Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano. Nitajikita katika mambo machache kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, ni kwenye suala la afya. Ni ukweli usiopingika kwamba, kama wananchi wetu wakiwa na afya imara na Madhubuti, bila shaka Taifa hilo litakuwa ni lenye neema, ni Taifa ambalo litastawi kwa vizazi na vizazi.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu inapaswa ijikite katika afya za msingi, kwa maana ya kwenye Zahanati zetu. Tukiboresha afya inayotolewa, matibabu yanayotolewa katika Zahanati zetu, kwa hakika huu msongamano ambao tunaukuta kwenye Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufaa kwa kiwango kikubwa tutapunguza.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikijisifia hapa kwamba imejenga vituo vya afya vingi na kadhalika na imeeleza mambo mengi, imejenga vituo vya afya vingapi. Sawa, mmejenga, lakini vipi kuboresha huduma zinazotolewa katika zahanati zetu? Tukiweka mkakati wa kuhakikisha zahanati zetu zina maabara ya kutosha yenye vifaa vyote vinavyotakiwa, watumishi wa afya wanakuwepo kwenye level kabisa ya chini ya zahanati. Pia kuhakikisha miundombinu yote kwa maana ya nyumba za Madaktari, Manesi, barabara inayoelekea kwenye hivyo vituo, kuhakikisha vinapitika mwaka mzima, maana yake tutakuwa tumemsaidia mwananchi yule wa chini kabisa ambaye anakaa karibu kabisa na zahanati.

Mheshimiwa Spika, tukumbuke kwamba, mwananchi wa kawaida akiugua huduma yake ya kwanza ni kwenye zahanati kwa sababu pia iko karibu na yeye, anaweza kuifikia, tofauti na hata akitaka kutafuta huduma hiyo kwenye ngazi ya kituo cha afya. Kwa hiyo ni vema sana Serikali ikaona umuhimu wa kuwekeza na kuweka nguvu kubwa kwenye huduma ya afya katika ngazi ya msingi ambayo inamgusa mwananchi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna mada hapa asubuhi, mjadala mkubwa kuhusu ununuzi wa ndege na Shirika letu la Ndege. Mpango sasa hivi unaonesha kuna kununua ndege zingine nne, wanaweza kufikiria kuacha kununua hizo ndege, zilizopo tuziboreshe, hiyo fedha tukapeleka kwenye zahanati zetu kuziboresha moja kwa moja tutakuwa tumemgusa Mtanzania wa chini kabisa kwa sababu sio Watanzania wote ambao kwa namna moja ama nyingine wanaweza kuwa na mwingiliano au kufaidika moja kwa moja na ndege tutakazonunua, lakini ukiboresha zahanati kwa namna yoyote ile umemgusa yule mwananchi wa chini kabisa, yule mpigakura wetu, yule mwenye uhitaji wa kutosha wa kuhakikisha anapata huduma bora katika zahanati zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine katika Sekta ya Afya, ningependa kuchangia pia kuhusiana na suala la magonjwa yasiyoambukiza. Asilimia 33 ya vifo vinavyotokea hapa nchini vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza. Magonjwa yasiyoambukiza wataalam wanasema yanatokana na lifestyle, namna tunavyoishi, ukiacha mengine ya kurithi na kadhalika, lakini mengi ni namna gani tunavyoishi, pressure, sukari, moyo, saratani, figo na kadhalika na ndivyo nilivyosema kwamba asilimia 33 ya vifo vinatokana na magonjwa ya namna hii.

