Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima kuweza kupata tena nafasi hii kuzungumza ndani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, naungana na Wabunge wote waliosema kuna umuhimu wa kuwa na agenda za kitaifa. Kuna maana kubwa ya kuwa na agenda za kitaifa. Tunatambua kuanzia Awamu ya Kwanza mpaka sasa tuko Awamu ya Sita, kuna mambo ambayo yaliibuliwa na awamu zote, lakini unaona umaliziaji unakuwaje. Tunapokuwa na agenda za kitaifa kila anayekuja, hatujui kesho atakuja Rais wa namna gani, atatokea chama gani, kukiwa na agenda za kitaifa zinam-guide kwamba Taifa tunakwenda hivi. Kwa hiyo, ni vizuri jambo hilo likaangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Taifa letu limebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi, ukiangalia ndani ya Bunge, tika nimeingia Bunge lililopita, tukianza kuzungumza suala la maji kila Mbunge anasimama anazungumza uchungu ulivyo.

Mheshimiwa Spika, nchi hii tuna mito ya kutosha, tuna maziwa ya kutosha, tuna bahari za kutosha, nini kimekosekana kwenye nchi yetu? Je, wataalam wetu hawatushauri vyema? Au tumetanguliza siasa zaidi hata mambo ambayo yanahitaji utaalam? Ni vizuri tukajipima tuangalie shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisimama wiki iliyopita kuuliza Habari ya maji; Ziwa Tanganyika na kina chake, lakini kutoka Kilando kuja Namanyere ni kilometa 64 tunazungumza habari ya maji miaka nenda rudi, shida ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tumeanza kufikiria maji kutoa Ziwa Viktoria tumefikisha Tabora tufikiri mikoa hii mitatu, tufikir Katavi, tufikiri Rukwa, tufikirie Songwe hawa wote wanaweza kufaidika na maji kutoka Ziwa Tanganyika badala ya kutimia fedha kidogokidogo kwenda kuanzisha miradi ambayo haiwezi kutatua changamoto ya maji. Ni bora tukafikiria kitu ambacho tunaamini tunakwenda kumaliza changamoto ya maji na suluhisho ni kutumia maji kutoka Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Ziwa hilo Tanganyika ukiachana na kufaidika na maji tuna uvuvi pale. Slogan ya Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa ni Serikali ya Viwanda, tujiulize tuna viwanda vingapi leo kwa ajili ya uvuvi kutoka kwenye maziwa yetu kama kweli tunachokisema ndio tunachokimaanisha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba, Serikali imekuwa inakuja na slogans mbalimbali, lakini siamini kama slogans hizo zinakuwa zimeshirikisha kikamilifu wataalamu wetu na kama zinaweza kutekelezeka. Leo kama tunaweza kusimamia kwenye kilimo lazima tujue kabla hatujafikiri viwanda tunazungumzia raw material. Mashamba yapo, maeneo yapo, shida ni nini kwenye Serikali yetu ya Tanzani? Ni vizuri kuwashirikisha kikamilifu wataalamu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba kumekuwa na ilani mbalimbali, kuandaa ilani ni jambo moja na kutekelea ilani ni jambo jingine. Tukianza kuzungumzia utekelezaji tunakuja kwenye mpango huu ambao tunausema. Na mpango lazima uendane sambamba na hiyo ilani ambayo mnakuwa mmeipanga ya miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ziwa Tanganyika pamoja na kwamba, hatujalitumia vizuri hilo eneo la Ziwa Tanganyika, tuna-share zaidi ya nchi moja; tuna nchi ya Tanzania ambayo sisi tunamiliki kwa ukubwa zaidi, lakini kuna Kongo, kuna Zambia. Leo unapokuja na utaratibu wa kanuni juu ya wavuvi kutumia nyavu gani ni vizuri kabla ya kuja na