Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake kwa bajeti ambayo waliwasilisha jana. Naomba nijiongoze katika maeneo yafuatayo;

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ahadi ambazo viongozi wetu wa juu wanazitoa ambazo kwa kweli zinahitaji kutekelezwa kwa sababu ahadi ya viongozi hao ni maagizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2011 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya nne alitoa ahadi pale Nanyumbu kujenga kituo cha afya katika Kata ya Mkangaula. Ahadi ile imekuja kutekelezwa mwaka jana. Katika utekelezaji wa ahadi ile zilitolewa milioni 200 lakini milioni 200 mpaka sasa hivi hazijatolewa. Kwa hiyo naomba Ofisi ya Waziri Mkuu, jambo hili liangaliwe katika utekelezaji wa ahadi za viongozi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwahi kufika Mangaka tarehe 26/2/2018 na akatoa ahadi ya kujenga barabara zetu za lami kilometa tano; mpaka sasa hivi hakuna hata kilometa moja iliyotekelezwa. Kwa kweli naomba sana, ahadi hizi zinapotolewa wananchi wana imani na viongozi wetu, na zisipotekelezwa tunatoa mashaka kwa wananchi wetu kuwaamini viongozi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mama yetu Rais, Samia Suluhu Hassan alipokuja kwenye kampeni pale Nanyumbu alitoa ahadi ambayo ipo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kujenga barabara ya lami itakayounganisha Mkoa wa Mtwara na Morogoro kupitia Seluu; na barabara ile inaanzia ndani ya jimbo langu. Ni matarajio yangu kuwa utekelezaji wa ahadi ile utaanza katika mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba sana niungane na Waheshimiwa Wabunge ambao jana walizungumza, kwamba kuwe na kitengo maalum cha kuratibu ahadi za viongozi wetu. Mheshimiwa Rais wetu mpenzi ambaye ametangulia mbele ya haki kuna ahadi nyingi alizotoa, ni matarijio yangu zitatekelezwa ndani ya awamu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mfuko wa wanawake, vijana, na wenye ulemavu; mfuko huu unategemea mapato ya Halmashauri. Halmashauri nyingi mapato yao ni madogo sana. Wanaonufaika na mfuko huu ni zile Halmashauri ambazo zinauwezo wa kimapato. Lakini mimi concern yangu ipo katika asilimia mbili ya walemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mlemavu na ni Mbunge wa Jimbo, tunazo changamoto kubwa sana sisi walemavu halafu mnatupangia asilimia mbili, jamani hamtuonei huruma. Ninyi wazima mnaweka asilimia nne na sisi walemavu mnatupa asilimia mbili pamoja na changamoto zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kuishauri Serikali, lazima mfuko huu wa wawalemavu uangaliwe na usitegemewe fedha za Halmashauri. Serikali Kuu itenge fedha kwa kila Halmashauri kuwasaidia hawa walemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, walemavu tuna changamoto kwenye elimu. Tunasoma katika mazingira magumu na baada ya kusoma tunategemea tupate ajira. Ukisoma sheria ya ajira kifungu cha 31 (2) ajira za walemavu imeeleza bayana kila mamlaka itakayoajiri watu kuanzia ishirini na kuendelea asilimia tatu wawe walemavu. Najiuliza sheria hii inatekelezwa? Ni kweli taasisi zetu, Wizara zetu zinaasilimia tatu ya walemavu? Na mimi namshukuru sana Mheshimiwa Rais, ndani ya Wizara hii Naibu Waziri ni mlemavu, naamini ataisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nyingine naomba nijielekeze kwenya afya. Kule Jimboni kwangu kuna mgogoro wa afya. Kuna fedha zilitakiwa ziletwe ndani ya Jimbo langu kujenga kituo cha afya Nanyumbu…

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mhata kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa

T A A R I F A

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimsahihishe tu Mheshimiwa anayeongea pale, asahihishe, watu wenye ulemavu sio walemavu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khadija

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, Yes.

NAIBU SPIKA: Toa taarifa yako.

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yangu ni kwamba nataka nimsahihishe kwamba ni watu wenye ulemavu na sio walemavu. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Yahya Mhata unaipokea taarifa hiyo.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana mlemavu mwenzangu amenisahihisha, ni watu wenye ulemavu, na ulemavu ni wa aina zote; nashukuru sana kwa masahisho hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nieleze tatizo la Wizara ya Afya katika Jimbo langu. Tuna kituo cha afya ambacho kilitengewa fedha kwenye Hospitali, kwenye Kituo cha Afya Nanyumbu. Fedha zile hazikuja Nanyumbu, fedha zile kuna mahali zimepelekwa. Uthibitisho wa hili vifaa tiba vikaletwa Nanyumbu; sasa tukawa tunajiuliza vifaa hivi vinakuja kwa hospitali gani? tumeshindwa kuelewa. Kwenye hili naomba Ofisi ya Waziri Mkuu itusaidie. Fedha hizi wamezipeleka wapi kujenga kituo cha afya? kwa sababu tumeletewa machine kwa ajili ya kituo cha afya ambacho hakipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo nawaomba sana, wananchi wapale wanamasikito makubwa kwamba kuna fedha Serikali yao ilileta kwa ajili ya kituo cha afya lakini fedha zile hazikufika na badala yake waletewa mitambo (machine) kwa ajili ya kituo cha afya ambacho hakijajengwa. Kwa hiyo mimi nina imani kwamba hizi fedha kuna mahali zimekwenda kimakosa, naomba huko zilikokwenda zijereshwe ili wananchi wa Jimbo langu wanufaike na huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nijielekeze katika suala la ufundi ndani ya wilaya yetu tuna majengo yaliyoachwa na kampuni ya kichina ambayo walikuwa wanajenga barabara ya kwenda mpakani Mtambaswala. Majengo yale ni mengi na yapo pale ndani ya Kijiji cha Maneme ndani ya Tarafa ya Nanyumbu; majengo yale yangeweza kutumika kikamilifu kwa shughuli ya elimu ya ufundi. Naomba niishauri Serikali, majengo yale yapo pale idle na yanazidi kuharibika ni bora yakatumika kwaajili ya elimu ya ufundi. Uwekezaji wake hautakuwa mkubwa kuliko kuuanza upya. Kwa hiyo naomba sana wizara inayohusika tuyatumie majengo yale ili kufufua elimu ya ufundi ndani ya wilaya yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nazungumzia kwenye kilimo. Mheshimiwa Mwambe amezungumza kwamba kilimo chetu kimeathirika sana, uzalishaji wa kilimo wa zao la korosho umeathirika kutoka tani 324 hadi tani mia mbili na kitu, na sababu kubwa zinajulikana na mojawapo ni mbegu bora ambazo tulitegemea wakulima wazitumie hazikutumika. Kwa maana ya Sulphur I mean pembejeo za kilimo na mambo mengine. Wananchi wa jimbo langu walitumia fedha, walitumia nguvu zao kuzalisha mbegu za korosho ambazo miche ile waliwauzia Bodi ya korosho, lakini huu ni mwaka watatu mpaka sasa hivi hawajalipwa pesa zao...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)