Mheshimiwa Spika, haya magonjwa yasiyoambukiza, kama Serikali ikaweka mkakati wa dhati wa kuhakikisha tunawekeza kupunguza magonjwa haya yasiyoambukiza kwa kushirikiana na jamii na wadau wengine bila shaka tutapunguza vifo hivi, hata mwisho wa siku ule msongamano wa wananchi wetu kukimbilia huduma zote ambazo zinatakiwa kwenye zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya za kanda na za rufaa utapungua, kwa sababu tutakuwa tumejikita katika kuona namna gani tunapunguza magonjwa haya yasiyoambukiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi leo wote ambao tumesoma bila shaka tulikuwa tunafahamu, leo mtoto yeyote au hata sisi tuliosoma enzi hizo tunafahamu kabisa tunaambiwa, unapata malaria kwa sababu utang’atwa na mbu, ipo ni masomo yanafundishwa, ni mtaala upo na unafundishwa na watoto wanakua wakijua kabisa niking’atwa na mbu nitapata malaria. Sasa vivyo hivyo Serikali inatakiwa kufikiria kuingiza mtaala wa namna gani mtoto huyu anakuwa akifahamu kwamba kuna magonjwa yasiyoambukiza na naweza kukabiliana nayo kwa elimu nitakayoipata. Kwa hiyo ni vyema sana Serikali ikafikiria katika mpango wake namna gani ku-appear kupitia mitaala yetu kuingiza jambo hilo na lenyewe likawa sehemu kama ambavyo tunafundishwa kuhusu malaria na mambo mengine mengi, mwisho wa siku tutakuja kuona, inawezekana tusiyaone matokeo kwa muda mfupi, lakini kwa muda mrefu tukaona matokeo ya kile ambacho tunakieleza. Kwa hiyo ni muhimu sana Serikali ikaweka mpango thabiti wa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Spika, pia kutoa elimu kwa jamii ni muhimu sana. Kuna wataalam walikuwa wanatupa takwimu sisi Kamati yetu. Wanasema ni fahari leo kwa sisi wazazi unamchukua mtoto wako unampeleka asubuhi na gari lako kwenda shuleni na anarudishwa nyumbani jioni. Akifika anakaa kwenye kochi, anasema mama nataka chipsi mayai anapewa, anakaa kwenye kochi, labda mzazi ana na tablet kidogo anachezea, anaangalia TV, inafika jioni anakula analala, yaani hiyo inakuwa ni lifestyle, kumbe mtoto huyu anaandaliwa mazingira ambayo mwisho wa siku katika ukuaji wake anaanza kupata magonjwa yasiyoambukiza. Uzito kupita kiasi, sukari mwisho wa siku hata uwezo wa kufikiri na kuchanganua mambo unapungua kwa sababu ya lifestyle.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hapa iko haja ya Serikali kwa kushirikiana na jamii kutoa elimu ya kutosha, yaani tusione kwamba huo ndiyo ukisasa au ndiyo style Fulani, wale wataalam wamekuja wametuambia kwamba walivyofanya utafiti kwenye aina ya wazazi ambao wanahudumia watoto wao kwa namna hiyo na yule ambaye anapanda daladala asubuhi kwenda shuleni, wakakuta kwamba mtoto huyu ambaye mzazi wake anamlea kama mayai ana-risk kubwa sana ukilinganisha na yule ambaye atapambana kivyake kutembea kwenda shule au atapambana kwenye daladala kwenda shuleni, yule automatic atajikuta mwili wake unafanya kazi kuliko hata yule ambaye tunampeleka asubuhi na gari kwenda shuleni na anarudishwa na gari na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niishauri Serikali katika mipango yake hii, lazima iangalie namna bora ya kuigeuza jamii yetu kulingana na maisha tunayoishi leo. Unaona tunafurahi kwenda kwenye ma-supermarket makubwa unaingia labda hapo shoppers, unaenda Mlimani City na kwingineko, tunachukua samaki waliohifadhiwa kwenye makopo, basi tunaonekana kama ndiyo tuna maisha fulani mazuri, kumbe tunajiandalia matatizo. Yaani mtu anayeenda maeneo hayo anaonekana ni bora kuliko yule anayeenda Majengo pale sokoni Dodoma. Kumbe yule ni bora zaidi kwa sababu anapata kitu fresh! Anapata matunda fresh kutoka shambani, anapata labda samaki fresh, nyama ya ng’ombe fresh!

