Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Na mimi awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kupata uzima katika siku hii ya leo kuja kuchangia kwenye bajeti hii kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza katika mjadala wangu ambao nataka kuchangia ni ukurasa wa 22 ambao Mheshimiwa Khatib amegusia. Lakini nitagusia katika utoaji wa haki, na hasa katika ujenzi wa mahakama ambazo zinajengwa na utaratibu unaotumika sasa hivi ambao unachangia katika utoaji wa haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na ukurasa huo, nitaunganisha na ukurasa wa 74 mpaka 76 wa hotuba ya Waziri ambapo ameelezea utatuzi wa changamoto za Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza mimi niipongeze Serikali katika kutatua zile changamoto tano za Muungano ambazo zimeelezwa pale, zimefanyiwa kazi, na tunaipongeza na kuishukuru sana Serikali yetu kwa kutatua changamoto hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushiriki wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika kuondosha umaskini, kuna Mfuko wa TASAF unatumika vizuri; kuna Mfuko wa Mazingira unatumika vizuri katika pande zote mbili za Muungano. Sasa kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ukurasa wa 278, katika kifungu 227(c) ambacho kinasema kwamba tutahakikisha masuala muhimu ya Muungano yanaratibiwa kwa faida ya pande zote mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nirudi katika ile miradi. Kuna miradi ya utoaji wa haki ambayo inafadhiliwa au ni mkopo kutoka World Bank. Miradi hii inafadhiliwa na World Bank katika upatikanaji wa haki kwa Tanzania nzima. Na miradi hii inahusisha mkataba ambao ulisainiwa na Mheshimiwa Rais wa dola milioni 65 ambazo ni sawa na bilioni 135, kwa ajili ya upatikanaji wa haki. Nachozungumzia hapa kwamba mgao wa Zanzibari mpaka hivi sasa hivi tunazungumza haujapatikana katika fungu hili, hicho ndicho ambacho hoja yangu ya kwanza niliyotaka kuizungumza. Kwenye bilioni 135 Zanzibar haijaenda hata elfu mbili,

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ikumbukwe kwamba Zanzibar sio mwananchama wa World Bank, mwanachama wa World Bank ni Tanzania na Zanzibar anakuwa kupitia Tanzania naye ni mwanachama kwa hiyo anastahili kupata mgao wake kupitia fungu hili. Na hili nilizungumze katika majukumu ya Tume ya Pamoja ya Fedha ambayo katika Katiba ibara ya 133 na 34 inazungumzia kwamba itakuwa na kazi ya kuchunguza kwa wakati wote mfumo na shughuli za fedha za Jamhuri ya Muungano na pia uhusiano katika masuala ya kifedha kati ya Serikali mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hapo mimi ndiyo kwenye hoja yangu ambapo nazungumzia kwamba kuna fungu lilipaswa kwenda Zanzibar kwa ajili ya kufuatilia utoaji wa haki. Kwa hiyo naishauri Serikali ilifanyie kazi hili. Katika hotuba ambayo Rais wetu mama Samia alivyokuwa anawahutubia mawaziri wakati anawaapisha na Katibu Mkuu Kiongozi alizungumzia changamoto hiyo, kwa hiyo tulikuwa tunaomba ipatiwe ufafanuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la pili, tunazungumzia masuala ya uhusiano wa kimpira, football kuna TFF, TFF inatuwakilisha Tanzania nzima, TFF anapopata msaada wa fedha au ruzuku ya fedha kutoka FIFA inapaswa pia na Zanzibar nao wapate. FIFA kila mwaka inatoa dola 1,500,000 kwa ajili ya maendeleo ya soka Tanzania lakini kwa miaka mingi hakuna hata senti tano ambayo imekwenda Zanziba.

Mheshimiwa Naibu Spika, na Zanzibar hawezi kuwa mwanachama wa FIFA kwa sababu Zanzibar hawezi kujiunga na shirikisho lile la kimataifa. Au, kama inawezekana basi kama hizi fedha haziwezi kugawiwa iruhusiwe na Zanzibar ijiunge kwenye haya mashirika; na kama haiwezi kujiunga sheria haikubali basi huu mgao ufanyike.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna mkataba umesainiwa na Korea Kusini pamoja na Falme za Kiarabu, lakini TFF amesaini peke yake, Zanzibar haiwezi kwenda kusaini mkataba huo. Kwa kuwa haiwezi kwenda kusaini mkataba huo, ilikuwa tuiombe Serikali sasa iiambie TFF kama wao wanaweza kwenda FIFA basi labda na Zanzibari iruhusiwe kwenda FIFA, hilo nalizungumiza hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, linguine ni kuhusu ushirikishwaji wa Timu ya Taifa. Kuna jambo jana nililisikiliza sana nikasikitika sana, na hili nilikuwa naomba Wabunge wanisikilize vizuri. Nimesikiliza maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama kimoja cha upinzani ambayo anasema yeye anawahutubia Watanzania kwamba Watanzania wamsikilize yeye maneno ambayo anayasema.

Nimeisikiliza hotuba yake kuanzia mwanzo hadi mwisho, Lakini kitu, alichokuwa anazungumza ni kana kwamba Watanzania wote wadai haki ya kuchaguliwa kuwa na mamlaka ya kama labda kuwa Rais au kuwa Wabunge. Hakuongea jambo la kijamii hata moja. Sasa Watanzania hawa hawapo kama hivyo, hakuna haki kama hiyo ya kwamba watanzania wote wanahitaji haki moja tu, watanzania wanahitaji haki nyingi. Miongoni mwa haki ambazo Watanzania wanahitaji ni kupata elimu, kupata maji safi na salama, kupata usafiri, maisha yao yawe mazuri, wapate na mambo mengine, sasa haya yote hajagusia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania hawa hivyo leo wanasomeshwa bure hivyo kweli wakatazame haki moja tu? Watanzania wanazunguka kila nchi, watu wa Dar es Salaam pale safari zao wanakwenda vizuri, hivyo kweli ukawashauri Watanzania kwa matakwa yako wewe kwamba wadai haki hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano, mmoja tukienda kule katika Jimbo la Hai kati ya watu 300,000 waliotaka Ubunge ni wawili tu, kwa hiyo wewe uliyekosa usiwashawishi wengine kwamba hii nchi haikutenda haki. Watu hawa wamepatiwa haki katika elimu, afya, usafiri, pamoja na masuala yao chungu nzima ya kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda tuwapeleke darasani, kuna Abraham Maslow’s hierarchy of needs. Katika hierarchy of need cha kwanza ni basic needs, nicho watu wengi wanachohitaji. Hawa wanaohitaji mahitaji mengine ni wachache, kwa hiyo huwezi kuwashawishi Watanzania katika mahitaji haya machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye basic needs kuna elimu, chakula na vitu vingine. Watu wamepatiwa umeme pamoja na mahitaji yao muhimu. Hivi hatuoni umuhimu wa kumuheshimu huyu ambaye aliyefanya hizi huduma za jamii na muhimu zikapatikana?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi maoni yangu kwa Watanzania hawa tuwapuuze na tuwapuuze kama ushuzi wa ngomani, maana ushuzi wa ngomani hata mtu hashughuliki na harufu, tuwapuuze kama ushuzi wa ngomani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana mheshimiwa.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru naunga mkono hoja.