Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona na napenda kwanza nimshukuru sana na nimpongeze Waziri wa Fedha na timu yake pamoja na Kamati ya Bajeti kwa namna ambavyo wamewasilisha Mpango huu. Natumaini wote imetufurahisha. Nataka nianze kwa kusema kwamba naunga hoja yake mkono, japokuwa nitakuwa na maoni mawili au matatu ili kuweza kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme hivi kwamba kusema ukweli kwanza tunawapongeza pia Wizara na Serikali kwa ujumla kwa kuweza kutuwekea uchumi wetu kwenye hali ya utulivu. Tunajua kwamba ukuaji umekuwa mzuri sana, hata wakati huu wa covid, lakini pia mfumuko wa bei uko chini, uko vizuri, japokuwa namuunga mwenzangu mkono aliyezungumza kwamba pengine asilimia tatu ni ndogo sana, inatunyima fursa fulani ya kuweza kukuza zaidi kwa kuipa Sekta Binafsi na wale wanaouza, nafasi ya kuona faida watakayopata wakiendelea kuzalisha Zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeona kwamba hali ya deni la Taifa ni himilivu. Pili, tunaona pia kwamba thamani ya shilingi yetu iko vizuri na pia tuna International Reserves ambazo ni nzuri. Hiyo ina maana kwamba ni strength kubwa sana ambayo tunaweza tukaitumia tukafanya assessment ya nchi yetu kwa athari ya wawekezaji na hivyo tukaanza kukopa kwa riba ya chini sana. Riba ya asilimia tano au sita unaweza ukapata kwa mfumo huo wa infrastructure bond au pia kwa kukopa moja kwa moja kwa direct placement ya bond yetu kwa wale wanaotaka kuwekeza Tanzania kwa sababu Tanzania imekaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niseme kwamba hakuna sababu ya kuchelewesha utekelezaji wa miradi elekezi. Hii miradi tunasema ya vielelezo kama SGR na mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere wakati tunaweza tukakopa, tukahamasisha na tukafanya haraka haraka tukaanza kuona matunda kutokana na miradi hii mikubwa ambayo itatoa chachu katika ukuaji wa Taifa letu. Nataka niseme kwamba tutumie hiyo kama fursa, kama ni strength na hiyo strength tuweze kuitumia kuweza kufanya mchakato huo wa kuweza kwenda kwenye soko la Kimataifa na kukopa na tusizingatie sana kukopa ndani kwa sababu tukikopa ndani maana yake tunai-crowd out private sector. Watu binafsi hawawezi kwenda nje kwa sababu hawajulikani, lakini Serikali inajulikana kwa sababu ni Serikali na Serikali is as good as gold.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini tukihamasika sisi Serikali tukakopa nje, tukaacha resources za ndani zinakopwa zaidi na watu binafsi, kwanza riba zitakuwa chini. Sasa hivi tuliambiwa kwamba riba nashangaa kwamba licha ya vigezo hivi vizuri vya uchumi, riba bado ziko kwenye asilimia 15. Nimekutana na watu wa BOT walituambia kwamba kwa sababu tunakopesha Serikali kwa asilimia 15, sio kweli! Serikali inalipa asilimia 15 kwa bond ya muda kati ya miaka 15 na 20, lakini Benki zinakopesha mikopo ya mwaka mmoja mpaka miwili sanasana pengine ni michache sana kwa miaka zaidi ya hapo. Sasa wakikopesha kwa asilimia 15 ni kubwa sana ambapo Serikali ikikopa kwa kipindi hicho kifupi riba inakuwa ni kwenye asilimia chini ya 10. Kwa hiyo unaona kwamba kuna uwezekano wa kushusha hizi riba kwa kuwezesha Sekta Binafsi kukopa zaidi na hivyo kuwezesha Sekta Binafsi kuwekeza na tukaona matokeo ya Mpango wetu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kitu kimoja ambacho nimekisikiliza hapa. Tunafanya mambo kimazoea mazoea sana, yaani tatizo la sisi Waafrika pengine ni kwamba tunaanza kuzalisha halafu ndiyo tunatafuta soko. Kumbe uzalishaji unatakiwa uanze sokoni, unatafuta soko liko wapi. Ukishaona soko liko wapi na bei zake zikoje, ndiyo unasema sasa niki-incur au nikitumia gharama hizi kuzalisha nitapata faida, lakini mtu anazalisha ndizi heka 20 halafu zimeshaiva, anasema anatafuta soko liko wapi, hamna soko lolote namna hilo, huwezi kupata na mtu akijua unazo ndizi zinaoza anakupa bei ya chee! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tujifunze kufanya biashara kitofauti kwanza tufanye utafiti tujue kwamba ni kitu gani kinauzika wapi. Tunapoendelea kulima, tunazungumzia mazao haya ya asili siku zote, pamba, kahawa, tumbaku. Hivi tumeshajiuliza ni wapi masoko haya yakoje duniani kwa sasa hivi? Bei za huko mbele za kahawa zinaenda wapi, bei za tumbaku zinadidimia na tunaendelea kusema tumbaku na kadhalika. Ukweli tukifanya tathmini sahihi tukajua kwamba ni kitu gani cha kuzalisha hapa kwetu, sio lazima iwe ni mazao haya tunayoona, tumeona kwamba tulivyowaambia Wachaga kule kwamba hawa jamaa wenzetu wa Kyela wanalima avocado halafu wanapata kilo moja shilingi 1,500; kila mtu anatafuta mbegu ya avocado, huna haja ya kumtafutia mbolea, anatafuta mwenyewe kwa sababu anajua kwamba ina faida kulima avocado.