Mheshimiwa Spika, sasa hii ni kuangalia namna gani tunabadilisha mind-set ya jamii tunayoiongoza, Serikali wakaweka kitengo maalum au fungu maalum kwa kushirikiana na wadau, kushirikiana na jamii na viongozi sisi wa kisiasa, tukaendelea kuibadilisha jamii yetu kuishi kwenye lifestyle ambayo itatusaidia ili mwisho wa siku tuepukane na magonjwa yasiyoambukiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya pili inajikita katika Sekta ya Utalii. Bila shaka Serikali na wadau mbalimbali tumeona kwamba jinsi gani ambavyo corona ilivyofika imeathiri kwa kiwango kikubwa Sekta ya Utalii na imeathiri mpaka yule mtu mmoja mmoja ambaye anategemea utalii ule. Naongea hivyo kwa sababu natoka Mkoa wa Arusha na nafahamu jinsi ambavyo watu katika Sekta ya Utalii wameathirika kwa kiwango kikubwa. Sasa huko nyuma tuliongea na kuishauri Serikali iangalie namna gani ya kuweka mipango, inapotokea dharura za namna hii wafanyabiashara na wale wanaonufaika moja kwa moja na Sekta hii ya Utalii wapunguziwe mambo fulani fulani yanayowaumiza.

Mheshimiwa Spika, mfano, hoteli nyingi zilifungwa wakati wa corona, nyingi mno kukawa hakuna wageni, wakapunguza wafanyakazi lakini mwekezaji au mtu yule mwenye hoteli hajawahi kupunguziwa kodi na Serikali hata siku moja, tena alitakiwa alipe na wengine kodi zikaongezeka. Sasa sina uhakika sana kama tunataka kweli kuendeleza utalii ambao unachangia pato kubwa la Taifa au tunataka kuumaliza na kuukandamiza. Kwa hiyo nishauri kwamba ni vyema panapotokea majanga ya namna hiyo, hatuyaombei lakini yanaweza yakatokea, ni lazima kwenye Sekta ya Utalii pamoja na sekta zingine Serikali iwe na mipango ya kuhakikisha inatoa unafuu au kwa mwekezaji mmojammoja au wawekezaji kwa ujumla ambao moja kwa moja wanaungana, kunakuwa na mnyororo wa moja kwa oja ambao unamgusa mwananchi mpaka chini kuhakikisha inatoa unafuu wa mambo fulani fulani ambayo yatamfanya mtu huyu aweze kuendeleza biashara ile ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado inatakiwa mikakati ya kuendeleza na kukuza utalii wetu. Bado tunahitaji kuwa na mikakati mizuri ya kuhakikisha Serikali inapata mapato katika utalii wa picha, hatujawekea mkazo na huko nyuma ripoti ya CAG zimeeleza mara nyingi kwamba Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kwa sababu haiweki mpango thabiti wa kuhakikisha utalii wa picha unatuingizia pato na kuhakikisha unasimamiwa vizuri. Vivyo hivyo kwenye Sekta ya Uwindaji pia inapaswa kuwekwa mipango thabiti ya kuhakikisha kwamba inaingiza kodi ambayo mwisho wa siku itatusaidia.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kidogo pia kuhusu Serikali zetu za Mitaa hapa nchini. Halmashauri zetu nyingi zimepokonywa mapato, mwisho wa siku zinashindwa kujiendesha, mwisho wa siku ufanisi unaotarajiwa hauwezi kufikiwa kwa sababu hamna mapato yale yanayokusudiwa. Kwa hiyo niishauri Serikali, kuna mapato ambayo Serikali iliyachukua haiwezi hata hiyo TRA yenyewe kukusanya bado imekuwa ni changamoto, niishauri irudishe kwenye Serikali za Mitaa. Ikirudisha kwenye Serikali za Mitaa pawepo na usimamizi thabiti, pawepo uhakika kwamba kile kilichorudishwa kinatumika moja kwa moja na kinafanya kazi ambayo inakusudiwa. Hiyo itatusaidia sana kwa sababu kwenye wananchi ni kwenye Serikali za Mitaa, ndiyo tunamgusa mwananchi moja kwa moja kule chini. Ukiziwezesha na kuzisaidia halmashauri zetu moja kwa moja umemgusa Mtanzania. Kwa hiyo ni vyema sana Serikali ikalitazama jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi, mno! Ripoti ya CAG na taarifa mbalimbali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Cecilia Paresso.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie. Ripoti mbalimbali zinaonesha kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi vivyo hivyo basi ni vyema Serikali ikahakikisha watumishi wanapatikana. Watumishi wa kutosha wakiwepo, ukirudisha mapato, ukasimamia vizuri, matokeo tunayoyatarajia kwa nchi yetu yataweza kufikiwa. Ahsante sana. (Makofi)