Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai mpaka leo, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu wa Maendeleo ya Miaka Mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na zao la chikichiki. Zao la chikichi kwetu Kigoma ni utambulisho wetu, ni identity yetu, ukitaja chikichi ama mawese Tanzania hii kwa watu inakuja ya Kigoma picha, lakini chikichi kwetu ni ajira lakini pia chikichi ni siasa. Sasa nimesoma Mpango huu wa Miaka Mitano vizuri sana, ni mzuri kwa kweli, lakini niseme tu, nchi hii mahitaji yake ya mafuta kwa mwaka ambayo tunaagiza kutoka nje ni jumla ya tani 570,000 kwa mwaka bado kwa mujibu wa takwimu ya Serikali. Watanzania wanahitaji mafuta tani laki 570,000 kwa mwaka, lakini ambayo tunazalisha sisi Tanzania ni tani 205,000 peke yake. Maana yake tunaagiza kutoka nje tani 365,000. Zaidi ya asimilia 50 ya mafuta ambayo tunatumia sisi watanzania tunaagiza kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba katika huu Mpango wa Miaka Mitano, Serikali ijikite kuweka malengo ya kuhakikisha kwamba tunaweza kuzalisha mafuta ambayo tunaweza kulisha watanzania pasipo kuangiza nje na inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye matunda yanayotoa mafuta, tafiti inaonesha mchikichi ni namba moja, zao namba moja kwenye matunda yanayotoa mafuta. Ziko ripoti zinazoonesha, wapo waliokuja kwenu Tanzania wakachukua mbegu za michikichi, wakaenda kwao, leo hii wanatumia yanawatosheleza mpaka mengine wana-export kwenda nje ya nchi. Sasa ushauri wangu kwa Serikali kwanza nimshukuru Waziri Mkuu kabisa kwa moyo mkunjufu kwa namna alivyovalia njuga suala la kufufua kilimo cha michikichi na kupendeza katika Mkoa wa Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja mara kadhaa kwa miaka ile ya kwanza, akasisitiza akatoa maelekezo ambapo hamasa imekuwa kubwa sasa, lakini pia kuna mbegu mpya tumepata na kuna chuo kizuri sana kwa ajili ya utafiti wa michikichi kipo. Sasa wananchi wamehamasika wamepanda chikichi kwa wingi sana. Sasa kinachofata hapo ni kwamba wataalam wanasema inawezekana baada ya miaka mitatu minne uzalishaji wa mafuta ya mawese uka-triple yaani ukawa mara tatu. Sasa hofu yangu ni moja tu, tunapoenda kuongeza uzalishaji wa mafuta ya mawese, tumejipanga vipi kisaikolojia ili kuhakikisha kwamba tunaweza kuboresha au kuongeza thamani ya mawese ili yasiliwe Kigoma peke yake yaje kuliwa Dodoma pamoja na mikoa mengine na hata nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawese kwa asili tunatumia kwenye chakula, sisi watu wa Kigoma, lakini kwa sababu yanakuwa kama crude oil, watu wengine wanakuwa hawawezi kuyatumia. Sasa ukiongeza uzalishaji kama mara tatu, kama hatujajiandaa kuyatengeneza yaweze kutumiwa na watu wengi kwa maana ya kutanua soko, nina uhakika Mkoa wa Kigoma leo hii dumu moja ni Shilingi elfu kumi. Itaenda kushuka mpaka iende elfu tano elfu mbili. Kwa wale wananchi tuliokuwa tunawahamasisha walime mawese, michikichi wataanza kutupiga mawe kwa sababu mawese ni mengi, lakini hatujatanua soko la mafuta yatokanayo na michikichi ili walaji wawezi kuwa wengi. Kwa maana hiyo mengi yatakuwa Kigoma, utashangaa dumu kutoka elfu kumi itaenda mpaka elfu mbili au elfu tatu na kitakachotokea hapo wananchi wataanza kuichukuia Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri wangu katika hili, ni lazima sasa Serikali kupitia Waziri Mkuu ambaye kwa kweli amekuwa ni rafiki yetu Mkoa wa Kigoma katika hili, tuanze kujielekeza kwenye kuwekeza kwenye teknolojia, tuanze kubuni teknolojia ndogondogo za kuweza ku-refine mafuta ya mawese. Kwa kufanya hivi tutaongeza soko la mawese na hata uzalishaji utakapokuwa umeongezeka, tunaamini kwamba wananchi wataendelea kuuza kwa bei ambayo ni nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukipiga hesabu mafuta ya mawese dumu moja kama nilivyosema ni shilingi elfu kumi, lakini mafuta ya alizeti ambayo ni refined ni shilingi elfu 35 yaani ni sawasawa lita moja ya mawese unauza shilingi 2000 au chini ya hapo, lakini lita moja ya alizeti unauza zaidi ya Shilingi 7000, maana yake nini? Ukifanya double refine kwenye mafuta ya lita tano labda let say unaondoa uchafu labda wa robo lita tu. Kwa