Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii. Nianze kwa kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao kwenye Sekta ya Viwanda na Biashara ambayo kwa kweli ilikuwa mingi na imekuwa hivyo kwa sababu Mpango wenyewe kwa kweli ukiangalia malengo 12 ya Mpango wa Maendeleo ambao tumeujadili hapa, malengo sita yanahusu Sekta ya Viwanda na Biashara. Mule ndani kuna hatua 116 za kiutekelezaji. Zaidi ya theluthi moja tu, 54 zinahusu Sekta ya Viwanda na Biashara. Kwa hiyo, naelewa kwa nini michango imekuwa mingi.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu ya muda, naomba nichangie tu jambo kubwa ambalo limejitokeza, ambalo nawe umelisisitiza; na nipanue pale Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji alipoishia kuhusu suala la utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara, maarufu kama Blueprint, ambao unalenga kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, kwenye mpango huo kuliibuliwa changamoto nyingi ambazo zinakwamisha mazingira ya biashara na uwekezaji, lakini unaweza kuzigawa changamoto hizo katika maeneo 11 ambayo tunayafanyia kazi. Ningetaka kuleta taarifa kwenye baadhi ya maeneo ili kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Nataka nitolee taarifa maeneo manne ambayo ni ya msingi sana. Moja sitalizungumza kwa sababu Mheshimiwa Mwambe ameshalieleza kuhusu suala la tozo, ada na adhabu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, kwenye mpango huu iliainishwa kwamba tozo 45 ziliainishwa kama ni tozo za kero; na ziondoke; na zilifutwa. Ukiacha hiyo, tulienda mbali zaidi, zimefutwa jumla ya tozo 273 kama ambavyo Mheshimiwa Mwambe ameeleza. Kwa hiyo, ni hatua kubwa na hii ilikuwa ni moja ya kero kubwa sana ambayo iliainishwa kwenye changamoto za kufanya biashara.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, ilikuwa eneo la utungaji wa sheria na uboreshaji wa sheria na kanuni mbalimbali. Hapa zilitambuliwa sheria na kanuni 90 ambazo zinakwamisha mazingira ya biashara na uwekezaji. Tayari sheria na kanuni 11 zimefanyiwa kazi, pia tumeweka misingi 10 ya kuzingatia katika kuboresha sheria hizo.

Mheshimiwa Spika, kama baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanavyofahamu, baadaye ilikuja kuonekana kwamba kuna haja ya kuwa na sheria moja ambayo ni kubwa, inayozungumzia biashara. Kwa hiyo, tuko katika mchakato ndani ya Serikali kuja na Muswada wa sheria ambao kwa sasa unaitwa Business Facilitation Act ambao utajibu changamoto nyingi za Sheria ambazo ziliainishwa hapa.

Mheshimiwa Spika, suala la tatu lilikuwa ni kuweka mfumo wa electronic. Hapa Waheshimiwa Wabunge wengi wanafahamu kwamba, ndani ya Serikali mifumo mingi ya electronic imeanzishwa kutokana na utekelezaji wa mipango hii ikiwemo GePG, BRELA, TBS, TIC, TMDA, kokote kule kwa sasa wanatumia mifumo. Wengi wanafahamu ukitaka sasa hivi kusajili Kampuni, huhitaji kwenda physically kwenye ofisi, una log in tu kwenye mfumo.

Mheshimiwa Spika, ya nne na hii ni kubwa ni suala la uanzishwaji wa vituo vya pamoja vya kutoa huduma. Vimeanzishwa ndani ya TIC, EPZA na mipakani. Nitoe taarifa pia hapa kwamba hatua inayofuata ni kuanzisha vituo vya kutolea huduma, yaani One Stop Service Delivery Center kwenye ngazi ya Halmashauri. Bahati nzuri tayari tumepata grant kutoka Umoja wa Ulaya Euro million 9.5. Hizi zinakwenda kujenga vituo vya One Stop Center kwenye ngazi za Halmashauri ili sasa kuja kwenye Halmashauri, badala ya mtu kwenda TRA, BRELLA na TBS, anaenda sehemu moja, anapata huduma zote kwa wakati mmoja. Tunaamini hili litakuwa ni mkombozi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka tu niseme kwamba utekelezaji wa Blueprint unaendelea vizuri, tutakachofanya ni kuimarisha utoaji wa taarifa, nasi ambao tumeteuliwa na Mheshimiwa Rais hivi karibuni, tutaongeza kasi zaidi ili kuona kwamba, utekelezaji unakwenda vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nitoe taarifa, ilitolewa hoja hapa kwamba viwanda vyetu vya mafuta vinavyo tu single refinery. Hii siyo kweli. Ninayo orodha hapa ya zaidi ya viwanda 20 ambavyo finafanya double refinery. Nami nataka kushauri Waheshimiwa Wabunge, Wazungu wanasema, extra ordinary claim, demands extra ordinary evidence.

Mheshimiwa Spika, sasa ukitoa hapa claim ambazo ni kubwa, kwa sababu inataka kuonekana kana kwamba Tanzania mafuta ambayo tunatumia kule hayana ubora unaostahili, hapana. Mafuta yetu inajulikana kwa vipimo vyote kwamba ni mafuta bora sana ambayo tunazalisha hapa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka kulitolea maelezo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, ni miradi ya kielelezo ambayo imetajwa hapa Mradi wa Chuma cha Linganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma. Nataka tu niseme mradi huu ni miongoni mwa miradi 17 ambayo ipo katika miradi ya kielelezo na kwa kweli ambacho kilichochelewesha na nilitolea taarifa mwezi Februari ni kwamba tutaleta taarifa kamili katika Mpango…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: …na katika bajeti ambayo tutakuja nayo mwezi Mei.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)