Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia mpango huu wa maendeleo. Naomba nimshukuru Waziri wa Fedha na Mipango kwa taarifa nzuri ya mpango huu wa maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nitakuwa sijatenda haki kama sitachangia mawili matatu ambayo naona kuna umuhimu wa kuyazungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ambalo ni muhimu ni kwamba mpango huu wa maendeleo ni makakati wa kuendelea kuwaondoa wananchi wetu katika umaskini. Ni kweli mpango uliopita umeweza kutufikisha katika uchumi wa kati lakini uchumi huu bado umekosa tafsiri chanya katika maisha ya mtu mmoja mmoja, bado umebakia kwenye Takwimu. Kwa hiyo katika utekelezaji wa mpango huo wa maendeleo naomba uende ukatoe tafsiri chanya katika maisha ya mtu mmoja mmoja ili mabadiliko ya uchumi huu tuyaone kwa macho na si kwa takwimu tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa kuliko yote mpango huu ni lazima ujikite katika ukuaji wa uchumi mpana na jumuishi wenye kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa na kuwanufaisha watu wengi hasa wanaoishi katika mazingira ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili jitihada za ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, ufufuaji wa bandari na meli kubwa kubwa na ndogo kwa kweli umeweza kuonyesha ni jinsi gani uchumi ambao tunataka uwe unakuwa jumuishi. Lakini reli hii ya mwendo kasi ambayo tunaijenga inaambatana pembezoni mwake na barabara ambayo inatumika kwa ajili ya ujenzi wa reli hii. Barabara hii imeweza kufikia vijiji vingi ambavyo awali kabla ujenzi wa reli hii vilikuwa havifikiki. Vijiji hivi ni muhimu sana katika uzalishaji wa bidhaa za mashambani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba Waziri wa Fedha na Mipango ashirikiane na Wizara nyingine kama za Ujenzi na Uchukuzi kuona barabara hii inaenda kuwa ya kudumu, kwasababu tukiiacha barabara hii tutakuwa tumepoteza kitu kikubwa na cha thamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kutoka hapa Makutopora kwenda Kilosa ni pa fupi sana ukipita kwa barabara hii ya SGR ambapo awali ilikuwa uende mpaka Dumila. Lakini kutoka Kilosa kwenda Morogoro pamekuwa karibu sana kwa kutumia barabara hii, lakini miaka minne ya nyuma ulikuwa huweze kufikia baadhi ya vijiji hata kwa pikipiki lakini kwasababu za ujenzi wa Reli hii vijiji vyote vinafikika, na unaweza kuona mabadiliko chanya katika maisha ya mtu mmoja mmoja katika vijiji hivi kwasababu ya uwepo wa barabara hizi ambazo lengo lake si kurahisisha usafiri wa wananchi ilikuwa ni ujenzi reli hii. Kwa hiyo tuiangalie barabara hii kwa jicho la kipekee kwa nia ya kubadilisha maisha ya wananchi wetu katika maeneo ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia hatuwezi kuepuka kilimo. Kilimo tunasema ni uti wa mgongo kilimo tunazungumzia kwamba ndiyo dhana ambayo inaweza kututoa katika umaskini, na kilimo ndicho kitu ambacho kinaajiri watu wengi kupita kiasi, lakini tuna changamoto ya masoko. Masoko haya ambayo tunayazungumzia mengine yanatokana na uzalishaji ambao hauzingatii mahitaji ya soko, lakini kuna maeneo ambayo kwa Sheria ama kwa taratibu ambazo tuliziweka ni kwamba zinamnyima fursa Mkulima kuwa na soko la uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano katika Jimbo la Mikumi kilimo cha miwa ndio uti wa mgongo. Katika bonde lile kuna zaidi ya tani laki nne kila mwaka zinaharibikia mashambani kwasababu mnunuzi ni mmoja ambaye ame- monopolize soko la Miwa. Miwa hii ambayo inaharibika tunaweza tukai - convert kwenda kwenye tani 40 elfu za sukari ambazo ndizo tunazoagiza kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mzalishaji huyu ambaye alikuwa anapaswa kutafuta suluhisho la kudumu la wakulima hawa kuangalia jinsi gani anaenda kununua miwa yao yeye anapewa kibali na Serikali kwa ajili ya kuagiza Sukari ambayo ni rahisi kuingiza kuliko kuzalisha, kwa hiyo tunajikuta kama Serikali tunaumiza wakulima wetu wenyewe badala ya kuwa - encourage ama kuwapa incentive ya kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunataka tumkomboe mkulima kikweli kweli basi ni lazima tuhakikishe tunamuwekea mazingira rafiki ya uzalishaji, lakini pia kumuwekea mazingira ya uhakika wa soko. Kama mzalishaji huyu ameshindwa kununua miwa hii basi tuanze kuangalia utaratibu wa kuwawezesha wananchi kupitia vyama vya Ushirika ama mmoja mmoja kupitia Benki ya Kilimo kuanzisha viwanda vidogo na vya kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeishi nchi ya Asia kwa zaidi ya miaka minne, huwezi kukuta viwanda vikubwa vya sukari. Viwanda ni vidogo vidogo na watu wanashiriki katika kilimo cha miwa lakini uzalishaji wa sukari ya miwa na viazi katika uwezo mdogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hili, ili tuongeze mnyororo wa thamani na kukuza stadi za uzalishaji wa bidhaa za kilimo basi ni vyema tukajikita katika taasisi zetu za fedha kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wakati kujiingiza kikamilifu katika uzalishaji wa sukari katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kubwa kuliko yote ni uboreshaji wa miundombinu. Tunapozungumzia miundombinu maeneo mengi ya uzalishaji wa kilimo ni mabonde na maeneo haya wakati wa masika hayafikiki. Nchi za Asia zimepata kuendelea kwasababu kwanza walihakikisha barabara zao zote ambazo zinaenda katika maeneo ya uzalishaji zinapitika mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi kama China ambayo tunaweza kuichukulia kama model ya maendeleo yetu ni kwamba wenyewe walijikita katika kuhakikisha barabara zote zinapitika kwa changarawe kwasababu uwezo wa Lami hawakuwa nao. Sisi tunaweza tuka - copy model hiyo ya maendeleo kwa kuhakikisha kwamba barabara zetu zinaweza zikapitika katika maeneo yote uzalishaji wa kilimo na kuunganisha na barabara kuu. Hilo litapunguza gharama za uzalishaji lakini litafikisha bidhaa masokoni katika bei ambayo inauhalisia na kuongeza ushindani wa bei ya soko na kuongeza tija kwa maisha ya mkulima mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia taasisi zetu za fedha ni lazima zisiseme tu kwamba zinashiriki katika kumwezesha mkulima bali pia zionekane zikifanya hivyo. Riba yetu bado ni kubwa na riba sio rafiki kwa wakulima wetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni dakika sita tu nimeweka stop watch hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika hili tunaweze kuangalia ni jinsi gani tunaweza kuweka sera rafiki kwa taasisi zetu za fedha ili kuhakikisha kwamba zinapunguza Riba lakini pia zinamwezesha mkulima mmoja mmoja katika kuongeza tija ya mazao yake pamoja na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika hili kwakweli hatuwezi kuacha utalii pembeni. Sekta ya utalii ni muhimu mno na ni uti wa mgongo. Kwa Jimbo langu la Mikumi sekta ya utalii imeajiri wengi, lakini tafiti na stadi mbalimbali zinaonyesha kwamba ni asilimia 20 tu ya watalii wanaokuja Tanzania ambao wanarudi tena, kiasi hiki ni kidogo, na hasa ukizingatia kwamba utalii ni moja ya maeneo muhimu katika ukuaji wa uchumi wetu. Kwa hiyo nilikuwa naomba Serikali iangalie ni vitu gani ambayo vinafanya watalii wasirudi hapa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuangalie tena jukumu la Bodi ya Utalii na taasisi zake ambazo zina jukumu la kuhakikisha kwamba mtalii anakuja Tanzania. Wanaboresha huduma zao wanatangaza vivutio vyetu lakini pia wanashirikisha wananchi wetu katika suala zima la sekta hii ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika hili miundombinu katika mbuga zetu na hifadhi zetu hatuwezi kuliweka kando. Pale Kilosa ama katika Mbuga ya Mikumi kuna geti moja tu la kuingilia mbugani; lakini tunasema tuna reli ya SGR ambayo inakuja mpaka Kilosa. Unaposhuka Kilosa kwa SGR maana yake unaenda kuongeza idadi ya watalii ambao wangependa kuja Mikumi lakini mtalii huyu angeweze kuja akaingilia katika geti la hapa Tindiga ama Mabwelebwele ama Kilangali ambako ni kilomita 15 kutoka stesheni ya reli ya SGR. Sasa kwa sababu ya kutokuwa na geti pale na kwa kutokuwa na barabara ya kuingilia pale mbugani unamsababisha mtalii huyu atembee kilometa zaidi ya 120 kabla hayakutana na geti.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunapozungumzia miundombinu ni pamoja na kurahisisha usafiri kwa watalii lakini pia kumpunguzia muda na kuongeza thamani ya fedha zake kwa kulinda muda wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo si kwa umuhimu wake ni suala zima la kwanini tulishindwa katika mipango yetu ya maendeleo huko nyuma. Mipango ya awali ilishindwa kufanikisha malengo yake mengi ilhali Serikali ilikuwa imedhamiria katika ukuzaji wa viwanda kama kipaumbele chake cha miaka mitano iliyopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais imefungua maeneo mengi ambayo yanahitaji mjadala wa kina. Moja ambalo ni kubwa mazingira yetu ya uwekezaji si rafiki kwa sababu hatuangalii Watanzania kama sehemu muhimu ya wawekezaji, lakini pia masharti yetu yakufungua biashara yamekuwa magumu mno. Tuna taasisi nyingi ambazo mfanyabiashara ama Mwekezaji anapaswa kuwasiliana nazo kabla ya kufungua biashara yake; matokeo yake uwekezaji umekuwa ni wa gharama kubwa mno Tanzania ukilinganisha na washindani wetu katika maeneo ya Maziwa Makuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika uwekezaji Watanzania wote lazima wapewe kibaumbele bila kujali maeneo yao ya kijiografia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia mpango wa maendeleo haujazungumzia diaspora. Diaspora ni eneo kubwa na muhimu sana katika uwekezaji wa ndani. Ninaamini kabisa hapo awali tulishindwa kutumia kikamilifu rasilimali watu hasa ndugu zetu wa diaspora ambao wana skills lakini pia wana access ya mitaji katika maeneo ambayo wapo. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango anapohitimisha hotuba yake atuelezee ama alielezee Bunge lako ni jinsi gani wanaenda kuangalia Watanzania kama significant players katika uwekezaji, hasa hawa ndugu zetu za diaspora.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)