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa na taarifa hizo lakini ukweli ni kwamba taarifa hizi hazimfikii mkulima, tunakaa na hizo taarifa, hujui kwamba unaweza sasa badala ya kulima kahawa ukalima avocado, kwa nini? Ukiendelea kulima kahawa kwenye ule udongo wa kule kwetu umeshakwisha kabisa kwa sababu umelima kahawa miaka 40 au 50, kwa hiyo hauna tena rutuba na hauna tija. Kwa sababu hauna tija badilisha uzalishe linguine, baada ya muda mwingine unaweza ukarudia tena kahawa na ndiyo mambo ya crop rotation, wale wanaojua mambo ya kilimo. Kwa hiyo naweza kusema kwamba pengine kuna haja ya kusema kwamba ni eneo lipi nibadilishe zao lile, kama kule Uchagani kahawa haiendi tena, pengine twende upande wa avocado na mambo kama hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine pia unaona kwamba unatumia gharama nyingi kwa sababu ule udongo unatakiwa ufanye rotation, uzalishe kitu kingine. Naamini kwamba tunaposema tutafutiane masoko, cha kwanza ni hizo taarifa na hizo taarifa sasa hivi ni kielektroniki, tufungamanishe masoko yetu. Mtu hajui kwamba kama nina ndizi, Mbeya wananunua namna gani ndizi, Moshi wananunua namna gani, Nairobi wananunua namna gani kwa kutumia hizi gadgets zetu za mawasiliano hizi ambazo zinatupa bei kila mahali duniani virtually unaweza ukajua kila kitu kinauzwa namna gani. Kwa hiyo watu watajua bei zake na sio lazima ukutanishe mtu physically, unaweza ukakutanisha watu kwa mawasiliano haya tuliyonayo na hiyo ni bei nafuu ya kukutanisha watu, ni bei nafuu ya kumpa mtu tija ya kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hivi, mimi nafikiri kwamba katika huu Mpango wetu, suala zima la ushirikishi, kujenga uchumi shirikishi na uchumi shindani. Issue iliyopo ni kwamba tutafanyaje vijana hawa wapate ajira na hawawezi kupata ajira bila kujiajiri wenyewe sasa hivi kwa sababu watu ni wengi ambao hawana ajira na hawataki kuingia kwenye kilimo kwa sababu kilimo hakina tija na kwa sababu hawajafundishwa namna ya kulima kwa tija au kwa faida. Kwa hiyo naomba hivi, kwamba pengine umefika muda sasa tujaribu kutengeneza mfumo wa kuwa-organize vijana kwenye vikundi na kuwaonesha namna gani ya kutengeneza mashamba yenye tija, kutengeneza viwanda vidogo vidogo vyenye tija na mtu asifikirie kwamba kiwanda ni kiwanda cha Mchuchuma, hapana. Tena sasa hivi hata kuzungumza mambo ya chuma ni kitu tofauti kidogo kwa sababu dunia haiendi kwenye mambo haya, inaenda kwenye software zaidi sasa hivi, kwa hiyo Sekta ya Huduma ndiyo itakuja kuwa ni sekta muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Huduma maana yake ni sekta ya kuhudumia viwanda, kwa sababu ukiwa na kiwanda lazima kihudumiwe, maintenance na kadhalika. Sasa kama wewe unakimbizana tu hiki unasahau kule, haitawezekana, lazima tuingize fedha, lakini ili vijana waweze kufanya hivyo wanahitaji mtaji, mtaji unatokana na nini? Tunasema tutawapa vimikopo vidogo dogo kwenye halmashauri, haina kitu hiyo! Tuunde ile Mifuko ya Serikali ambayo imetawanyika kila mahali, tuunde National Credit Guarantee Scheme or Fund au kuwe na misingi ya kibiashara lakini nafuu ambayo itakuwa imewekwa na Serikali ili watu wanaotaka mikopo wanajua tunaenda pale ambapo kutakuwa na kitengo cha wakulima, vijana, vinakaa mahali Pamoja. Pia unaweza uka-leverage ile guarantee scheme ikazalisha maradufu kwa sababu kama default rate kwa mkopo, hiyo iliyotoka kwa vijana pengine ni only ten percent ina maana kwamba ukiwa na mkopo wa ku-guarantee watu 100 unazidisha mara 10, uta-guarantee watu mara 10 yaani kiasi cha fedha mara 10. Sasa hivi unatumia kile unam- guarantee mtu mmoja ambapo tunaweza tukapeleka kwenye guarantee fund tukawapa watu wakaendesha kibiashara, tukaweza kuwezesha watu kupata mikopo kwa wingi na mitaji kwa wingi kwa muda mrefu na muda mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba, mimi ni muumini wa masuala ya kwamba, kilimo cha sasa hivi ni lazima kibadilike na kubadilika kwa kilimo hicho ni lazima tusifanye mambo ya mazoea, tujaribu kuona ni kitu gani kitaoteshwa wapi na wakulima wapewe taarifa za masoko ambayo ni sahihi. Kwa kumalizia niseme hivi, ili tuweze kuongeza lile fungu la kukopesha au kuwezesha watu kupata mitaji, lazima tuunde National Credit Guarantee Fund or Corporation ambayo itashughulika na Mifuko yote na ile fedha inakaa mahali pamoja na inatumika kwa faida ya wengi. Hapa nataka kukuhakikishia kwamba inaweza ikawa ni kubwa kuliko Benki zote hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. (Makofi)