Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi. Niseme tu kwa kuwa, hapo nyuma nilishapata nafasi ya kuchangia, hasa kwenye upande wa shughuli za kijamii, kwa maana ya maji, umeme na shughuli nyingine. Leo kwenye mpango nilitamani sana nijikite eneo moja la ardhi pamoja na makazi.

Mheshimiwa Spika, kwenye mpango natambua tumeiweka kwamba, Serikali ina mpango wa kuhakikisha angalao eneo lililosalia ambalo halijapimwa kwa ukubwa wa eneo letu zaidi ya 880,000 kilometa za mraba tumepima eneo zaidi ya asilimia 25 peke yake. Lakini kwenye mpango umetamka namna gani ambavyo kwa miaka hii mitano tunajikita kwa ajili ya kutambua, kupanga pamoja na kupima.

Mheshimiwa Spika, sasa nilitamani nishauri kwasababu, uliwahi kusema hapa ndani na mimi niendelee kuisema kama tukiitumia ardhi yetu vizuri, tukiipima vizuri ardhi yetu naamini kwa sababu, ni mdau wa sekta hii ya ardhi naamini inawezekana ndio kikawa chanzo kikubwa sana cha mapato ndani ya nchi yetu hii Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nishauri? Nini tufanye kutokana na mpango uliopo? Cha kwanza. Ipo idara ambayo inasimamia shughuli za kupanga, kupima pamoja na kurasimisha ardhi ambayo iko chini ya Wizara ya Ardhi. Tulivyokuwa na changamoto ya maji vijijini tulianzisha chombo cha kushughulika na changamoto za maji, RUWASA. Tulivyokuwa na changamoto za barabara vijijini tulianzisha TARURA, tulivyokuwa na changamoto za umeme tulianzisha REA.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashauri baddala ya kuwa na idara ambayo imejificha ndani ya wizara inayoshughulika na kupanga, kupima na kurasimisha haya maeneo, twende tuone namna gani tunatengeneza agency iwe wakala inayojitegemea ambayo kazi yake kubwa sasa iwe ni kupima na kuendana na mpango wa Serikali huu uliopangwa wa miaka mitano. Tukifanya hivyo, maana yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza itakuwa na wigo mpana wa kushirikiana na sekta na taasisi nyingine. Hii migogoro tunayoizungumza ya ardhi kati ya wananchi na jeshi tukiwa na wakala anayejitanua maeneo yake maana yake atafanya kazi kubwa, lakini ataendana na kasi ya sisi tunayoizungumza kwamba, kwa muda mfupi asilimia 75 ya ardhi iliyosalia iweze kupimwa ndani ya miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili. Mpango ujikite uone namna gani unaweza ukashirikisha halmashauri moja kwa moja. Pamoja na kwamba, halmashauri nyingi zina vyanzo vingi vya mapato ningetemani sana mpango upeleke maelekezo moja kwa moja kwamba, halmashauri zirudi sasa zitambue kupanga na kupima maeneo yao ya ardhi, ili angalau moja kuongeza mapato, lakini mbili kama mnavyotambua tukipanga na tukipima eneo tunapunguza migogoro, kwa kufanya hivyo maana yake tutaipunguzia Wizara mzigo.

Mheshimiwa Spika, wizara sasa inafanya kazi kubwa sana ya kutatua migogoro badala ya kuibadioisha ardhi iwe source au chanzo cha mapato kwenye Serikali yetu. Ningetamani, sasa kwasababu Mheshimiwa Waziri ameshafanya kazi kubwa sana ya kukimbizana na migogoro aende aifanye sasa ardhi iwe ni sehemu ya kuongeza mapato, ili angalau mwisho wa siku tuweze wote kufaidika na sekta hii ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa miezi nane peke yake, kuanzia mwezi wa nane mpaka sasa Wizara imeingiza zaidi ya bilioni 93. Unaweza ukaona asilimia 25 ya ardhi iliyopimwa peke yake tuna bilioni 93, lakini asilimia 77 kati ya 880,000 ya ardhi ambayo haijapimwa tujiulize leo ardhi yote tukiipima kukawa na usimamizi thabiti ambao tukawa na mawakala ambao wanashughulika moja kwa moja na wanawajibika kabisa na upimaji na urasimishaji wa ardhi, Serikali itakusanya kiasi gani cha fedha kupitia sekta ya ardhi peke yake?

