Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ili niweze kuchangia hoja ambayo Yanga mwenzangu ameileta ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa kwa miaka mitano hadi mwaka 2025/ 2026.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kuunga mkono hoja hii na nina sababu kadhaa za kuunga mkono na wakati huohuo kuleta mapendekezo ambayo naamini kabisa kwa namna moja au nyingine yataweza kuboresha Mpango huu ambao leo tunaujadili. Nitaanza na hii dhana ya Serikali Sikivu. Mpango wowote ambao Serikali inaubuni ni lazima isikilize maoni kutoka kwa wachangiaji, hasa kutoka kwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, Serikali Sikivi imeoneshwa vizuri sana na Mheshimiwa Rais Samia naamini kwa kusikiliza mchango tuliokuwa tunautoa mwezi wa pili. Tulizungumza kuhusu ufanyaji kazi wa TRA na jinsi gani TRA inavyotukosesha mapato pale ambapo taratibu za ukusanyaji wa mapato zinavyokuwa sio sahihi. Vilevile tukazungumza suala la baadhi ya biashara kufungwa kutokana na ugumu wa ufanyaji kazi, Mheshimiwa Rais alichukua hatua za haraka sana. Naomba tumpongeze Mheshimiwa Samia kwa kusikiliza, hii ndiyo maana thabiti kabisa unapozungumzia Serikali Sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeonesha mwelekeo mpya huko nje business community imekuwa na imani kubwa sana na Serikali. Nina imani kabisa kutokana na imani ambayo inajengwa sasa wasaidizi wa Mheshimiwa Rais akiwemo ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu Mchemba atasikiliza vizuri hoja zetu ambazo tunazileta uzichuje, zisaidie huu Mpango ili uwe bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala zima la maendeleo, nataka nimuangalie Mheshimiwa Hayati Julius Nyerere ambaye aliwahi kuzungumza na akatoa kauli ni nini maana ya maendeleo. Hili limekuwa likizungumzwa pia na Waheshimiwa Wabunge katika Mabunge mengi yaliyopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hayati Nyerere anasema: “Maendeleo hayawezi yakawa maendeleo kama sio people centred.” Maendeleo lazima yaguse watu ndipo yatakuwa ni maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haina maana vitu sio sehemu ya maendeleo, hapana, vitu ni sehemu ya maendeleo, lakini lazima i-translate na ishuke chini kwa mwananchi mmoja- mmoja. Hapo ndipo panapotuletea maelezo ama swali, je, Mpango huu unamgusa vipi mwananchi wa kawaida? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tuangalie hapo kwamba, Mpango huu lazima uwe na vielelezo vinavyopelekea mwananchi wa kawaida kusema naam, Serikali inakuja na mpango ambao utanigusa mimi, yule na mwisho jumuiya nzima ya Watanzania watafaidika na mpango huu. Yote haya ambayo tunayasema yanaelekea katika maeneo mazima ya uhuru wa watu kuweza kufanya biashara zao, kufanya kilimo chao katika nchi yao, kupata mazao ambayo wanaweza wakayapeleka nje wakaenda kuyauza. Hata utawala wa kisheria kwa sababu, kuna wakati tulilalamika sana hapa yale ambayo yanapangwa katika sheria nayo hayatekelezwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwepo na mjadala mkubwa sana, sitaki nirudie huko, mjadala ambao ndugu yangu msemaji wa mwisho alizungumzia wa korosho ule uliumiza watu wengi sana. Turudi katika utawala ule ambao tumejiwekea sheria zetu na zile sheria tuzifuate. Naamini kwa muelekeo ambao umeoneshwa na Mheshimiwa Rais ni dhahiri kabisa haya sasa yanakwenda kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Serikali imezungumza mambo mengi sana humu ndani, lakini Mpango huu lazima uwe ni unaotekelezeka. Tunataka Serikali itakavyokuja kufanya majumuisho itueleze ni namna gani