Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Pia nishukuru wananchi wangu wa Jimbo la Arumeru Magharibi.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira tuliyonayo ya kuchangia bajeti hii tunaamini kwamba bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu inakwenda kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2021/2022, ndiyo maana hapa tumeanza mchakato huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea ningependa sana kusema maneno machache kabla sijachangia. Nitumie maneno ya Mungu, wakati ule Yesu alipokuja duniani kwa ajili ya kuokoa dunia alikuwa na wanafunzi wake 12. Katika wale wanafunzi, Yesu alitabiri kwamba kuna wawili watakaomsaliti, alikuwa ni Petro na Yuda Iskariote. Alipokuwa pia akiendelea alijaribiwa na shetani sana akampandisha juu ya mlima mkubwa sana akamwambia ukinisujudu nitakupa dunia hii yote itakuwa ya kwako na miliki zote, lakini Yesu akamwambia rudi zako nyuma shetani kwa sababu miliki yote hii ni ya kwangu.

Mheshimiwa Spika, nayasema hayo, lakini pia alipokuwa akiendelea alikutana na watoza ushuru, wakamuuliza sisi tufanye nini Bwana? Akawaambia na ninyi mtosheke na mishahara yenu. Nimeona nianzie na hapo. Nasikitika sana, Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambaye aliinadi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa nguvu zake zote na nia yake yote na moyo wake wote, leo tunapata akina Yuda. Leo kina Yuda wamejitokeza kumsaliti Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano. Inasikitisha, mzee wa watu ametangulia mbele ya haki, hawezi kujitetea, lakini ninyi mlioko ndani na nje mnataka kumdhalilisha. Hakika, asilani kabla hamjamdhalilisha Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano, nina hakika Mwenyezi Mungu atawashughulikia usiku na mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Magufuli alifanya kazi ya kuwaaminisha Watanzania kwamba kweli ni Rais anayejali maskini, anayejali Taifa hili kama alivyokuwa mtangulizi wake Rais wa Serikali ya Kwanza Nyerere alifuata hizo nyayo na Serikali zote zingine zilizofuata alionesha njia kubwa. Alipokuwa akitunadi, niliumia sana ninapoona kwenye mitandano watu wanachafua hali ya hewa Magufuli hata panya akitoboa gunia kule nyumbani kwa mtu, Magufuli! Kwa sababu yeye hayupo. Kama kuna watu wamefanya ufasadi kwenye Wizara, Bandari na halmashauri watu wanasema Magufuli, kawatuma? Nasikitika sana, lakini Mwenyezi Mungu atawashughulikia kabla ya siku zao si nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, akina Yuda hawakosekani, lakini nawaambia ninyi ambao mnadhani mtaishi milele hakuna nafsi, kila nafsi iliyoko hapa kwenye Bunge hili na nje ya Bunge hili itaonja mauti. Hakuna anayedumu milele wala hatuna mji udumuo katika dunia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, mama Samia Suluhu Hassan alikuwa ni msaidizi wa Dkt. John Pombe Magufuli na Mheshimiwa Rais wetu wa sasa mama Samia Suluhu Hassan alikuwa mwaminifu na muadilifu na ndiyo maana Mwenyezi Mungu amemuona akawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mtaona jinsi gani mama yule, Rais wetu mpendwa amehakikisha kwamba wale waliokuwa wanatazamia kwamba atabadilisha Serikali kwa asilimia sijui ngapi, amesema “Kazi Iendelee”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tusifikiri kwamba kwa mwelekeo huo Mheshimiwa Rais aliyeko ataweza kumsaliti Magufuli. Legacy ya Magufuli itaendelea kubaki sasa na hata milele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa niendelee kutoa mchango wangu. Najua kabisa Chama Cha Mapinduzi katika kutekeleza Ilani ya Mwaka 2020/2021 imefanya kazi kubwa na hakuna mtu asiyejua, hakuna asiyaona. Kwenye dispensary tumefanya vizuri Chama Cha Mapinduzi, kwenye bandari, kwenye reli, kwenye masuala ya hospitali na kadhalika. Barabara nchi hii ni kubwa lakini imetekelezwa Ilani kwa asilimia 90 kuunganisha