Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nasimama hapa jioni hii ya leo kutoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa msiba mkubwa ambao umelipata Taifa letu. Natoa pole kwako wewe mwenyewe Naibu Spika na Spika wa Bunge letu. Natoa pole kwa Wabunge na Watanzania wote kwa msiba huu uliotupata. Ni msiba mkubwa ambao kwa kweli umetutikisa, lakini nashukuru kwamba tunaendelea vizuri kama Taifa. Ni jambo la kumshukuru Mungu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku ya Ijumaa tarehe 26 nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu kutoka Australia. Alinipigia simu kutoka Australia akiniambia kwamba, ameshuhudia bendera katika taifa lile zikipepea nusu mlingoti. Nilifurahi sana moyoni mwangu nilipojua kwamba bendera ile ilikuwa inapepea nusu mlingoti kwa sababu ya rais wangu Hayati John Pombe Magufuli. Ni jambo la kujivunia sana na kwa kweli sio jambo dogo kijana kutoka Chato kufanya bendera za dunia hii zipepee nusu mlingoti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kama raia wa nchi hii ambaye nina kila sababu ya kujivuna kuwa na kiongozi kama Mheshimiwa Magufuli ambaye alijitoa sadaka, alijitoa uhai wake, alijitoa nafsi yake kwa ajili ya Watanzania masikini wa nchi hii. Amefanya mambo mengi ambayo siwezi kuyataja yote, wote mnayafahamu. Ameuthibitishia ulimwengu ya kwamba Tanzania inaweza kuendesha mambo yake bila kumtegemea mzungu. Tanzania inaweza kujenga reli yake yenyewe bila kutegemea mkopo. Tanzania inaweza kujenga bwawa la umeme bila kutegemea msaada wa mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni jambo kubwa. Kwa miaka mingi sana tumeishi tukiamini ya kwamba sisi ni watu masikini, hatuwezi kufanya lolote bila msaada wa mzungu, lakini Mheshimiwa John Pombe Magufuli amezunguka nchi hii akiwaambia Watanzania nchi hii ni tajiri. Nimesimama hapa leo napeleka ujumbe kwa dunia nzima wapate kuelewa ya kwamba, mimi Erick Shigongo sitoki Taifa masikini, ninatoka Taifa tajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilifika mahali anakuja mzungu hapa mbeba mizigo tu kule, lakini ukimuona unaona kwamba ni msaada. Sisi Watanzania, sisi waafrika, tunao uwezo wa kujiletea mabadiliko wenyewe bila kumtegemea mzungu wala mtu mwingine yeyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inakwenda kwa kasi. Nchi yetu leo iko kwenye uchumi wa kati. Ni kweli, ziko nchi zilizoingia uchumi wa kati, lakini baadaye zikarudi nyuma kuwa masikini tena. Kama Watanzania tunapaswa kujituma, kuteseka, kutimiza ndoto za Rais wetu, Hayati John Pombe Magufuli, ambaye ametangulia mbele za haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufikiria kwa dakika moja, wakati Mheshimiwa anatuacha alikuwa anafikiria nini akilini mwake. Najua alikuwa anafikiria angetamani kuona Daraja la Busisi magari yanapita, angetamani kuona treni inapita pale TAZARA, treni inaenda kwa kasi kwenda Morogoro, hayo yote hayakutokea. Mahali fulani naamini ya kwamba, alikuwa ana disappointment kwa sababu ameondoka mapema. Kazi yetu sisi tuliobaki ni kumpa furaha Rais wetu, ni kumpa furaha Hayati Magufuli huko aliko kwa kuyatimiza haya mambo aliyokuwa ameyaanzisha, na inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, azimio la pili ni la Mheshimiwa Rais Suluhu Hassan ambaye, kwa kweli nataka nikuhakikishie moyoni mwangu sina hofu hata kidogo wala sina wasiwasi. Matumaini yangu ni makubwa sana leo kwa sababu naamini uwezo wa mwanamke. Wanawake wana uwezo mkubwa sana, wanaume naomba tukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanasayansi walifanya utafiti katika Chuo Kikuu cha Havard wakagundua ya kwamba, mwanamke ana-emotional intelligence kubwa kuliko mwanaume, na ndiyo maana anaweza kufanya kazi tano kwa wakati mmoja, mwanaume ukipewa kazi moja unateseka. Kama hiyo ni kweli nina uhakika nchi yangu iko katika mikono salama, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan atalivusha Taifa hili mpaka kwenye uchumi wa juu kabisa badala ya uchumi wa kati. Tumempata na Makamu wa Rais mtaratibu, mnyenyekevu, wote hapa tumetoa kura asilimia 100. Huyu mtu atamsaidia Rais wetu kutumiza ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisiongee mambo mengi. Nataka niwaombe wote pamoja tumuunge mkono Rais wetu kuipeleka nchi yetu mahali inapotakiwa kwenda. Ahsanteni kwa kunisikiliza, naunga mkono hoja. (Makofi)