Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nakushukuru kwa ajili ya kunipa nafasi hii. Pia nitoe pole kwa Watanzania wote kwa msiba mkubwa uliotufika. Kimsingi nimesimama mbele yako niweze kuchangia kidogo, lakini niweke msisitizo; naingia moja kwa moja kwenye Sekta ya Kilimo. Natamani kila mtu akisimama aweze kuona upana na ukubwa wa sekta hii ili tuweze kuweka nguvu inayohusika katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme sekta ya kilimo inaweza kuchukua asilimia 56.5 ya ajira zote za Watanzania. Nikienda kwenye asilimia; nakwenda kwenye asilimia 20 ya mauzo yote ya nje. Unaona hapa kidogo kuna ufinyu, kwa sababu sekta hii haijachukuliwa kwa uzito wake. Ikichukuliwa kwa uzito wake, hatutalia ajali za boda boda barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa Nairobi wameweza kutenga SACCOSS maalum, wakakusanya vijana katika makundi na wanatengeneza mfumo wa kununua daladala kule wanaziita matatuu ili waweze kuwekeza. Sisi tuna ardhi kubwa ambayo ina rutuba, tuna maji. Kwa mfumo wa umwagiliaji, kama hatuna ile miundombinu, lakini tuangalie hizi mvua zinazonyesha, tunalia mafuriko; haya maji yanayotokana na mvua tungeweza kuweka pale miundombinu ya umwagiliaji tukavuna yale maji yakatusaidia kwenye kumwagilia, tusingelia leo mambo ya mafuta, tungewekeza kwenye alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa hawa vijana wanaokufa kwa boda boda hawajapata Plan B za ajira. Wakipata Plan B hatutalia vifo hivi, kwa sababu kila kijana anafikiria ajira ni boda boda. Pia tungeweza kuwapa elimu, wakaweza kuwekeza kwenye kilimo ambao ni asilimia kubwa sana, hawa vijana wangetoka na wangekwenda kusimama na utaona uchumi unakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuomba, kuna benki ambazo zinatoa mikopo kwa wakulima, benki hizi hazijaona vijana. Vijana hawawezi kuwekeza kule kwa sababu wanaonekana hawana thamani fulani hivi. Labda wawekwe kwenye vikundi ili waweze kwenda kwenye benki hizi waweze kukopeshwa au waundiwe SACCOSS zao maalum waweze kukopa maana hawana dhamana, ndiyo maana hawakopesheki.

Mheshimiwa Spika, kijana wa Tanzania hata akienda mahali anaonekana muhuni tu, lakini ni Mtanzania ambaye kimsingi tukimpa mbinu, tukampa elimu, tukawekeza kwenye kilimo, hawa vijana wasingelia leo. Kingine, akina mama wengi wanalima kwa jembe la mkono, hawalimi kilimo chenye tija. Hata wakilima hiki kilimo chenye tija, hawajui zao ambalo wanaweza kulima liweze kwenda nje. Tuwekeze kwenye tafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiwekeza kwenye tafiti, tukalima kilimo chenye tija, tutamkomboa mkulima mdogo na mkubwa na wote tutasimama. Niweze kusema hili suala kwa sababu tuna akina mama wengi wanalima kila siku ni kilio. Analima anaambiwa tu kwa maneno, kwa nadharia kwamba kilimo kitakukomboa, lakini haoni ukombozi wa kilimo hiki.

Mheshimiwa Spika, tukienda vijijini tukakusanya akina mama tukawapa elimu, wakalima kilimo ambacho kitakidhi vigezo kule nje, kwa sababu akina mama wengi wanalima, wanaweka mbolea ya chumvi chumvi, wakija kupima wanaona zao hili halifai. Tuwape elimu. Tuna mifugo; tuchukue mbolea za mifugo, tuweke kwa akina mama wale tuwekeze kwenye tafiti, leo kina mama tutawainua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa ninachoweza kusema kwenye sehemu ya pili ni mambo ya demokrasia. Mheshimiwa ameongea juu ya kuimarisha demokrasia, usawa na amani. Kuna watu wenye makovu, wana makovu yaliyopita huko nyuma. Tuna mategemeo; Tanzania, Taifa hili sasa hivi lina mategemeo makubwa na Rais wa sasa, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu. Lina mategemeo makubwa kutokana na kauli zake, wanasema kimjazacho mtu moyoni ndicho kinachotoka kwenye kinywa chake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu ameonyesha kunyesha suluhu kwa Watanzania. Kwa hiyo, Watanzania waliokata tamaa wamekuja kivingine. Niwaambie, kuna watu walikuwa wanagugumia, wanalia, wanashika matumbo, leo wanatembea vifua mbele, hata hawajaona kitu, kwa kauli ya kiongozi wetu mkuu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu. Nampongeza lakini tumwombee kama Watanzania mama huyu asimame kwa hizi kauli anazosema azisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipindi kilichopita, watu walipata makovu. Kuna Watanzania wanaogopa kuja kwenye nchi yao, kuna Watanzania wana kesi za kubambikiwa, za kisiasa zisizoisha, kesi hazina ushahidi zinapigwa tarehe, hatuwezi kuzizungumzia. Mheshimiwa Mama Samia Suluhu amesema kesi zile zifutwe. Niweze kusema jambo moja, kwenye demokrasia wanasema, bila haki kuonekana inatendeka, demokrasia itakuwa inambwela mbwela. Najua kwa kipindi hiki cha mama yetu, demokrasia itakwenda ku-take place na haki za watu zinaenda kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba mamlaka husika na viongozi ambao wako hapa wenye dhamana waweze kuangalia hii michango ya Wabunge. Wabunge wanachangia kutokana na mambo yanayowakuta huko na wananchi wao, tuweze kuyachukua kwa u-serious ili tuyatekeleze ku-reflect kule nje ambapo tunapotoka. Vinginevyo tutakuwa tunaimba mapambio na mambo hayachukuliwi, yakibaki pale pale tunaonekana huku tunakuja kula bata, lakini huku tumesimama kwa ajili ya wananchi wetu. Tunaomba yachukuliwe kwa u-serious ili yaweze kutekelezwa na wananchi waweze kuona matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)