Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyeweza kutukutanisha mahali hapa na hata tukaweza kuanza mfungo siku nzuri hii ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Waziri Mkuu kwa hotuba iliyojaa matumaini na maendeleo kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa mama Samia Suluhu; najivunia kuwa mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuwapongeza sana Mawaziri wote mlioteuliwa kwa kazi nzuri ambayo najua iko katika nafasi zenu ambayo tunakwenda kuitendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba nimeweza kuona mambo mengi ambayo yamesemwa katika hotuba ile ya Waziri Mkuu, kwamba tutakwenda kutekeleza miradi yote ya kimkakati ambayo imepangwa, lakini pia nimeona kwamba yako malengo mazuri ya Serikali iliyoko madarakani bila kusahau kuibua miradi mipya inayokwenda kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende sana pia kuwapongeza sana kwamba tutakwenda kuitendea haki Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Kwamba mengi tumeyaandika katika Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi, na ninaamini kwa jinsi ambavyo tunakwenda, tutakwenda kuiekeleza kwa ukamilifu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado naomba niendelee kuipongeza Serikali yetu, kwamba imefanya kazi nzuri sana katika miundombinu, hasa miundombinu ya barabara kubwa ambazo zimeonekana kila mahali tunakopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza kwamba tumeweza kuunganisha mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya na hata tunafikia sasa kuona kwamba tunapita kwa ujasiri wote tukitaka kwenda katika mikoa fulani fulani bila kuwa na msongamano wala kuwa na makorongo ya namna tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kwamba pamoja na kwamba nawapa hongera kwa kutengeneza miundombinu ya barabara, lakini niseme sasa umefika wakati wa kuona ni namna gani sasa miundombinu ya barabara hizi inakwenda kuunganisha kati ya kata na kata, hata tuweze kuunganisha Kijiji na Kijiji ili tuweze kuona sasa yako mambo mazuri ambayo Serikali yetu imeyafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejengewa zahanati nzuri sana katika kata zetu, tumejengewa masoko, tumejengewa stendi za mabasi, hasa kwetu Dar es Salaam. Lakini kutoka kwenye kata yako kufika kwenye kata nyingine kwa ajili ya kwenda kwenye zahanati au kwenye soko au kwenye stendi ya mabasi, hizi barabara kwa kweli ni tatizo. Hazina mwonekano mzuri. Naamini si kwa Dar es Salaam tu lakini naamini kwa hata mikoa mingine, nasemea kama Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuombe sasa basi, kama kuna namna yoyote ya TARURA kuongezewa au kutafutiwa fedha za kuweza kufanya barabara hizi zipitike, niombe sana Bunge lako Tukufu tuweze kupitisha au tuweze kuona namna gani ya kujadiliana ili tuweze kupata fedha za kuwapa hawa TARURA maana naamini tumeongea nao sana lakini fedha walizokuwa nazo ni ndogo sana kiasi kwamba hawawezi kufanya miundombinu katika barabara zetu zile za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama jinsi mwenzangu jana aliongea kuhusiana na Mradi wa DMDP Mkoani Dar es Salaam, Mheshimiwa Bonnah aliongea vizuri sana, lakini bado naomba nisisitize, kama alivyosema sisi Dar es Salaam tunatamani kulima lakini hatuna maeneo ya kulima. Sasa inapendeza sana kama tutapata Mradi huu wa DMDP ili sasa mafuriko yaliyoko katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam yaweze kukatika na hata tuone kwamba barabara zetu zinaweza kupitika vizuri na vilevile kufanya maendeleo katika kata zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana, pamoja na mambo mazuri ambayo Serikali imefanya. Lakini naomba pia niweze kuona kwamba Jimbo langu la Temeke nilisemee ya kwamba hakika kabisa kata zile 13 tumekaa vizuri, tumepata maeneo mengi mazuri, lakini bado nalilia barabara hizi za ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Temeke wako vijana wengi waliopitia JKT na vilevile walikwenda katika huduma ile ya kujenga ukuta ule wa Mererani lakini pia waliweza kuingia katika kujenga ukuta wa ikulu. Lakini sasa hivi wamerudi na makaratasi tu ya kwamba wamehitimisha kufanya yale mambo lakini tunapokwenda kuomba ajira, vijana wetu hawa wa JKT hawaangaliwi wala hawapewi chochote kwenda kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa Serikali yako kwa usikivu kabisa waangalie basi hizi hatma za vijana wetu ili waweze kupata kazi maana ndiyo hasa tunaowategemea katika kipindi kijacho, sisi tunakwenda kuzeeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Temeke tuna tatizo kubwa sana la umeme kukatika kila wakati. Umeme huu sasa sijui umekuaje, mwenzangu wa Mbagala aliliongelea hili. Nami niseme, hata sasa hivi hapa nina meseji ambayo tayari umeme umekatika, kwetu Temeke imekuwa ni salamu sasa hivi kwamba ikifika asubuhi lazima ukatike ama saa mbili au saa tatu au saa nne. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sioni namna gani ambavyo TANESCO watatusaidia ili tuweze kupata umeme kama wenzetu. Na ukizingatia sana kwamba Jimbo letu la Temeke tunayo miradi mingi ya wafanyabiashara na makampuni mengi ya uzalishaji ambayo yanazalisha kupitia huo umeme ili hata sisi wenyewe kama manispaa tuweze kupata fedha za ndani katika makusanyo ya viwanda hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kuunga mkono hoja, lakini niombe haya niliyoyasema tuweze kuangaliwa na kutimiziwa. Ahsante sana. (Makofi)