mikoa yote ya Tanzania. Hakuna ubishi na anayebisha hapa asimame, hii nchi ni kubwa, hata kule Roma, Mji wa Baba Mtakatifu unajengwa mpaka leo wajenzi wapo wanajenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakwenda kwa ajili ya kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2021/2022, sasa ni kazi yetu kuikumbusha Serikali kwamba kuna upungufu ule mdogo mdogo yaliyoko kwenye vijiji, kata, wilaya na kwa ujumla kwenye mikoa. Ni wajibu wa Serikali yetu kwenda kutekeleza kwa kutumia bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la ahadi ya Waheshimiwa Viongozi wetu Awamu ya Tano, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne. Awamu ya Tano ambayo kwa sasa ndiyo iliyoongozwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi barabara za lami kwenye majimbo yetu, aliahidi kutengenezwa hospitali, ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu yeye tunamuamini na tunamwona ni mchapakazi, yeye ndiyo anasimamia shughuli za Serikali Bungeni, hebu sasa Serikali ije na mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba hizi ahadi ambazo Waheshimiwa Marais wetu wanatoa, Waheshimiwa Mawaziri wahakikishe kwamba wameweka kwenye bundle moja ili iweze kutekelezwa kikamilifu na iweze kuwepo katika reference. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala la ahadi linasumbua sana wananchi kwa sababu wanasema Rais ametuahidi kila siku anasema Mbunge wakumbushe, wakumbushe. Sisi ni wajibu wetu kama Wabunge kuikumbusha Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi na imefanya kazi kubwa, imetekeleza ahadi nyingi imepungua hizo ndogo tu, lakini ningeomba ingewekwa kwenye bundle moja ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye jimbo langu Awamu ya Nne iliahidiwa barabara ya Hospitali ya Oturumeti, hospitali ya wilaya kwa lami. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameahidi barabara ya Mianzini – Kimbolo –Ngaramtoni; barabara iliahidiwa na Mheshimiwa Jaffo, barabara ya kwenda Hospitali ya Nduruma, Bwawani na katika majimbo mengine yote Tanzania. Najua hii nchi ni kubwa, lakini ni wajibu wetu kuendelea kuikumbusha Serikali yetu tukufu na sikivu kuhakikisha kwamba imeondoa hizo ahadi za Waheshimiwa Marais wetu.

Mheshimiwa Spika, suala la ajira; kama tunavyojua Serikali inajitahidi, sasa niombe ijitahidi sana kuboresha katika Sekta Binafsi na kwa ajili ya kupata mazingira mazuri ya kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa ili vijana wetu ambao wanahangaika huku na huku waweze kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kilimo; kuna mashamba makubwa yametelekezwa kama mashamba haya yangeweza kuchukuliwa na Wizara ya Kilimo wakaunganisha kama wale ma-settler walivyokuwa wanalima kahawa, maharage, mahindi, ingeweza kuleta tija na ajira. Bado naamini kwa sababu Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu itaendelea kuchapa kazi na kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanafanya kazi vizuri. Kwa mfano kwenye Jimbo langu, kuna mashamba makubwa kama ya Aga Khan, imechukua mwaka 2006 ikisema itajenga Chuo Kikuu, zaidi ya heka 3,000 hadi leo shamba hilo limesimama, lilikuwa linaajiri zaidi ya watu 1,500, lakini naamini Wizara ya Ardhi itaekwenda kufuatilia shamba hilo ili kujua hatma yake.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuchangia katika ardhi na ajira, kuna suala la Mfuko huu wa Akinamama, Vijana na Wenye Ulemavu. Naomba Wizara husika ije na mpango mahsusi wa kuboresha Mfuko ule ukae vizuri kwa sababu, hivi sasa kuna utata mkubwa katika mfuko huo, watu wanaopata mikopo ni 18 – 35, lakini utaona ni jinsi gani bado watu wa age hiyo wako shuleni. Sasa ni vizuri wakaja pia na marekebisho kama itawezekana wakanzia 18 mpaka angalau 40, hapo utapata watu wengi ambao wataongea uchumi na wataanzisha biashara.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)