Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuunga mkono maazimio mawili. Moja, la kumuenzi Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na la pili la kumpongeza Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nichukue fursa hii kuwapa pole Watanzania wote kwa msiba uliotufika. Pia nichukue fursa hii kuwashukuru wote ambao walichukua jitihada za ziada kuwasiliana nami kunipa pole kwa kuondokewa na kiongozi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kumuenzi, mtu mwema anapofariki na muungwana akaamua kumuenzi Marehemu, njia nzuri ya kumuenzi marehemu ni kutenda yale mema ambayo yeye alipendezwa nayo. Si mara moja au mara mbili; hasa Bunge lililopita nilimsikia, siyo mimi peke yangu Hayati Dkt. Magufuli akisema nawashukuru sana Wabunge kwa kuniunga mkono nikaweza kutekeleza yale niliyoyatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge tuna deni. Kama alitushukuru kwa kumuunga mkono sasa tutekeleze kama tulivyotekeleza kwake kwa huyu ambaye amekuwa mrithi wake. Tumuunge mkono Rais mama Samia kama tulivyomuunga mkono Hayati Magufuli. Hili sizungumzi na Wabunge tu, nazungumza na watendaji wa Serikali, nazungumza na wananchi wote Tanzania nzima, Mkoa mzima wa Kagera bila kusahau jimbo langu kwamba yale tuliyotenda kwa miaka mitano dunia ikatushangaa basi kwa kumuenzi na tutende maradufu tunapokwenda kufika mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aliyeondoka ni rubani mkuu lakini rubani mkuu alipokuwa anga za juu katika mwendo wa mbali alikuwa na rubani mkuu msaidizi. Kumbe hawa wote tulikuwa nao safarini na sisi abiria tulishajua tunakwenda wapi, tulishajua dira. Mwenyezi Mungu akaamua rubani mkuu akaishiwa pumzi, bila mtikisiko rubani mkuu msaidizi bila kuyumba akaendesha chombo na wakati muafaka akatuambia kwamba rubani mkuu hatunaye lakini hatukutetereka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapompongeza Mheshimiwa Rais, nampongeza kwa hilo. Watu waliyumba, watu walitetereka lakini rubani mkuu msaidizi akakaa kwenye usukani akaelekeza chombo kule kule. Tunakokwenda Watanzania tunakujua, tunakwenda katika ujenzi wa Taifa imara, siyo uchumi wa juu, Taifa imara, Taifa lililoendelea na uzuri wa bahati, mwenye bahati habahatishi. Kumbe dira ya Taifa mwaka 2010 aliyekaa kupanga mipango mitatu ya miaka mitano mitano ni Dkt. Phillip Isdor Mpango. Sasa yeye anakwenda kuwa rubani mkuu msaidizi chombo kinakwenda kwa kasi ile ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri ukauliza watu wanakuonaje. Watu wanapanga matabaka, huu ni uchumi wa chini, huu ni uchumi wa juu; Dkt. Mwigulu Nchemba alisema Tanzania haikwenda kuomba ili iwe uchumi wa kati, haikuomba Tanzania, walikaa huko wakapanga. Ukitaka kujua demokrasia ya Tanzania ni tabaka gani, waulize Waganda, waulize Wakenya, watakwambia sisi ni demokrasia ya daraja la juu, la kati au lipi. Waheshimiwa Wabunge, kipekee niwaombe tunalo deni kubwa, wale nilioweza kuwaandikia niliwaandikia, Mheshimiwa Spika ni shahidi, tunachopaswa kufanya sisi Wabunge ambao ni viongozi wakubwa, wataalam wa mikakati wanasema ni ku- hold yaani tushikilie haya mafanikio.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo katika kujenga maendeleo ya nchi hii kwa miaka mingi iliyopita tulikuwa tunajifunza au tunapambana, sasa yale mafanikio ambayo tumeyapata katika kipindi cha Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tuyahodhi. Tumefanya vizuri katika ujenzi wa shule, tuhodhi. Tunapaswa kuongeza ubora wa watoto mashuleni, tuhodhi twende mbele. Tumeweza kudhibiti ukwepaji wa kodi, tuhodhi. Tumeweza kufanya vizuri, tuhodhi na yote aliyoyasema Makamu wa Rais mtarajiwa, tuhodhi na yote haya yamefanyika kwa mafanikio na kwa ushirikiano wa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono na napongeza yote yaliyoletwa mbele yetu. (Makofi)