Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kwa kuteuliwa kuwa Rais wetu wa Awamu ya Sita, lakini pili nikushukuru wewe kama mlezi wetu sisi Wabunge, najua na sisi tulipoanza humu tuliitwa vijana, lakini naona sasa tunaenda tunazeeka-zeeka kwa sababu umesajili vijana wengine, Mungu akubariki sana.

Mheshimiwa Spika, lakini nimpongeze sana Katibu Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Bashiru, tunakushukuru sana. Kwa sisi tuliosota CCM tunatambua mchango wako Mheshimiwa Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri uliyoifanya. Umeweza kutuunganisha Wabunge wote pamoja na Serikali yako unayoiongoza, lakini pamoja na Mawaziri unaowasimamia.

Mheshimiwa Spika, nitaanza kushauri upande wa kodi, nimezungumza humu zaidi ya mara mbili mara tatu nikiomba Serikali ione namna ya kuweza kukaa na wafanyabiashara, ili kuweza kuona jinsi nzuri ya watu walipe kodi bila kuichukia Serikali na bila kuwa maadui na wataalamu wetu wa TRA. Lakini mara nyingi mawazo mazuri tunapoyatoa sisi kwa kuwa ni darasa la saba, yaani tukitoa wazo, yaani kabla hamjalielewa ninyi wasomi mnalibeba linakuwa la kwenu wakati utafiti umefanywa na watu wengine.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka nishauri, tunajua kwamba, Mheshimiwa Waziri amepewa maagizo na Mheshimiwa Rais kwamba, nendeni mkarekebishe TRA, hawawezi kurekebisha. Na mimi nikuombe kwenye hili hata Waziri tunamvalisha kengele ambayo hawezi kuicheza. Ningeomba Mheshimiwa Rais awaite wafanyabiashara, suala hapa sio harassment, suala hapa ni kodi ambazo ni za miaka 25 ya nyuma. Kwa maisha ya sasa inabidi tubadilishe kulingana na hali halisi, ukisema tu wasitusumbue bado wanakuja na mavitabu yaleyale, kilichobadilika wamekuwa tu na ka-lugha, tunaomba utulipe, wameacha kufunga yale makufuli, lakini kodi ni ileile.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningeomba ni vizuri Mheshimiwa Rais akawaita wafanyabiashara akakaanao, kama tulivyofanya kwenye madini, wamwambie hiki kinatukwaza, hiki kinatukwaza, aone namna aseme nendeni mkabadilishe hili. Kama hatutabadilisha hakuna namna ambayo mtamsaidia mfanyabiashara wa Tanzania bado mateso ni yaleyale na ninadhani ndio kama rushwa itaongezeka japokuwa haitaombwa kwa ukali, itakuwa ni ya maelewano tutoe kidogokidogo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri mawazo haya mkayafanya yawe endelevu muwaite wenye matatizo. Ninyi wengi huku mnaoelekezwa mnakaa ofisini, hamjui huko field watu wanavyoteseka. Kwa hiyo, ningeshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu ni vizuri Rais akawasikiliza wafanyabiashara ndio hub yetu kwenye nchi yetu. Baada ya kuwasikiliza aone namna ya kitu gani na kitu gani tutakachokiondoa, ili wafanyabiashara wawe na amani na walipe bila kusumbua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa mfano; leo ukienda Kariakoo utakuta watu wamekimbia wale wafanyabiashara, nakupa mfano mdogo tu wa glasi. Glasi ina aina kama sita, kuna glasi inauzwa 200/= tunatumia kule kwetu kijijini, kuna ya 1,500/= wanatumia Wagogo, kuna 15,000/= wanatumia Dar-es-Salaam, ukienda kwenye kodi tariff inayotajwa ni ushuru wa glasi. Inawezekanaje ushuru uni-charge 2,000/= wakati glasi inauzwa 1,000/=? Kwa hiyo, ni vizuri tukawa na uwanja mpana wa kuweza kuwasikiliza hawa wafanyabiashara ili muweze kukusanya kodi bila kusumbuana na bila kuwalaumu watu wa TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, napenda nishauri kwenye upande wa tanzanite. Maisha yangu nimekulia kwenye madini ni vizuri wakatusikiliza watu tunaotoka kwenye madini. Huwezi ukasema tanzanite inatoroshwa, na sisi kama kamati tumeenda kwenye tanzanite pale Mererani, kwa kweli Serikali imefanya kazi kubwa sana na askari wetu wako pale wanalinda vizuri na kamera. Tumeingizwa chumba cha kamera unaona mita 50 nje mita 50 ndani ni ulinzi ambao unajiuliza sisi watu wa dhahabu tungepewa huo ulinzi pengine Serikali ingekusanya mara tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka nishauri mnaibiwaje Serikali. Unaweza ukalaumu wanajeshi, unaweza ukalaumu wizi uko pale, naomba nitoe mfano; tangu mpate lile jiwe la Laizer lile lililotangazwa kwenye TV la bilioni sita mkatoza kodi, halafu mkapeleka ma-valuer mkaweka na askari na askari na askari, kama aina tatu za maaskari wako pale na watu kweli wanapita kwenye geti. Niwaulize swali, ni lini toka mmepata jiwe la Laizer ni lini mmepata tanzanite ambayo imezidi milioni thelathini, arobaini? Ni kwasababu, nyie mkipewa mawazo kabla hamjayafanyia kazi mnapeleka utaalamu. Sasa watu wanawapigia chenga palepale na tochi yenu mnamulika pale.

