Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante niungane na wasemaji waliotangulia kuunga mkono hoja iliyoko mbele yetu, lakini pia kuipongeza sana Serikali kwa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano, ambao unaonekana ni taswira njema kwa ajili ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inapiga hatua kimaendeleo.

Mheshimiwa Spika, nilitaka nijielekeze moja kwa moja kwa juhudi za Serikali ambazo kupitia mwongozo ulioletwa mwaka 2018, ambao ulikuwa ni mkakati madhubuti wa Serikali kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweza kutelekeza miradi ya kuchochea upatikanaji wa fedha ili ziweze kujitegemea na hivyo kutoa huduma sahihi kwa wananchi. Fedha hizo za kuwezesha miradi ya kimkakati ziliendelea kutolea na Serikali kutoka Serikali Kuu; na tumeona katika sehemu kubwa zimekuwa za tija na zimeleta matokeo chanya.

Mheshimiwa Spika, niseme katika maeneo ambayo miradi ya kimkakati imeweza kutekelezwa kwa ufasaha tumeona matunda mazuri, moja wapo ni ushahidi kupitia taarifa ya CAG. Jiji la Dar es Salaam kabla halijavunjwa kwa zile hesabu zilizofungwa tarehe 30 Juni mwaka jana lilikuwa na uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 484; kwa hiyo maana yake lilikusanya Bilioni 16 na lina uwezo wa kutumia Bilioni tatu. Kwa hiyo tunaona kama tuna miradi mingine ya kimkakati, huduma za wananchi kama kujenga zahanati, kujenga vituo vya afya na Mengine kuchangia barabara kupitia TARURA jiji hilo lilikuwa na uwezo. Lakini siri ya mafanikio ilikuwa ni nini, ni uwezeshaji uliotoka Serikali Kuu, ni mbegu iliyopandwa katika baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa moja wapo ikiwa hilo Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, tunaona sasa hivi mkakati wa Serikali unavyokwenda na katika bajeti hii inayokuja ni ushuhuda tosha, Ofisi ya Rais TAMISEMI imeelekeza Mamlaka za Serikali zote 185 kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya, kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa kituo kimoja. Najua kupitia huu uwekezaji uliokwenda kule kupitia miradi ya kimkakati vituo hivyo vitajengwa; na baadhi ya halmashauri ambazo hazijapata uwezeshaji huo inawezekana zikatekelezwa kwa kusuasua, lakini niseme ni mwanzo mzuri. Kwa hiyo tunachotakiwa kufanya ni nini? kwa kuishauri Serikali. Ni kukuhakikishia sasa huu mkakati ambao uliundwa madhubuti ambao umeanza kuonyesha matokeo chanya uendelezwe.

Mheshimiwa Spika, mkakati huu kwa sasa haufanyi kazi ulisimamishwa na Serikali, na maelezo hayakuwa wazi kuonyesha kwamba umesimamishwa kwasababu gani na unaanza lini?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe kwa kusema kwamba Serikali, kwa kazi nzuri ambayo tumeshaiona matokeo yake ni kwanini tusiwezeshe? Tukiziwezesha halmashauri hizi maana yake tunategemea sisi tunakuwa tunatoa maelekezo kwamba sasa mwaka huu kama nchi yetu kuna kigezo fulani cha kuanzisha miradi fulani weka katika bajeti zenu mradi moja, mbili, tatu unaweza kutekelezwa kwa ufasaha na tutaona maendeleo makubwa sana. Katika mwongozo huo kuna baadhi ya vitu ambavyo inatakiwa kama Serikali kuvifanyia kazi. Suala la kwanza vipo vigezo madhubuti 14 katika mwongozo huo, baadhi ni vizuri baadhi vinahitaji kufanyiwa marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano suala moja wapo ni kuwa na hati safi. Tunaona kwenye taarifa ya CAG leo zipo halmashauri jumla 63 hazina hati safi, anayeadhibiwa ni nani? Ni yule ambaye alisababisha, kama mtaalam wetu au mwananchi? Kwa nini tunapeleka adhabu kubwa kwa mwananchi; ambapo Serikali ingeweza kupeleka fedha za kuwezesha miradi ambao utasaidia baade apate huduma tukamuadhibu kwasababu hana hati safi? Mwananchi hajui hati safi, haijui kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niiombe sana Serikali, sisi wote ni waumini wa kuhakikisha fedha zinasimamiwa vizuri, kwa umadhubuti kabisa, lakini sasa suala hilo naomba tuliangalie kwa mapana, kama kuna hati ambayo sio safi wale wawajibishwe lakini fedha ziendelee kupelekwa kwenye halmashauri.

Mheshimiwa Spika, wakati naendelea kumalizia dakika zangu zilizobaki kupitia meza yako hiyo nimuombe Waziri wa Fedha na Mipango. Zipo barua nyingi ambazo zimepelekwa kwake kwa zile halmashauri ambao zimeshakidhi vigezo. Moja wapo ni Wilaya ya Misenyi Jimbo la Nkenge ambapo ilipelekwa barua tarehe 4/09/2019 ya mradi wa maghala nane katika mpaka wa Mutukura kukiwa na stendi ndogo pamoja na jengo la biashara.

Mheshimiwa Spika, niombe, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, wakati unakuja kwenye bajeti angalau uweze kuhakikisha kwamba mradi huo ndani ya Wilaya ya Misenyi unaweza kutekelezwa. Tupo mpakani mwa Uganda mradi huo utaleta matunda ndani ya muda mfupi.

Mheshimiwa Spika, barua hiyo haina mradi wa Wilaya ya Misenyi peke yake, iko miradi mingine. Babati TC nao waliomba Bilioni 5.1 kujenga Stendi, kuna Meru DC nao waliomba Bilioni 10 kuna Lindi MC waliomba ujenzi wa Stendi 7.8 pamoja na Soko katika Manispaa yetu ya Lindi. Kwa hiyo niombeā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: basi nikushukuru naunga mkojo hoja. (Makofi)