Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Nami ningependa nijielekeze katika kuhakikisha namna ya kuipunguzia Serikali gharama; kwasababu kwa siku mbili hizi tumesikia michango mingi sana ya Waheshimiwa Wabunge ambayo yote inalenga kuboresha hali ya uchumi wetu na kuboresha pia hali ya maendeleo ya Taifa. Lakini ili Serikali iweze kutimiza yote hayo Serikali inahitaji fedha, Serikali inahitaji Bajeti. Kwa hiyo mimi ningependa kuishauri Serikali, ifike mahala sasa iangalie suala zima la idadi kubwa ya mahabusu walio gerezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwasababu hivi sasa Tanzania ina takribani wafungwa 16,836, lakini vivyo hivyo ina maabusu 16,703 ambapo Jeshi la Magereza kila mwezi linatumia takribani milioni 900 kwa ajili ya kuwalisha hawa wafungwa pamoja na mahabusu; sasa hii ni gharama kubwa sana kwa Serikali. Nasema ni gharama kubwa sana kwa Serikali kwasababu Jeshi la Magereza halina vyanzo vya mapato ilhali linajitegemea. Kwa hiyo binafsi kwanza ninafarijika sana kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria kwa hiyo jambo hili analifahamu fika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile hata katika hotuba za hivi karibuni za Mheshimiwa Rais Mama yetu mpendwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameongelea pia suala la idadi kubwa ya mahabusu gerezani. Sasa tupate picha kidogo ikiwa tutaweza kupunguza idadi ya mahabusu gerezani, ina maana kati ya ile milioni 900 kila mwezi…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Neema kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, ni taarifa ndogo tu. Katika mchango wake amesema Waziri wa Fedha alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, napenda tu kumjulisha kwamba alikuwa pia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwenye hilo eneo u- concentrate vizuri kuishauri Serikali, ahsante (Makofi).

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Neema endelea na mchango wako.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru lakini pia naomba unilindie muda wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa mantiki hiyo ile milioni 900 ambayo Jeshi la Magereza inatumia kila mwezi kwa ajili ya kulisha chakula wafunga na mahabusu tukiweza kupunguza idadi ya hawa mahabusu ina maana kuna kiasi kikubwa cha fedha ambayo tutaweza kuokoa; na kiasi hicho kila mwezi kitaweza kwenda kufidia kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinahitajika ili kutekeleza mipango mbalimbali na ushauri mbalimbali ambao wametoa Waheshimiwa Wabunge ndani ya hizi siku mbili. Kwa hiyo mimi ningependa kuchukua fursa hii kuishauri Serikali ichukue maamuzi madhubuti kabisa ya kuona namna gani tutapunguza idadi ya mahabusu kule gerezani kwa lengo kubwa la kuchangia kupunguza gharama kwa Serikali. Kwasababu mimi ninaamini tunavyochangia mpango lazima pia tuangalie tunaipunguziaje mzigo Serikali, tunaokoaje fedha za Serikali ili zielekezwe huko kunakostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi naona huu ni upotevu wa fedha usio wa lazima. Kwa hiyo pamoja na ushauri huo pengine njia nyingine ambayo tunaweza tukafanya Mahakama ibebe jukumu la kugharamia hii bajeti ya kulisha hawa mahabusu wako gerezani kwasababu kimsingi wako kutokana na ucheleweshaji wa wao kuhakikisha kwamba kesi zote hizi zinafikia kupata hukumu. Na kwa mantiki hiyo hiyo pengine hata na Jeshi la Polisi pia linajukumu katika hili; kwasababu ni kuendelea kuionea Jeshi la Magereza ilhali Serikali imesema ijitegemee na Jeshi la Magereza halina mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi binafsi nina imani kubwa sana atakapokuja kuwasilisha hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ukizingatia, kama alivyosema dada yangu pale kwamba alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alikuwa pia ni Waziri wa Katiba na Sheria basi atatueleza ni namna gani Serikali inapanga kwenda kupunguza idadi ya mahabusu ili ile bajeti ambayo inatumika hivi sasa iende kwenye mambo ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo naomba kuunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)