Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

Hon. Mariamu Ditopile Mzuzuri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Ninukuu maneno ya Mheshimiwa Rais wetu Kipenzi Mama Samia Suluhu Hassan aliyozungumza pale Dodoma UDOM akiwa anaongea na viongozi wa dini mbalimbali. Alisema, Wabunge tulieni, acheni kudemka. Sasa sijui hatukumwelewa! Kwa sababu leo hii wananchi wetu wana changamoto nyingi, wanatutaka sisi Wabunge wao tuje hapa tuielekeze na kuieleza Serikali namna gani ya kuunga mkono juhudi za Rais wetu ili Tanzania ifike kwenye nchi ya ahadi. Leo hii tunapoteza masaa yote kwa ajili yao kudemka na kutafuta kiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kaka yangu Bishop Gwajima anajua ni namna gani ninampenda na tunaongea mambo mengi, lakini mimi siyo mnafiki. Nilimwandikia ujumbe mfupi kwenye WhatsApp nikamwambia kaka hapa umepotoka. Hatukatai kutokukubali chanjo; na ndiyo maana msimamo wa Serikali chanjo ni hiari, lakini mwenzetu huyu anatumia vibaya kanisa lake kwenda kuweka tuhuma nzito kwa viongozi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaposema viongozi wamepewa fedha, Mheshimiwa Rais amepokea rushwa, ndicho unachomaanisha. Ukisema viongozi wetu chanjo wanazopigwa wanadanganya, unamaanisha Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Spika ambaye kwa kweli ndio anayetuongoza hapa, Waziri Mkuu na wote waliochanja wanawadanganya Watanzania. Ni vizuri mmemwita mbele ya Kamati ameshindwa kuleta vielelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kawe kwenye chama chetu waligombea wengi. Kawe kwenye Uchaguzi Mkuu viligombea vyama vingi na alitupa mzigo mkubwa sana. Ilibidi twende Roman Catholic tufute mambo aliyoyasema, ilibidi twende kwa Waislamu tufute mambo aliyoyasema, chama kimemwamini, wananchi wa Kawe wamemwamini, ana majukumu ya kuwatumikia wananchi wa Kawe, arudi kwenye mstari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kaka yangu Mheshimiwa Jerry Silaa kwanza sisi kama vijana wenzake; sijui wasomi wenzake wanasheria, maana mimi sio penguin; tumesikitishwa mno na drama zako. Umeitwa kwenye Kamati, jishushe brother, tuna safari ndefu. Unamtunishia misuli Ndugai, mwenzako kawa Mwenyekiti, Naibu Spika, Spika miaka kumi. Kongwa mimi mwekezaji kule, wanampenda huyu hawataki hata astaafu. Umekuja na begi zima unaanza kuongea kauli za shoo shoo, umejibiwa na vitu viwili; salary slip na kitabu hiki chenye maslahi na mwongozo wa kazi za Mbunge. Unajiita Wakili Msomi, nami nili-post picha yako kabisa umevaa joho. Kaa ujitathmini, Taifa lilikuwa linakuhitaji, umeshajitia doa. Rudi kwa Mungu wako, rudi kwa wazazi wako, rudi kwa viongozi wako, chutama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli mimi niseme naunga mkono Azimio la Kamati, lakini adhabu ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa suala alilolifanya Gwajima ni uhaini. Sisi kama Watanzania tunayemwamini Rais wetu, mimi kama Mwanachama wa CCM ambaye namwamini Mwenyekiti wangu, anapaswa kupewa adhabu. Kama anaona Uaskofu ni mkubwa, atuachie Ubunge wetu. Wapo wana-CCM wengi mahiri wa kuweza kuleta maendeleo makubwa. Kawe ilicheleweshwa chini ya upinzani, tunataka iende mbali. Kwa hiyo, naomba adhabu iwe ya juu kabisa kwenye Bunge na pia hatua nyingine za kinidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama vijana tunaipenda nchi hii, hatuko tayari kuona mtu yeyote akikwamisha juhudi za Serikali yetu chini ya Rais ambaye kwa kweli siku zote mama huyu hakuchukua fomu kugombea Umakamu wa Rais; Mama huyu hakutaka Urais, alimsindikiza mgombea wake wa Urais kunadi Ilani ya Chama. Yaliyotokea ni ya Mwenyezi Mungu. Ndiyo maana tunasema ni chaguo la Mungu, hana kundi huyo. Kwa hiyo, tunaomba kwa kweli adhabu ziwe kali mno na baada ya hapo vyombo vingine vya mamlaka viwape adhabu. Hakuna lingine. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Umesahau kutoa hoja tu. (Kicheko)

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.