hayo maamuzi mjiulize hizo nchi nyingine wanatumia nyavu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa Samaki hawajui kwamba, mpaka huu leo tuko Tanzania, kesho tuko Kongo. Inawezekana tunakuwa na sheria na kanuni ambazo zuinatuadhibu sisi wenyewe tunashindwa kutumia rasilimali tulizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo leo wakati tunafikiria viwanda tumewawezeshaje wavuvi wetu ambao wanaweza kutumia hizo teknolojia na kuwawezesha, sio kuwapa tu hizo kanuni na sheria kwasababu, lazima Serikali tujue tuna wajibu kwa wananchi wetu. Pamoja na kwamba, tunawaambia waende kutumia nyavu za milimita nane na hatujui zile nchi nyingine ambazo tuna-share kwenye ziwa moja hilohilo Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tujiulize ni kwa nini wakati tunafikiri viwanda na kipaumbele chetu ni kuwaambia wananchi au wavuvi wetu watumie milimita nane tumejiwekeza kiasi gani sisi wenyewe kutengeneza hizo nyavu ambazo tunafikiri ni halali, ili tuweze kuwawezesha wavuvi wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inafikia mahali sio kila mvuvi ni mtaalamu, akienda dukani akauliza kwamba, hii ndio milimita nane, anapewa kwamba ndio yenyewe. Akifika kule, kwa bahati mbaya zaidi, Serikali badala ya kukamata kiwanda ambacho kinazalisha wanakwenda kwa mlaji wa chini kabisa ambaye hajui, yeye ameambiwa ni milimita nane anakwenda kutumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na miongoni mwa kanuni ambazo ni vizuri tukaziangalia kama lengo ni kuwasaidia wavuvi wetu na Watanzania, sisi hapa tunazungumzia milimita nane kwamba, ndio wakatumie kuvua Samaki, wavuvi hawa wanatumia hizo milimita nane. Wakifika kule wakiwa wanavua samaki, wametega wale samaki, ile nyavu haizuii chini ya ile sentimita ambayo wanaitaka wao Serikali, unakuta Samaki wale wengine wamefuata. Kwa bahati mbaya zaidi watendaji walipo huko chini anapofika kwa mvuvi huyu badala ya kuangalia kwamba, ile nyavu ndio iliyosababisha sio mvuvi. Kwamba, ni kweli ni milimita nane, lakini Samaki waliongia pale labda wawili au watano, mvuvi anapigwa fine milioni mbili, milioni tano, milioni kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yawezekana lengo la Serikali ni kweli ni kukomesha uvuvi haramu, lakini ni vizuri tukajua chanzo, ili tuje na suluhisho kama Taifa badala ya kuja na hizi operations ambazo hazieleweki, matokeo yake watendaji wamekuwa wamekuwa mahakama, wamekuwa ndio askari. Sasa kama tunataka hapa tunafikiri kwamba, namna gani sekta ya uvuvi imesaidia Taifa kwa pato, lakini tufikiri pia tunapotaka kupata pato kubwa tumeandaaje juu ya kesho? Hawa wavuvi tumewajengeaje mazingira rafiki, ili kesho tuendelee tena kupata fedha zaidi kwa ajili ya kukuza uchumi wa Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitarudi kwenye jambo ambalo ni la muhimu zaidi. Kwenye ileile ya kwanza kwamba, agenda za kitaifa. Kumekuwa na wimbo usioisha Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, ni jambo jema Liganga na mchuhcuma, lakini limekuwa linazungumzwa halina majibu. Ni vizuri leo Mheshimiwa Waziri uje utuambie nini kimejificha kwenye hili jambo ili tuweze kujua tunachokizungumza. Kwasababu, kama jambo ni jema nini kinazuwia hili jambo lisitekelezeke? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika tuliambiwa tunaenda kwenye uchumi wa gesi. Gesi ya Mtwara imeishia wapi? Mje mtupatie majibu hapa nini kinaendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tunaangalia zawadi nyingine ambayo Mungu ametupa Mkoa wa Rukwa, helium gas, tunajua kwamba Serikali imefanya hatua mbalimbali, lakini tunataka kujua ukitazama kiuhalisia bado hatuko serious na uchimbaji wa gesi hii kuanzia miundombinu, kuanzia elimu kwa wananchi wanaozunguka eneo lile, tunataka tena mambo ya Mtwara yaje yajitokeze na Mkoa wa Rukwa. Ni vizuri tujipange vizuri na lengo ni jema, lile suala sio la Mkoa wa Rukwa ni suala la kitaifa. Makosa yaliyojitokeza iwe ni fundisho tunapoandaa jambo jingine kutokea.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia, tumekuwa na utaratibu ambao tunatamani kumuokoa mtoto wa kike. Kumekuwa na mkanganyiko kidogo wa sheria zetu, sheria ya ndoa na sheria ya mtoto. Kwenye Mpango wa Miaka Mitano tunatamani akina Mheshimiwa mama Samia wengine, wajengewe mazingira rafiki ili tupate Marais wazuri wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kila sababu leo, natambua kwamba, sheria zipo, lakini kuna mianya ambayo bado watu hawa wanatumia kuwaumiza watoto wa kike. Ni vizuri tukalinda ndoto za watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeangalia kuna namna ambavyo Mkoa wa Shinyanga wameanza, pamoja na kwamba ndio walikuwa wanaongoza wakiwa na asilimia 59 kwa takwimu ambazo zimetokea 2006 nafikiri.

Mheshimiwa Spika, wale watu wamekuja na mikakati mbalimbali ambayo ni mizuri kuiga kama Taifa. Cha kwanza wamekuja na utaratibu wa kujenga shule ya girls, kwa maana ya kwamba wameamini mazingira pia yalichangia watoto wa kike kupata mimba za utotoni na ndoa za utotoni. Jambo hilo si baya kama likawa ni mpango wa kitaifa, kwamba kila Halmashauri angalau ikawa na shule moja ya girls ili tuone namna gani tunaweza tukalinda vipaji vya watoto wetu wa kike.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la kubadilisha vipengele hivyo ambavyo vimekuwa ndio uchochoro, yaani mtu amebaka, anafika pale mtoto wa kike anaulizwa anasema ni kweli, wazazi walikubaliana lakini mimi nilikuwa nataka kusoma. Akija kwenye sheria hiyo ya ndoa wanamuuliza mlalamikaji kwamba wewe kuna taasisi ambazo zimejitolea kwa ajili ya kutetea haki za watoto wa kike, anapofika pale anaambiwa ulipoenda huko mpaka unataka kufunga ndoa ulikuta kwamba wameandaa sherehe kwa maana ya vyakula na nini anakubali kwamba ni kweli. Wanamwambia soma sheria ya ndoa ina maana kulikuwa makubaliano ya wazazi na ndiyo maana hatua hiyo ikafikia hapo.

Mheshimiwa Spika, bado bado narudi, pamoja na kwamba sheria tulitunga ndani ya Bunge kama lengo ni kumlinda mtoto wa kike, tufanye marekebisho ya sheria hizo ambazo bado zina mwanya ambao watoto wetu wa kike wanaendelea kuangamia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mazingira hayo hayo, namalizia kusema; kama kilimo tuna uwezo wa kulima Tanzania, kama uvuvi tuna uwezo wa kuvua zaidi kuliko maeneo mengine, tayari Serikali imewekeza kwenye Bandari mbalimbali ikiwemo Bandari ya Kagwe, tutumie Ziwa Tanganyika, kwasababu Mpango wa Serikali Awamu ya Tano ilikuwa ni kufua Meli ya MV Liemba; ile itasaidia kusafirisha minofu, kusafirisha mazao mbalimbali badala ya kupiga kelele habari ya soko. Leo Zambia wameanza kuchukua eneo la Kongo na sisi tupo jirani tunashindwa kutumia hiyo nafasi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana ahsante.