Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu. Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Timu ya Simba Sports Club kwa ku-qualify kuingia robo fainali ya Club Bingwa Afrika, lakini pia niwapongeze waliokuja na lile wazo la visit Tanzania kwasababu pia inasaidia katika kutangaza utalii. Niwashukuru pia wenzetu wa Yanga sasa hivi wanatushangilia kwasababu pia wao mwakani, kwa namna moja au nyingine Tanzania itapata nafasi nne, kwa hiyo nao watapata nafasi ya kushiriki. Kwa hiyo nawashukuru sana; lakini pia nawatahadharisha Simba, kwamba hawa hawa wanaotushangilia leo kesho wanaweza wakatuzomea, kwa hiyo tuwe carefully.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi, tumeona katika Taifa letu wapo watu ambao; jana Mheshimiwa Kibajaji alisema vizuri sana, Mheshimiwa Msukuma alipendekeza; kwamba ikimpendeza mamlaka Mheshimiwa Lusinde apate doctorate ya heshima. Mimi kwa binafsi yangu na kwa mamlaka yangu mimi mwenyewe binafsi tayari Mheshimiwa Kibajaji huwa ninamwita professor, nilishampa professorial kwasababu zangu binafsi na pia kwasababu katika uwanda wa siasa na ujengaji wa hoja kwakweli yupo vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupata msiba wa mpendwa wetu Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli nilikuwa naongea na Mheshimiwa Kibajaji, kwamba tuombe sana Mungu; kibajaji akaniambia maana; yeye huniita mimi tena professor sijui kwa nini, kwasabau zake binafsi. Lakini akasema utakuwa unakosea yako ya Mungu halafu yako ambayo sisi lazima tuwajibike kwamba hatuwezi kufanya mambo ya kijinga kijinga alafu tunasema tuombe Mungu, hapana. Yapo ambayo tunatakiwa tuombe Mungu, na yapo ambayo sisi kama binadamu tuna sehemu yetu ya kuyafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tulimuona juzi kwenye ziara kule kwenye mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere, lakini pia kumpongeza Mheshimiwa Rais Amini Jeshi Mkuu tulimuona Uganda akishuhudia kutia saini kwa makubaliano yale na kuanza kutekeleza kwa bomba la mafuta. Yote yale ni katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na kwamba kazi iendelee. Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake amezungumza mambo mengi lakini moja wapo ni jambo la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali langu namba 16 kwenye Bunge lililopita niliuliza kuhusu lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara za lami katika Mji wa Mafinga. Ili kuendeleza sekta nzima ya uchumi wa viwanda ili kupiga hatua na kukuza ajira zaidi ya milioni saba ambazo tumeahidi katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi Ukurasa wa 29 moja wapo ya nyenzo muhimu ni ujenzi wa miundombinu hususan ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninatoka Mafinga, mara zote nimesema, na Mheshimiwa Pacha wangu David Mwakiposa Kihenzile amesema juzi, kwamba bila ujenzi wa miundombinu ya barabara hasa maeneo ambayo yanauzalishaji mkubwa kiuchumi hatua yetu ya kupiga kasi ya uchumi itakuwa ndogo. Kwa hivyo mimi ninapendekeza na kuishauri Serikali, tutakapokuja kujadili suala la TARURA tuone namna ambavyo tutaiwezesha TARURA ili kusudi tuweze kuweka misingi imara katika ujenzi wa miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ninapozungumza kuna watu wanasema ukiongeza labda shilingi 50 kwenye lita moja ya mafuta utaongeza gharama za usafiri. Gharama za usafiri haziongezeki kutokana na gharama za mafuta isipokuwa kutokana na barabara mbovu ambazo hazipitiki mwaka mzima. Ikiwa tuna barabara zinapitika mwaka mzima hata gharama za nauli haziwezi kuwa kubwa na wala gharama za usafirishaji haziwezi kuwa kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kutoka Mafinga kwenda Sawala umbali wa kilometa kama 40 nauli kipindi cha mvua inafika mpaka elfu 10,000 - 15,000, lakini umbali huo huo kutoka Dodoma kwenda Iringa ambao ni umbali wa kilometa zaidi ya 260 nauli haizidi elfu 10,000. Kwahiyo gharama za usafirishaji zinaendana sana na hali yetu ya miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kutoka Mafinga kwenda Mtwango kwenda Ifupila baadhi ya magari yamepaki hayawezi kwenda kwasababu mbali ya ubovu wa barabara lakini pia inachangia gharama kubwa za matengenezo ya magari. Kwa hiyo mimi niombe sana, pamoja na