imejitayarisha kuhakikisha kwamba inaitumia sekta binafsi ambayo ndiyo itakuwa ni moja kati ya wabia wakubwa katika Mpango huu. Ukiangalia numbers zinaonesha shilingi trilioni 40.6 zitatoka katika mchango wa sekta binafsi, lakini hata ule mchango wa Serikali wa shilingi trilioni 74.2 mchango ule utatetegemea vilevile sekta binafsi, Serikali haifanyi biashara. Ili 74.2 trillion shillings ziweze kukusanywa lazima business community hapa sasa iweze kuangaliwa na kuwa natured vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo, napenda nione kwamba, mchango wa Serikali katika kuhakikisha kwamba business community inalelewa vizuri uweze kuelekeza vizuri zaidi na Mheshimiwa Waziri aje kutuambia maana kuna kitu kimoja mimi kimenitia moyo, lakini kimenisononesha. Tuna watu wazuri sana katika nchi hii katika mawazo mema ya kufanya biashara na hapa nimpongeze Mpinzani wangu Mohamed Dewji ambaye tumesikia ameteuliwa na Rais wa South Africa kuwa ni mmoja kati ya watu ambao watamshauri. Sasa kama tuna mtu kama yule ndani ya Tanzania ambaye wenzetu wanamuona, sisi tunawatumiaje watu kama hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndipo sasa naiomba Serikali na napendekeza kwamba ni wakati umefika sasa Serikali ikaunda angalau timu ya wataalamu pamoja na wafanyabiashara mashuhuri, wakiwemo watu kama Mohamed Dewji, watueleze tufanyeje ili tuweze kufanikiwa zaidi katika suala zima la uwekezaji katika nchi yetu. Tuangalie tu, tusemeni kweli, Kamati ya Bajeti inazungumzia kwamba haijaridhika kuona kwamba Tanzania ni nchi ambayo si nyepesi ya kufanya biashara na wakatoa numbers wakasema tuko nafasi ya 141. Hata Mpango ule unaomalizika sasa ulikuwa unajitahidi kuifanya Tanzania iwe ndani ya nchi 100 katika wepesi wa kufanya biashara, lakini hatukufika huko. Ni vikwazo gani vilivyosababisha Tanzania isiweze kuingia katika zile nchi 100 zenye wepesi wa kufanya biashara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Serikali itakapokuja Mheshimiwa Dkt. Mwigulu atueleze ni vitu gani ambavyo watavifanya kuhakikisha Tanzania inakuwa ni moja kati ya nchi ambazo ni easy to do business, ili wawekezaji waweze kuvutika na wakaja. Kwa sababu bila wawekezaji ukweli ni kwamba tutapata maendeleo, lakini yatachelewa na tusingependa kuchelewa. Mkumbuke Rais wetu aliyepita, Hayati Mheshimiwa Magufuli, aliisababisha Tanzania kwa haraka zaidi kuingia katika Uchumi wa Chini wa Kati, miaka mitano kabla. Naamini kabisa Mheshimiwa Suluhu Hassan atatusogeza mbele zaidi ya pale ambapo Mheshimiwa Hayati Magufuli ameacha, kama mipango hii mizuri ambayo imewekwa itaweza kutekelezwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho napenda nizungumzie kuhusu ahadi za viongozi wetu wakuu. Wananchi wana imani sana na Serikali, wana imani sana na viongozi wao wakuu. Leo hii Wabunge tumekuwa tukilalamika sana tunazungumzia barabara za miaka mitatu, minne, mitano ambazo Mheshimiwa Rais alitoa ahadi. Sasa tusiende mahali tukafikia kwamba viongozi wetu wakitoa ahadi wananchi wa kawaida waseme, aah, haya ni kama yale yaliyopita, lazima tuyaangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nampenda sana, kwa hiyo, napenda nione safari hii tunabadilisha mwelekeo, viongozi wakuu wakitoa ahadi zao wasaidizi wake wawe ni hodari wa kuzipokea na kuzifanyia kazi. Hatutataka tuje tukumbushie miaka mitatu iliyopita. Mheshimiwa Rais kama anayasikia haya nitaomba awape support ya kutosha Mawaziri wake katika suala kama hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemaliza na nilisema naunga mkono hoja hii, ahsante sana. (Makofi)