Mheshimiwa Spika, ni watu wanazunguka na wale vijana wa tochi pale. Hatuna sababu ya kutumia akili nyingi ya degree tu. Mnaona degree zinatufelisha, naomba nikupe dawa moja ndogo tu; kesho Serikali iwe na hela pale waweke vijana wa darasa la saba tu wanaojua mawe, tunahitaji tochi wala sio binocular hiyo mnayotumia pale, muwaweke pembeni pale hawa ma-valuer wenu wenye degree wapimee wakifika mwisho wakisema hii ni milioni 30 muwape wale vijana wa darasa la saba wachungulie wawaambie kama ni 30 mpe mara moja muone kama hawatayakimbia mawe pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnapigwa chenga palepale na askari wenu wako pale. Kwa hiyo, ni vizuri wataalam mtutafute tuwape madini, msione aibu kufundishwa na darasa la saba tumekulia huko, nyie field yenu mmesoma miezi mitatu sasa sisi tumekulia kulekule. Kwa hiyo, ni vizuri msishikane uchawi wowote wizi mnapigwa na makamera yenu yako pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nishauri pia, nchi kama Tanzania tuna ma-valuer wasiozidi kumi na moja, kumi na tano, ni aibu. Kama tuko serious chukueni wanajeshi hata 100 ni miezi sita tu kujifunza u-valuer kwa nini tuwe na watu kumi na moja, kumi na mbili? Walewale wanazungumza, ukizungumza na huyu akimaliza deal biashara imeisha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana ushauri wangu hawa wataalamu waweze kuufanyia kazi, lakini nataka nizungumze kuna mtu mmoja msomi humu mtaalamu Profesa alizungumza juzi akasema dhahabu hatujafanya vizuri. Nimekulia Geita, wakati wa utawala wa Mhesimiwa Profesa Muhongo wachimbaji wadogo mwaka 2015 tulikusanya gramu 120, 2016 wakati tumeanza kuruhusu wachimbaji wadogo baada ya kupokelewa mawazo yetu tumekusanya 337,000 gramu kwa mwaka, 2017, 800,000, 2018,6 1,600,000, 2019 4,000,000, na 2020 5,000,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunahitaji kuwa na maprofesa wa design hii? Hata kama hatujui kusoma, hatuoni haya maandishi hapa ndani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vizuri mtu anapofanya kazi nzuri tusitengenezeane ajali lazima apewe sifa. Hongera sana Waziri wa Madini, umefanya kazi nzuri wala hutuhitaji kupata degree hapa, tunajumlisha hesabu tunajua kutoka gramu 120 leo tuko milioni tano halafu mtu anasimama hapa anaanza kubeza. Nakumbuka maneno ya mtu mmoja nikiwa sio Mbunge, alikuwa anakaa pale nikimuangalia kwenye TV anaitwa Mheshimiwa Kigwangala, alimwambia binafsi hajawahi kuona Profesa muongo kama Mheshimiwa Muhongo kwa sababu… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Musukuma namlinda Mheshimiwa Mbunge Profesa Muhongo. Sijui yupo humu ndani?

MBUNGE FULANI: Hayupo.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, atapata taarifa.

SPIKA: Nadhani ametoka kidogo? (Kicheko)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, univumilie kidogo ninazungumza kwa uchungu. Mwaka 2016 Mheshimiwa Profesa Muhongo akiwa Waziri nimemuita Geita kumwambia Waziri tunaibiwa; hadharani kwenye mic, tunaibiwa haya makinikia wakipakia humu kuna dhahabu.

Mheshimiwa Spika, Profesa alishika mic ananiambia wewe ni darasa la saba, nyie watu wa Geita mlikosea kuchagua mtu wa darasa la saba. Tukamchenga Profesa, dakika moja Mheshimiwa nimalizie hoja yangu, tukampelekea marehemu Mheshimiwa Magufuli kamfuko tu kadogo tukamwambia Mheshimiwa hatuhitaji Profesa, naomba utusimamie tuoshe haka kamfuko tu kadogo tukaoshea na Coca-cola.

Mheshimiwa Spika, dakika 15 tulikuwa na dhahabu ya milioni 16, Mheshimiwa Dkt. Magufuli akawakia na kwenye gia. Sasa maprofesa wa design hii watatuchelewesha ni vizuri mtuiamini na sisi LY tunaumia, tunatumia nguvu kuwapa material halafu wanakuja wanapotosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)