Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia maazimio yaliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na Watanzania wote nami kutoa masikitiko yangu makubwa kwa kuondokewa na Kiongozi wetu. Pia niungane na wenzangu waliotangulia kusema kwamba Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Hatuna jinsi zaidi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Leo Mheshimiwa Dkt. Mpango amesema ni lazima Taifa liendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa demokrasia ile ile iliyopo kwenye nchi ya Tanzania ambayo wenzetu wengine hawaioni, tumeweza kufuata Katiba na kumchukua Makamu wa Rais na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napata shida sana kusikia mtu anasema Serikali iliyopita ilikuwa haina demokrasia. Nasema demokrasia ipo na ndiyo maana baadhi ya Wabunge wenzetu vyama vyao viliwakataa, lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikasema ni haki yao kuwa Wabunge. Walikuja hapa wakaapishwa wakati hakuna Bunge. Kwa hiyo, naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, lakini tuko na tunaipongeza na kuiombea kila la heri Serikali yetu ya Mama yetu, Rais wetu, Mama Samia Suluhu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilianza kumfahamu Mheshimiwa Rais wetu wa sasa wakati wa Bunge la Katiba, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Mama huyu alikuwa Mwenyekiti mahiri. Nakumbuka Mzee Samuel Sitta alikuwa ana-deal sana na mambo ya kiutawala. Mama alikaa kwenye mijadala mizito, aliweza kuiamua, Bunge la Katiba lilikuwa liko hot, lakini mama alienda nalo vizuri na hatimaye tulivuka tukamaliza Bunge la Katiba salama salimini. Nina hakika na ninayo kila sababu ya kuwaambia Watanzania, tutaenda kuvuka na kazi itaenda kupigwa na tutafikia malengo yaliyowekwa katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina imani sana na Mheshimiwa Rais. Mfano juzi au jana wakati anapokea taarifa ya CAG, maamuzi aliyoyachukua, Watanzania wamempokea kwa mikono miwili. Wameona tuko kule kule kwa mzalendo, ana uchungu na fedha za Watanzania, ana uchungu na wezi na anachukua hatua kama alivyokuwa anachukua mtangulizi wake. Sipati shida kusema Mheshimiwa Mama Samia na Marehemu Rais wetu walikuwa ni Kurwa na Doto, walikuwa wanafanya kazi zao kwa pamoja. Kwa hiyo, niwaambie Watanzania, wawe na imani kubwa kwamba tunakwenda kutekeleza mambo yote tuliyoyaahidi kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia mwenzetu mmoja hapa anaongea kwamba Mheshimiwa Rais ahakikishe Katiba mpya inapatikana. Niwaambie tu, wakati Mheshimiwa Rais aliyepo sasa hivi madarakani na aliyekuwa amefariki, walitembea Tanzania nzima kuomba kura kwa Watanzania wakiahidi maendeleo, zahanati, maji, shule, elimu bure na kadhalika. Hawakuweza kuwaahidi Katiba mpya. Msitake kumtoa Rais wetu kwenye reli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia kwenye mitandao, kuna raia mmoja wa Ubelgiji alianza kuandika kwamba tunataka Katiba mpya kwa Rais mpya. Mimi nimweleze tu, hawawezi wao kutupangia, tutajipangia wenyewe na tutakwenda kama tulivyojipangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nimwambie Mheshimiwa Rais, aliwaahidi Watanzania maendeleo, tunataka achape kazi alete maendeleo ili mwaka 2025 tutoke kifua mbele kwenda kuomba kura na hatimaye CCM iibuke kidedea kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na Wabunge wenzangu kusema kwamba Mungu anaipenda Tanzania. Tendo la leo lililotokea la kumchagua Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mpango, niseme Mungu anaipenda Tanzania. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Amina.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, tumekwenda kupata Makamu wa Rais mchapakazi atakayemsaidia Rais wetu kufanya kazi, mzalendo anayechukia rushwa, amekaa Wizara ya Fedha. Nani ambaye hajui Wizara ya Fedha? Leo angekuwa amejilimbikizia mali za kila aina, lakini siyo Mheshimiwa Dkt. Mpango. Ni mchumi aliyebobea. Tuna imani tutakwenda kupandisha uchumi wetu Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)