Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO NA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nami kuchangia Mpango huu wa Maendeleo ambao ulikuwa unajadiliwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia katika suala zima la Wizara ya Ardhi kwenye Mpango; ni Wabunge watatu ambao wamechangia. Ninachotaka tu kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge ni kwamba Wizara, inatambua wazi ya kwamba ardhi ni mali, ardhi ni mtaji, ukiitunza itakutunza.

Mheshimiwa Spika, vile vile katika suala zima la Mpango wa Maendeleo ambapo pia tunasema Tanzania inakwenda kwenye Sekta ya Viwanda na zaidi, tuko tayari; na ukiangalia kwenye ule Mpango kipengele cha 5.4.23 tumeainisha yale yote tunayokwenda kufanya.

Mheshimiwa Spika, tumeweka kipaumbele zaidi katika kupanga, kupima na kumilikisha, kwa sababu usipoipanga ardhi vizuri, utakuwa umekwamisha sekta nyingine zote katika suala zima la kimaendeleo, nasi tunatambua kwamba ardhi inahitaji kupangwa, kupimwa na kumilikishwa. Ni wazi mpaka sasa hivi hatujafikia asilimia kubwa, ni kama alimia 25 tu. Waheshimniwa Wabunge wameongelea hapa kwamba, ikiweza kupangwa vizuri na ikapangiwa matumizi, ni wazi inaweza ikakusanya kodi nyingi za kutosha. Ni kweli hatukatai hilo, lakini kama Wizara ndiyo maana mnaona kwamba Ofisi za kimikoa zilifunguliwa.

Mheshimiwa Spika, kuna Mbunge amependekeza suala la agency, ni wazo zuri, lakini kama tutatumia vizuri ofisi zile za Mikoa na Halmashauri ambazo ndiyo Mamlaka za Upangaji Miji zikaweza kukijikita katika kuweka mpango mzuri kama ambavyo upo kwenye suala zima la kutenga bajeti za kupima maeneo yao, hatutahitaji suala agency kwa sababu kila Halmashauri inao wataalam. Kila Halmashauri ikiweka kipaumbele, itaweza. Kama Wizara, katika siku za nyuma tumetoa baadhi ya pesa katika Halmashauri na wamefanya vizuri katika upangaji.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia suala la Mbeya, Kahama, Bariadi na Ilemela, walipewa fedha na wamefanya kazi hiyo nzuri. Kwa hiyo, tuna Imani, mbali na bajeti zinazokuwa zimewekwa na Halmashauri zenyewe, lakini wakiwezeshwa kidogo na Wizara, tunawasukuma kuweza kufanya kazi yao vizuri. Kwa hiyo, kama Wizara, tunaliona hilo na tunalizingatia.

Mjheshimiwa Spika, kuna suala lingine ambalo limeongelewa kuhusu kuwa na Sera ya Nyumba pamoja na Sera ya Makazi. Kama Wizara, tuko katika mchakato na tutaleta nakala kwa Wabunge ili muweze kuongeza input, kwa sababu tayari ile rasimu ya mwanzo imeandaliwa ambayo tunahitaji sasa tupate input za Waheshimiwa Wabunge kwa undani zaidi ili tuweze kutoka na final product itakayoweza kukidhi mahitaji na tutaondokana na haya malalamiko ambayo mara nyingi yanatokea.

Mheshimiwa Spika hata ile ya Real Estate Regulatory Authority nayo pia iko kwenye mchakato mzuri. Tumekuwa na madalali wengi hapa katikati na unakuta watu wengi wanadhulumiwa ardhi. Unaambiwa kuna ardhi ya uwekezaji hapa, lakini anayekwambia ni Middlemen mwisho wa siku unajikuta huwezi tena kupata ile ardhi. Kwa hiyo, sheria hiyo nayo iko ambayo, inaandaliwa kwa maana ya kwamba tutajikuta tumetoka katika suala zima la matapeli ambao wanakuwepo.

Mheshimiwa Spika, katika suala zima la uwekezaji kwenye maeneo ya viwanda ambayo hasa ndiyo tunafikiria kupeleka nguvu kule, tumetenga zaidi ya ekari 12,400 ambazo ziko tayari zinasubiri wawekezaji wakati wowote wakizihitaji. Kama Wizara pia, bado tunaendelea kupitia yale mashamba ambayo yameshindikana katika kuendelezwa ili tuweze kuyachukua na kuyatenga kwa ajili ya kazi hizo kubwa ambazo tunazitegemea kama Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa vyovyote vile, ukiweka mpango mzuri kwenye matumizi ya ardhi, ukiweka mpango mzuri katika suala zima la kupanga, kupima na kumilikisha, hizi sekta nyingine zote zitakuwa katika hali nzuri katika utendaji. Nasi kama Wizara tunasema, Serikali ilishaelekeza nini cha kufanya, kwa hiyo, Wizara tumejipanga kuhakikisha kila mpango ambao unapangwa, uwe unawiana na Wizara nyingine katika utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, hata haya ambayo yanaongelewa katika suala la kuwezeshwa kwenye maeneo ya huduma, bila kuwa na mpango mzuri na bila kufanya maandalizi, hatuwezi kufika huko. Kwa hiyo, niseme tu kwamba sisi kama Wizara, tuko tayari kuhakikisha kwamba mpango huu unatekelezeka kwa kuwa unakutekeleza yale ambayo tumeyaweka kama kipaumbele katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kufanya.

Mheshimiwa Spika, pia katika upangaji wa miji yetu, kwa sababu usipoipanga miji pia, napo itakuwa ni shida. Kama Wizara, tayari tumeshaandaa mwongozo ambao sasa kuna mbunge alielekeza kwamba tunaweza pia tukadai kodi katika maeneo ambayo hayajapimwa. Kisheria huwezi kudai katika maeneo hayo, lakini tunaweka mpango mzuri ambao draft yake iko tayari ili zile Halmashauri katika ile miji inayokua kwa kasi, tuwape mwongozo wa namna ya kuwekeza, namna ya kupanga miji yao ili iweze kuwa na maeneo ya huduma, maeneo ya uwekezaji na maeneo ya makazi ili kila mji utakapokuwa unakua ukitangaza kama ni eneo la huduma, liwe limepangwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)