kuutazama Mji wa Mafinga tuangalie Barabara ya Mafinga kwenda Mgololo, Barabara ya Mtwango kwenda Nyororo kwasababu inabeba uchumi mkubwa wa Wilaya ya Mfindi Mkoa wa Iringa na nyanda za juu kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema haya si kwamba tunazungumza kama luxuriously, hapana, tunasema hivi ili kusudi ku-bust kasi ya ukuaji wa uchumi. Leo hii ukienda Barabara ya Mafinga - Mgololo unakuta semi- trailer 10 zimepaki kwa muda wa wiki, haziwezi ku-move; maana yake ni kwamba tuna slow speed ya ukuaji wa uchumi na hata zile ajira milioni nane tulizozisema katika Ilani hatuwezi kuzi-realize kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilio changu kikubwa mimi leo ni kuhusu barabara. Kama tutaweza kuwekeza nguvu katika ujenzi wa barabara hususan maeneo hayo ambayo yana uchumi mkubwa maana yake tuta-speedup ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili napenda kusema, dunia leo hii ndugu zangu inafanya kazi 24/7 saa 24 siku saba. Jana nilikuwa na swali lini Serikali itaruhusu baadhi ya miji hasa ambayo iko kando ya barabara kuu kama vile Mlandizi, Chalinze, Morogoro, Mikumi, Ruaha Mbuyuni, Ilula, Ifunda, Mafinga, Makambako watu hawa wajiachie wafanye biashara saa 24, ajira ziko rasmi za Serikali lakini ziko za vijana kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi Mafinga pale inapofika saa nne Polisi wanapofika na kutaka vijana wafunge biashara wakati vijana hawa mchana kutwa walikuwa msituni wakiitafuta shilingi, tutakuza vipi uchumi? Kwa hiyo, nashawishi Bunge hili na Serikali tuangalie baadhi ya maeneo ya miji kama hiyo niliyoitaja na mingine miji kama Korogwe na Mombo kwa shemeji zangu, watu wajiachie wafanye biashara. Duniani kote kazi ya dola ni ulinzi na usalama, wao wa-guarantee vijana wajiachie wafanye biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini masuala ya saa tano kuanza kukimbizana na vijana wafunge biashara zao ambao mchana kubwa walikuwa wanatafuta kipato chao, mimi kwangu naona siyo sahihi na hili kwa kweli siwezi kukubaliana nalo. Ndiyo maana nikasema kwa mujibu wa utaratibu wa Serikali ziletwe hapa sheria tuweze kuwezesha maana kazi ya Serikali ni ku-facilitate.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake amezungumzia kuhusu sekta ya michezo na amesema contribution ya sekta ya michezo kwenye pato la Taifa ni 3% tu kati ya 2013 mpaka 2019. Pia ameeleza kwamba sekta hii inaajiri vijana wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina mambo mawili; kwanza ili tunufaike na Media Entertainment and Sports Industry kama siku zote ambavyo huwa nasema hatuna namna lazima tukiangalie kwa macho mawili Chuo cha Michezo cha Mallya na Taasisi ya Sanaa ya Bagamoyo - TaSUBa, ili kusudi tuweze kuwezesha vijana na nyenzo mbalimbali za masuala haya ya michezo, burudani na utamaduni.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili lazima tuangalie pia viwanja. Sasa hivi unakuta kwamba kiwanja kama cha Jamhuri kama tuna tamasha labda la Fiesta sijui Mziki Mnene la Wasafi au Mtikisiko unakuta matamasha haya yanafanyika katika viwanja vya mpira. Ni ushauri wangu kwa Serikali tujenge uwanja wa Standard Olympic ambao utakuwa kama One Stop Center; viwanja vya kuogelea, table tennis na kila aina ya michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia lazima tufike wakati tuhamasishe wawekezaji wawekeze katika majumba makubwa na viwanja maalum ambavyo ni kwa ajili ya masuala ya burudani. Kwa sababu as it is leo utakuta uwanja pale wa Taifa kuna tamasha iwe la muziki wa injili, iwe la muziki wa kimataifa yote yanafanyikia pale. Kwa hiyo, ama kupitia wawekezaji ama namna yoyote ambayo Serikali itaona inafaa kama tunataka tunufaike na sekta ya michezo na burudani lazima tuangalie Chuo cha Michezo cha Mallya na Taasisi ya Sanaa ya Bagamoyo lakini lazima tuwekeze katika miundombinu wezeshi ya kuwezesha vijana hawa kuwa na maeneo ya kufanyia hizi kazi zao. Michezo sanaa na burudani inaajiri vijana katika ajira isiyo rasmi siyo chini ya milioni 2 na huu ukuaji wa teknolojia ya sayansi na teknolojia kwa maana ya matumizi ya internet, inaleta sana ukuaji wa uchumi katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja nikisisitiza tufanye kazi saa 24 siku saba, ahsante sana. (Makofi)