Mheshimiwa Spika, lakini la pili. Nizungumzie kuhusiana na hii ni Wizara ya Ardhi pamoja na Makazi, niende sasa kuzungumzia kuhusiana na nyumba. Wabunge wengi tumekuwa tukilalamika hizi real estate developers, National Housing, TBA na watu wengine ambao wamekuwa wakijenga nyumba kwa gharama kubwa. Na wengine tulikuwa tukihoji hapa kwamba, affordability ya nyumba inapatikana wapi?

Mheshimiwa Spika, haya yote tunashindwa kufika mwisho kwasababu, hatuna housing policy. Tunazo sera za misitu na sera za nyuki na sera nyingine, lakini hatuna sera inayotudhibiti na inayotuongoza kwenye nyumba, ili mwisho wa siku National Housing wakijenga nyumba Rorya, tukisema nyumba ni ya bei nafuu iwe angalau tayari ina limit kwa sababu, tukiwa na policy maana yake tutatengeneza sheria. Akijenga Rorya nyumba ya milioni 20 tutakuwa tunajua kabisa hii kweli milioni 20 ni affordable. Akijenga Kongwa nyumba ya milioni 20 tunaweza tukamhoji, hii ni affordable nyumba ya vyumba viwili?

Mheshimiwa Spika, kwasababu, kutakuwa kuna sheria inayomuongoza yeye katika ujenzi, sasahivi hakuna sheria. Anaweza akajenga nyumba akai-term kama affordable, ukimuuliza kwetu sisi, mimi inaweza isiwe affordable milioni 50, lakini kuna mtu mwingine milioni 50 kwake ni affordable. Na kwasababu hakuna policy wala sheria inayomuongoza inakuwa ni wakati mgumu sana kujua sasa wapi Serikali inasimamia kusema affordability ya nyumba ni ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na huu utakuwa ni muongozo mzuri kwa TBA, national Housing na real estate developers wengine wote wanaofanya shughuli za kujenga maeneo. Hata Serikali kwa maana ya kupitia Wizara itakuwa na sehemu ya kujivunia, unapokwenda ukasema unaonesha nyumba za affordability’s unaonesha kulingana na uhalisia uliopo.

Mheshimiwa Spika, sio uwongo gharama za ujenzi wa kila maeneo zinatofautiana. Gharama ya ujenzi wa Rorya haiwezi kuwa sawa na gharama ya ujenzi wa Dar-es-Salaam. Kwa hiyo, maana yake ile ukii-term kwamba, huyu mtu ambaye anajenga nyumba ajenge nyumba ya affordability Rorya ya milioni 30 ukasema sio affordable atakuuliza ni sheria ipi inayomuongoza? Kwa hiyo, ningependa nichukue nafasi hii kuiomba sana Wizara, lakini kupitia Waziri wa mpango, Waziri wa Fedha, ilia one namna gani ile sheria, ile policy inaweza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho ni kwenye RERA, Real Estate Agency. Leo kuna watu sio vizuri kuwasemea, hawa tunaowaita madalali; brokers leo akiuza ardhi akiwa mtu wa kati hata kama ardhi ni ya milioni 500 akichukua commission hakuna kodi anayolipa. Lengo letu ni nini?

Mheshimiwa Spika, nilikuwa natamani sana tutengeneze Real Estate Agency, tutengeneze Real Estate Regulations ambazo zinawa-guide hawa ma-brokers na hawa ma-Real Estate Agency, ili mwisho wa siku moja itasaidia ku-regulate, lakini mbili itasaidia kukusanya kipato ambacho anashiriki kwenye kuuza kama mtu wa kati, lakini tatu itakuwa ni fursa kwao kufanya shughuli za kibiashara kwasababu, sasa watakuwa wanatambulika wako wapi. Leo ni ngumu sana kumtambua broker yupo wapi na anafanya kazi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Asante sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)