Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kutoa pole kwa watanzania wote kwa msiba mkubwa uliotupata lakini vilevile nitambue mchango mkubwa uliofanywa na Hayati Dkt. Magufuli kwa kushirikiana na mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Ni mchango mkubwa sana uliofanyika ndani ya muda mchache sana na mafanikio makubwa sana, tumeyaona na tutayaendelea kuyaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nijielekeze katika masuala ya kilimo na mazao ya mbogamboga. Ni zaidi ya asilimia 90 ya mazao ya mbogamboga yanayosafirishwa kupitia bandari ya Mombasa, kitu ambacho kinawapa gharama kubwa sana wafanyabiashara na wakulima wa mazao haya ya mbogamboga. Natambua Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda wamekaa kwa pamoja na kuweza kuanzisha mradi wa Kurasini Agricultural Logistic Hub itakayokuwa once stop center ambayo ndiyo itakuwa cold chain ya mazao haya ya mbogamboga yanapokuwa yanasubiri kwenda kusafirishwa nje ya nchi kwa kutumia bandari yetu ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mradi huu ni mradi ambao umehusisha sekta binafsi. Niwapongeze sana Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda kwa kuwa wasikivu kwa sababu haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambayo aliyatoa wakati akiwa Makamu wa Rais mwaka jana. Kwa kweli viongozi wa namna hiyo ndio ambao tunawahitaji katika Taifa letu la Tanzania; pale mkubwa anapotoa tu maelekezo na kuweza kuyafanyia kazi mara moja. Lakini kwa kuwa Kurasini Agricultural Logistic Hub ndio muarubaini wa mazao ya mbogamboga kusafirisha kupitia bandari kwenda nje, nilitaka kujua, ni lini mradi huu utakamilika na kwa sasa hivi mradi huu umefikiwa wapi? Ili tuweze kujua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo tunatambua kwamba imeanzisha mchakato wa Bodi ya Horticulture. Nataka kujua pia bodi hii ipo kwenye stage gani na lini itakamilika. Sababu katika mazao ya mbogamboga kuna zao ambalo linakuja kwa kasi sana, zao la parachichi. Na kama tunavyojua ni mikoa zaidi ya kumi Tanzania inalima zao hili la parachichi ikiwemo mkoa wa Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya, Rukwa, Tanga na mikoa mingine. Kuna umuhimu sana wa bodi hii ya horticulture kukamilika ili zao hili la parachichi pamoja na mazao mengine ya mbongamboga yawe yanafanyiwa kazi kwa utaratibu mzuri na kuweza kuleta tija kwa wakulima wa mazao haya ya mbogamboga likiwemo na zao la parachichi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika zao hili la parachichi, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja Njombe akatembelea baadhi ya mashamba ya parachichi, nilimuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba zao hili sasa ikiwezekana liwekwe katika zao la kimkakati kutokana na umuhimu na unyeti wake. Zao hili kama tutalisimamia vizuri tutaweza kuongeza mapato ndani ya Taifa letu lakini vilevile tutawakwamua wananchi kupitia ajira kupitia ajira mbalimbali zitakazotokana na zao hili la parachichi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fursa hii tunayoiona sisi ya kulima zao la parachichi na kusafirisha nje, imeonwa na nchi nyingine nyingi. Ombi langu kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba wanawasaidia wananchi ambao wanalima zao hili la parachichi kwa kuweka mikataba mizuri na nchi walaji kwa maana kwamba watakapokwenda kuuza hili huko nje Serikali imeshaweka mikataba itakayokuwa inawasaidia wananchi wetu wasikandamizwe. Kama hii fursa imeonwa sasa hivi na nchi nyingi baadaye soko linaweza kuharibika. Kama sisi tutakuwa tumewahi kuweka mikataba mizuri ina maana tutakuwa tumewasaidia kuwalinda wananchi wetu wasiweze kutaabika siku zijazo kutokana na supply kuwa kubwa na demand kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa Serikali imefanya kazi nzuri, imeshaagizia ndege ya mizigo kwa ajili ya kuweza kusafirisha mazao haya ya mbogamboga ikiwemo na parachichi na vilevile natambua kwamba Serikali imeandaa mfumo mzuri wa cold-room katika Kiwanja cha Ndege cha Songwe, lakini bado siyo wote wanaweza kusafirisha kwa kutumia ndege wengine watatumia Bandari ya Dar es Salaam. Pamoja na kuanzisha mradi mzuri ule wa Kurasini, bado kuna umuhimu wa kuboresha mfumo wa cold room kwenye baadhi ya mabehewa katika Reli yetu ya TAZARA ili wale wananchi wa Nyanda za Juu Kusini ambao wanalima zao hili la parachichi waweze kusafirisha parachichi yao kuanzia ile process ya kutoa shambani, kusafirisha sasa kutoka kule Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, kupelekeka Dar es Salaam waweze kutumia reli hii ambapo gharama ni nafuu kuliko usafiri mwingine watakaotumia mfano kama vile maroli na kadhalika ambayo gharama ni kubwa sana. Kwa hiyo, kwa kutumia reli, wanaweza wakasafirisha kwa gharama nafuu na hapo ndiyo tutaona umuhimu wa kutumia ile Bandari ya Dar es Salaam baada ya kumaliza mradi ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuzungumzia Bima ya Afya. Tunashukuru Bima ya Afya iko vizuri lakini kuna maboresho makubwa yanatakiwa yafanyike kwa wananchi, kwa sababu wanalalamika, wanapotumia Bima ya Afya ya Serikali kule hospitali hawapati dawa, kuna umuhimu wa kuboresha. Vilevile, ukija kwa Wabunge humu ndani, Wabunge wengi Bima hii ya Afya haiwafaidishi kwa sababu utakuta watu wengine ni wazee, kwa mfano, Mzee Mheshimiwa Athuman Maige, mama yangu Mheshimiwa Margaret Sitta, hawana watoto wenye chini ya miaka 18. Vilevile utakuta kuna Wabunge vijana humu, hawana watoto wadogo, hawajazaa kabisa. Kwa hiyo, bima hii ijielekeze kutumika kwa watu tegemezi, kwa maana kama mama yangu pale Mheshimiwa Margaret Sitta na baba yangu Mzee Mheshimiwa Athuman Maige, bima ile ikasadie wazee wao maana wazazi wao wapo. Vilevile kwa vijana hawa ambao hawana watoto ikasaidie wazazi wao.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Bima hii ya Afya iangaliwe na ifanyiwe maboresho makubwa kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini vilevile kwa wananchi wetu ili iweze kuleta tija na maana halisi ya Bima ya Afya. Kwa sababu nia yetu ni kusaidia wananchi lakini vilevile kuwasaidia Wabunge ukiwemo na wewe na Mheshimiwa Naibu Spika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, ahsanteni sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na siyo kwamba nafagilia kugombea Ukamishna. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Aaah, kwa hiyo hugombei tena? Ndiyo unamaanisha hivyo?

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nagombea ila hoja muhimu. (Kicheko)