Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Nichukue fursa hii ya kipekee kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini vile vile nitoe pole kwa familia ya mpendwa wetu Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Pia nitoe pole kwa Watanzania wote, niwape pole Mheshimiwa Spika na Naibu Spika, niwape pole Waheshimiwa Wabunge wote. Kila mja hakika kwake atarejea, Mwenyezi Mungu ampokee Kiongozi wetu ampokelee kitabu chake kwa mkono wa kulia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mambo mengi ya kuweza kuongea kwa mpenzi wetu mpendwa wetu baba yetu Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli, kwetu Watanzania alikuwa kama taa, alikuja kwetu amefanya kazi akiwa kama taa, ameimulika Tanzania, amemulika vijana wa Tanzania, amemulika wanawake wa Tanzania, amemulika rasilimali za Tanzania, amemulika miradi ya Tanzania, amesimamia rasilimali za Tanzania akiwa yeye kama tochi, kama taa yenye mwanga mkali, kila Waziri aliyefanya kazi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliiona taa inapomulika anajua hapa pana jambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, walisimamia kwa sababu kwetu alikuwa ni taa, lakini simuoni kama taa tu, haitoshi kwetu kuwa taa, alikuwa barabara, alikuwa njia, tumepita viongozi vijana akituonesha na kutufunza huu ndiyo uongozi, akitufunza ujasiri, akitufunza jinsi kiongozi anavyopaswa kuwa, ametufunza kuwa wakakamavu, ametufunza mambo mengi, kwangu nimeona kama ni njia, kwetu amekua njia. Nadhani wengi ni mashahidi Watanzania walipokuwa wakitembea barabarani alikuwa njia, kwetu sisi tumepita kwake kama njia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwetu amekuwa faraja, alikuwa faraja ya wanyonge, alikuwa jibu la wanyonge, alikuwa jibu la maskini, alikuwa jibu la akinamama wajawazito, alikuwa jibu la kumtua mwanamke ndoo kichwani. Kwetu alikuwa jibu, Mungu alimleta kwetu japo amefanya kazi kwa muda mfupi, lakini naamini dhamira yake ya kweli ametuacha sisi tumalize kazi. Tutahakikisha tunamuenzi kwa kupita kwenye njia ambazo yeye alitaka tupite, tutamuenzi kwa kuwa mwanga na sisi viongozi tuliokuwemo humu kama yeye alivyoangaza. Naamini Waheshimiwa Mawaziri wamekuwa na vitu vingi kutoka kwake wamekuwa na mitazamo mingi kutoka kwake watafuata njia ambayo yeye alitaka sisi tupite.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kwa jinsi ya kipekee nimpongeze Mama yetu, Mama Samia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niseme Mama Samia Mheshimiwa Rais alikuwa tuko naye hapa Bungeni, sisi tukiwa kama wanawake hatuna hofu juu yake, hatuna mashaka juu yake, tuna uhakika atatuvusha na tutafika salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka, kama kumbukumbu zangu ziko vizuri, kuna maneno ndani ya nafsi yangu kila ninapokaa yanakuja mara kwa mara, siku Mheshimiwa Mama Samia tuko kwenye kama sikosei kwenye kuapishwa, Waziri Mkuu mara hii tuko Ikulu alipata fursa ya kuzungumza, alizungumza maneno machache, lakini wakati anazungumza Mheshimiwa Rais wetu Hayati Dkt. Magufuli alikuwa yupo amekaa kitako, akatuambia baba umetufunza, tulichelewa kukufahamu, lakini kwa sasa tumekufahamu, tumekuelewa, alimwambia maneno hayo akiwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Magufuli Hayati alikuwa yu hai aliyazungumza mazungumzo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mazungumzo yale ndani ya nafsi yangu aliyoyazungumza Mama Samia yanaimba ndani ya nafsi yangu nikiamini kama aliweza kuyatamka akiwa yu hai, akisema tumekufahamu, tumekuelewa tutachapa kazi tuko na wewe, naamini hata sasa ndani ya nafsi yake bado maneno hayo yapo na ya hai, yanafanya kazi. Tuseme sisi kama wanawake tunamuunga mkono, kama Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunamuunga mkono na tutafanya naye kazi. Tuwatoe hofu Watanzania uwezo na ukubwa wa kufanya kazi Mama Samia unatosha, tutafanya nae kazi kwa jitihada zetu zote. Akiwa mama amebeba uchungu wa wanawake wote anao, akiwa mama amebeba uchungu wa watoto, akiwa mama amelibeba Taifa kwa uchungu wa mama anaugua na Taifa akiwa kama mwanamke hatuna mashaka nae. Tunajua anaumia kama mwanamke, tunajua atapita kwenye misingi aliyopita Rais wetu, tunajua atatembea kwenye misingi ya Rais wetu, hatuna mashaka nae. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuseme tunachukua fursa hii tena kumpongeza tunamtakia kila heri, Mwenyezi Mungu amnyooshee, ampe kauli ambazo Taifa letu linataka, ampe majibu ya Watanzania, aendelee kusimama nae akiwa kama mwanamke, lakini kama alivyosema maneno yake yeye ni mwanamke wa jinsia kwamba yeye ni mwanamke, ila anauwezo wa kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo maneno machache naomba nichukue fursa hii ya kukushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)