Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii angalau kutoa ufafanuzi wa hoja za Waheshimiwa Wabunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano, kwa maana ya 2021/2022 – 2025/2026 pamoja na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wakati wanachangia waligusia mambo mengi sana ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI. Nami kwa niaba ya Waziri, Mheshimiwa Suleiman Jafo, naomba nitoe baadhi ya ufafanuzi katika mambo ambayo tumeyasikia na tunaendelea kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo Waheshimiwa Wabunge walizungumzia ni mapendekezo ya kuiongezea fedha TARURA ili waweze kujiwezesha kujenga hizi barabara za vijijini. Kwa hiyo, kitu kikubwa ambacho Waheshimiwa Wabunge wanapaswa kufahamu, ni kwamba Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa kushirikiana na TARURA pamoja na TANROAD, imeandaa andiko linalopendekeza upya kupitia chanzo hiki cha mafuta ili tuone kama kinaweza kikasaidia. Pendekezo hili tunakwenda kuliwasilisha Serikalini kwa hatua zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Serikali inaendelea kupitia formula wa mgao wa fedha chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kupitia Bodi yake ya Mfuko wa Barabara. Kwa hiyo, hili tuliona tulizungumze kwa sababu ni Wabunge wengi walikuwa na nia njema kutaka kuona kuna ongezeko la mapato kwenye Mfuko wa TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la lingine ni kwamba watu wa TARURA hawawajibiki katika Halmashauri kwa maana ya Madiwani. Nieleze tu kwamba, Mwongozo wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini, unaelekeza vizuri kabisa kwamba Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambao ulitolewa na Katibu Mkuu mwaka 2018, inaitaka TARURA kufanya kazi moja kwa moja na Serikali za Mitaa. Pia Mheshimiwa Waziri alishalitolewa mwongozo kwamba miradi mingi inapaswa kuibuliwa na Madiwani ambapo watashirikiana na TARURA ili kuitengenezea bajeti na hivyo iwe inatekelezeka. Kwa hiyo, bado msimamo wa Serikali uko pale pale kwamba TARURA itaendelea kufanya kazi na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, lilikuwa ni kuimarisha miundombinu. Hili tumelipokea, nafikiri litakuwa affected zaidi baada ya yale mapendekezo ya awali ya ongezeko la mapato ambayo tunayapeleka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya nne, Waheshimiwa Wabunge walielezea kuhusu uendelezaji wa Mradi wa Jiji la Dar es Salaam kwa maana ya DMDP. Kwa kifupi tu ni kwamba Serikali inaendelea kukamilisha utaratibu kwa ajili ya uendelezaji wa mradi huu na kwa awamu ya pili tunatarajia huu mradi wa DMDP utatumia dola za Kimarekani milioni 120.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la afya, Waheshimiwa Wabunge walipongeza jitihada kubwa ambayo imefanyika katika ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali katika ngazi za Wilaya na wakataka kuhakikisha kwamba Serikali inamaliza miradi yake kama ambavyo ilikuwa imepangwa hususan yale maboma ambayo yameibuliwa na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu kwa kifupi kwamba kwa mwaka 2021, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 27.5 kuhakikisha kwamba tunakamilisha maboma 555 ya zahanati zote nchini. Kwa hiyo, tumeamua tuliseme. Tumetenga shilingi bilioni 33.5 kuhakikisha tunanunua vifaa tiba katika hospitali 67 za halmashauri ambazo zilikuwa zimejengwa katika mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu, Waheshimiwa Wabunge walieleza kwamba pamoja na jitihada nzuri ambazo Serikali imezifanya kwenye kujenga miundombinu mizuri, lakini walikuwa wanataka ihakikishe kwamba inaongeza idadi kubwa ya Walimu katika shule zetu. Sasa katika kukidhi jambo hilo, tueleze tu kwamba Serikali itaendelea kuajiri Walimu kama ambavyo tumefanya mwaka 2020, tulitangaza ajira 13,000; ajira 8,000 tayari zilikuwa zimeshatolewa na 5,000 ziko katika hatua ya mwisho. Vile vile ni kwamba tutaendelea kufanya hivyo, kulingana na mahitaji kama ambavyo tumeyaainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Waheshimiwa Wabunge walikuwa wamezungumzia ushirikishaji wa wananchi kwenye shughuli za kiuchumi. Sasa hili tumeliainisha vizuri kabisa kwamba kwa kushirikiana na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, tumeandaa Mkakati wa Miaka Mitano, kwa maana ya 2017 mpaka 2025 kuhakikisha kwamba tunawa-accommodate wananchi wote. Ndiyo maana unaona Serikali imeanzisha utaratibu wa kutumia force account ku-accommodate wananchi wa kawaida kushiriki katika uchumi wa nchi yao.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni miradi ya maendeleo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Silinde, kengele imegonga. Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)