Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HASNA S. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nichangie kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu Kigoma Kusini lina jumla ya shule za msingi 119; lakini kati ya hizo tuna shule nne zina darasa moja na zingine zina madarasa mawili. Kwa kweli hali ya shule hizi inatisha; nyumba za walimu hakuna, nimwombe Mheshimiwa Waziri, aliangalie Jimbo la Kigoma Kusini kwa jicho la huruma ukizingatia miundombinu ya barabara kuwafikisha walimu kutoka wanakopanga nyumba hadi kwenye shule ni mibovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri ahakikishe bajeti ya Halmashauri ya Uvinza inakuja bila kukosa kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017. Wilaya ya Uvinza tuna shule mbili za A-level na O-level za Lugufu Boys na Lugufu Girls; nimuombe Mheshimiwa atusaidie kuzisajili kuwa ya bweni ili ziweze kupata mgao wa chakula kwani tangu zianze zimekuwa ni za bweni ilhali zilisajiliwa kama za kutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe pia Mheshimiwa Waziri, atusaidie kusajili shule mbili mpya za sekondari za kata za Mloakiziga na Basanza. Kwani wanafunzi wa kata hizi mbili wanatembea zaidi ya kilometa 15 kufuata sekondari za kata za jirani. Kwa kuwa hizi ni nguvu za wananchi tuiombe Wizara ijitahidi kuzisajili japo kuwa hazijakuwa na miundombinu yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie pia uhaba wa vyoo. Kwenye shule zangu za Jimbo la Kigoma Kusini niombe pesa za ujenzi na ukarabati zielekezwe kama tulivyoomba kwenye bajeti ya Halmashauri ya Wilaya kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uhaba wa nyumba za walimu ni tatizo kubwa ndani ya Jimbo langu. Sambamba na haya niombe Wizara ituletee walimu kwani Halmashauri ya Wilaya, bado ina uhaba wa walimu hususani walimu wa sayansi na walimu wa kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nitoe pongezi kwa dada yangu Mheshimiwa Waziri Profesa Joyce Ndalichako, kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais, kuteuliwa kuwa Mbunge na kupewa dhamana ya kuiendesha Wizara hii nyeti ya kufuta ujinga kwa watoto wetu. Nizidi kukuombea afya na achape kazi kwani wanawake tukipewa nafasi tunaweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.