hiyo unaweza ukaona namna gani ambavyo wananchi wa Kigoma bado tunanyonywa kutokana na teknolojia mbovu na duni kwenye zao la chikichi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana maelekezo yatoke, SIDO wafanye ubunifu wa teknolojia ndogo ndogo ambazo watu wanaweza kumudu hata wananchi wa kawaida. Kama viko viwanda vya ku-refine alizeti vya milioni kumi, milioni nane, kwa nini Kigoma ishindikane, kwa nini mawese siku zote yaonekane yana rangi nyekundu. Tunahitaji teknolojia ambayo ni ya bei nafuu ili wananchi hata wa kawaida waweze kununua milioni kumi, milioni nane, waweze ku-refine mafuta ya mawese na waweze kuuza kwa bei nzuri na rafiki kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nizungumzie kidogo kuhusu reli ya SGR. Nashukuru tumeona mipango ipo clear na kwenye bajeti tunaona reflection kuanzia Dar es Salaam, mpaka Mwanza. Sasa ni zamu ya Kigoma; route ya kutoka Tabora kwenda Kigoma, ni ukweli usiopingika ukiangalia mizigo inayopita kwenye reli ya kati kwenda Mwanza na inayopita reli ya kati kwenda Kongo, ya kwenda Kongo ni mingi zaidi na kwenda Kongo unapitia Kigoma. Kwa hiyo tunachotaka na sisi kwenye hii miaka mitano, tumeona kuna mambo mengi sana, lakini nasi tunahitaji tuone kwenye makaratasi na kwenye bajeti ni kiasi gani kinatengwa kila mwaka au ujenzi wa SGR kwenda Kigoma sasa uanze.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesubiri, sasa ni zamu yetu, tunasubiri ikifika Mwanza tu na sisi tuanze kudai. Sasa Mwanza tumeona mpaka mikataba imeanza kusainiwa, juzi tumeona Waziri yupo kule, sasa na sisi Kigoma ni zamu yetu, tuone mikataba ikisainiwa, reli ijengwe kwenda Kigoma, it is our time now.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni la umeme. Kigoma sisi hatujaunganishwa na grid ya Taifa, ni miongoni mwa mikoa michache sana ambayo haijaunganishwa na grid ya Taifa, hii miaka mitano tunahitaji kuona sio story tena, mama ametupa msemo mzuri, ukinizingua nakuzingua, tunakaa humu ndani miaka mitano kwenye bajeti, Mawaziri tunawaomba wakajipange vizuri, Serikali ikajipange vizuri, tunahitaji kuona umeme wa grid ya Taifa unafika Kigoma sio ahadi tena, tutasubiri mpaka lini? Tunaposema viwanda vidogovidogo vije hivi, vinahitaji umeme, sasa kama hakuna grid ya Taifa, umeme wa jenereta wa kuwasha tu, viwanda vinakuwaje? Kwa hiyo tunaomba Serikali ijipange vizuri sana ili tupate umeme wa grid ya Taifa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sitakuwa nimetenda haki kama sitazungumzia michezo katika nchi hii. Napenda sana michezo, licha ya kuwa Mwanayanga mzuri sana, nawapoongeza Timu ya Simba kwa ilipofika kwa kweli; imejitahidi sana. Na sisi Serikali tuna tabia ya kuvizia mafanikio binafsi ya timu, sisi tunadaka, hata kama ni mazingira mazuri ya Serikali, kwa nini Simba peke yake? Kwa nini nyingine zisifike level hiyo ya Simba? Tuweke vizuri mikakati yetu kwenye upande wa michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na sehemu ya kuanzia, twende kwenye sheria za adhabu mbalimbali za TFF. TFF wana sheria kali kuliko hata za Kanuni za Bunge hili; wana sheria kali kuliko hata za ubakaji. Yaani leo hii Masau Bwire akiwa- challenge kidogo wanamfungia miaka mitano, sasa utafikaje kwenye nani? Uki-challenge kidogo, milioni tano, milioni moja, milioni ngapi; hatuwezi kwenda hivyo. Lazima waweke mazingira vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda michezo sana. Na nimekuwa Mjumbe wa Bunge Sports Club kwa miaka sita sasa. Na hata jana wakati Mheshimiwa Spika alivyotangaza kwamba fomu zinaweza kuchukuliwa, nilichukua fomu kabisa ya kugombea Uenyekiti wa Bunge Sports Club. Kwa hiyo, naamini muda ukifika hata wewe – kwasababu amesema wewe utakuwa msimamizi wa uchaguzi – muda ukifika ntaomba kura.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tujikite vizuri sana kwenye suala la michezo. Michezo ni ajira. Na kweli mimi kama ntapata nafasi hiyo ntaonesha mfano kwenye michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu jambo lingine moja, nimeona kwenye ujezi wa miundombinu, hasa barabara… ya kwanza, ya pili hiyo?

NAIBU SPIKA: Ya pili.

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Naomba kura yako.