwa historia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba katika kulidhihirisha hili kwa namna gani tupambane kufikia 95 tatu ama kufika 0 tatu kwa kuangalia mwenendo wa bajeti hii tunayoenda nayo. Tume yetu ya Kudhibiti UKIMWI yaani TACAIDS kwenye bajeti hii tunayoenda nayo iliidhinishiwa shilingi bilioni 4.9, kama fedha za miradi ya maendeleo ambapo shilingi bilioni 1 ndiyo fedha ndani, zilizobaki ukitoa katika bilioni 4.9 ni fedha kutoka kwa wa hisani. Nini tafsiri yake? Asilimia 76.6 ya fedha ya masuala ya UKIMWI zinatokana na wahisani. Fedha zinazotokana na wahisani sio vyanzo endelevu, lakini pia niseme kutenga bajeti ya masuala haya ambayo bado ni janga la Kitaifa, maambukizi ni kwa asilimia 4.1, kwa kutegemea wafadhili kama Taifa tunakuwa hatuendi sawasawa. Rai yangu kwa Serikali tujitahidi tuhakikishe kwamba asilimia 75 ya fedha za miradi ya maendeleo katika masuala mazima ya UKIMWI yatokane na fedha zetu za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa pengine niishauri Serikali, tunazo taasisi, NGO lakini pia tunazo zile Asasi ambazo kimsingi ziko chini ya TACAIDS au ambazo zinaangaliwa na TACAIDS hasahasa zile zinazopewa technical supports na TACAIDS, Serikali sasa wakati umefika wa kuangalia namna bora ili taasisi hizi kupitia maandiko yao watenge sehemu ya mchango angalau percent fulani ili iweze kuingia kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI. Tukifanya hivi, tutakuwa tumepata chanzo endelevu katika kutafuta afua hizi za UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikigeukia upande wa Mfuko huu wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (Aids Trust Fund) ambao wenyewe umetengewa shilingi bilioni 1. Pesa hizi ni za juzi juzi tu kwa msaada wa Mheshimiwa Spika baada ya kuitisha Kamati ya Uongozi na Kamati yetu ya Masuala ya UKIMWI kulibeba jambo hili kama jambo mahsusi ndipo Serikali ambapo mmetoa shilingi milioni 500. Kwa hiyo, nachopenda kuishauri Serikali tutoe hizi fedha kwa wakati. Hizi shilingi milioni hizi 500 mlizozitoa ambazo ni nusu ya bajeti, napenda sana kuiomba na kuisisitiza Serikali mpaka kufika Juni, 2021 mhakikishe mmemaliza sehemu iliyobaki ili afua za UKIMWI ziweze kupatikana kwa unafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa mwisho nitajielekeza kwenye masuala ya madawa ya kulevya. Tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Mamlaka imekuwa haitengewi fedha za miradi ya maendeleo. Kama hatutatenga fedha za miradi ya maendeleo, changamoto ya kwanza ni ile iliyosemwa na Kamati kwamba tutakuwa uhaba wa Vituo vya Waraibu wa Madawa ya Kulevya ambao wanapatiwa ile dawa ya methadone. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa tunapambana na pia kupitia wadhamini ama wafadhili wanaotusaidia kupambana na masuala ya UKIMWI pamoja na madawa ya kulevya, tunahangaika kuwasaidia vijana wetu kuwapatia afua za UKIMWI na methadone ili watoke kwenye ule uzombi warudi katika hali ya kawaida, lakini hatuna miradi ya maendeleo. Wanaporudi katika hali yao ya kawaida, tukikosa kuwajengea uwezo, wakikosa shughuli za kufanya, it’s obvious watarudia tena kule kwenye kuvuta haya madawa ya kulevya. Ndiyo maana tunaitaka Serikali kutenga miradi ya maendeleo ili kuweza kusadia kundi hili na hususan wengi wake ni vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunafanya ziara ya ukaguzi wa miradi, tumetembelea hizi sober house, unakutana na wale waraibu wa madawa ya kulevya, ambao tayari wameshapewa dawa ile ya methadone wamerudi kwenye hali ya kawaida, wanasema wakirudi mtaani hawana cha kufanya, wakienda kwenye familia wananyanyapaliwa, kwa hiyo wanajikuta wanarejea tena kwenye uvutaji wa madawa ya kulevya. Kwa hiyo, nachopenda kukisisitiza hapa, tutenge fedha za miradi ya maendeleo ili tuweze kuokoa nguvu kazi ya vijana wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja, nakushukuru. (Makofi)