Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa afya njema siku ya leo na kupata nafasi katika Bunge lako Tukufu. Pia nitoe pole katika familia ya mwenzetu Mheshimiwa Nditiye kwa msiba ambao umetukumba. Nasi sote ni njia yetu, zaidi sana ni kuombeana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba nijibu hoja kadhaa za Wabunge ambazo wamezitoa wakati wanachangia Mpango na zaidi ya Wabunge 25 walichangia katika Wizara yetu. Sisi tumepokea kama Wizara, maoni ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wameyatoa kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa uvuvi, kwa sababu muda ni mchache, niende moja kwa moja; nitakuwa nakwenda kwa hoja zile ambazo zimesemwa kwa ujumla wake; lakini zile ambazo pia zinahitaji majibu, Wizara yetu iko tayari kujibu kwa maandishi na kuwapatia Waheshimiwa Wabunge pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kubwa kwa upande wa uvuvi ilikuwa ni kuboresha uvuvi wa bahari kuu. Katika Mpango huu, Serikali imejipanga; tunafahamu kwamba tuna Mpango wa Miaka Mitano na Mpango wa Mwaka Mmoja. Wizara yetu imebahatika katika Mpango huu wa Mwaka Mmoja kuingiza mambo kadhaa ambayo yakienda kuanza sasa yatakwenda kuboresha uvuvi wa bahari kuu. Jambo la kwanza ni suala la ujenzi wa bandari kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe, Serikali ilishaanza upembuzi yakinifu kuangalia maeneo mbalimbali ambayo Bandari ya Uvuvi itajengwa. Pia Serikali ikishirikiana na wenzetu wa Italia wameshaanza na zaidi ya Shilingi za Kitanzania bilioni 1.4 zilitengwa na shilingi milioni 700 zilishalipwa kwa kampuni hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upembuzi yakinifu, eneo la bandari ambalo sasa Serikali tunaenda nalo ni eneo la Bagamoyo pale Mbegani. Kazi hii inaendelea. Muda wowote upembuzi yakinifu ukikamilika sasa tunaenda kuwa na actual design ya bandari hii na kazi hii ianze ili tunapoenda kwenye uvuvi wa bahari kuu, bandari iwe imeshaanza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi walichangia ni suala la ununuzi wa meli, kwamba tunapokwenda sasa kwenye uvuvi wa bahari kuu Serikali ihakikishe kwamba tunajipanga kununua meli zetu. Bahati nzuri wenzetu wa IFAD katika Mfuko ule wa Maendeleo wa Kilimo pamoja na Mifugo na Uvuvi wameshatukubalia kwamba watatupatia fedha kwa ajili ya ununuzi wa meli hizo na meli hizi nane; nne zitakuwa upande wa Zanzibar na nne zitakuwa upande wa Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Zanzibar wameshatoa vigezo, wanahitaji meli za namna gani, nasi Bara tayari tunafahamu ni meli za namna gani, kwa vipimo vipi. Pia wenzetu hawa watatupatia Dola za Kimarekani milioni 58 ambazo sasa sisi Uvuvi tutakuwa na gawio letu hapo kwa ajili ya ununuzi wa hizi meli. Kwa hiyo, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba kazi hii inaanza sambamba ikiendelea na upande wa ujenzi wa bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kazi hii itakapoanza, pande zote mbili za nchi yetu watashirikishwa. Pia usimamizi huu utaendelea kufanyika na mamlaka ya uvuvi wa bahari kuu ambayo sasa inaendelea na kanuni zake tumeshazitunga, tunasubiri Mawaziri wa pande zote mbili waweze kusaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa jumla kuhusu uvuvi, kulikuwa na tatizo la tozo. Kwamba wavuvi wetu wengi wanahangaika na tozo, lakini maeneo mengine inawezekana hawatendewi haki. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kuhusu suala la kanuni zetu ambazo tumezitunga za mwaka 2020 ambapo maeneo mengi zimekwenda kugusa wavuvi na zimesababisha sintofahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijulishe Bunge lako Tukufu kwamba Wizara hii ni sikivu; Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara, tumeangalia kwa upya kanuni hizo, lakini pia yale maeneo ambayo yalikuwa yanasumbua wavuvi, mfano uvuvi wa ring net katika bahari kuu, tumeyafanyia kazi nanyi mmeona. Kwa upande wa Tanganyika, suala la wavu wa dagaa, tumefanyia kazi na tuliwashirikisha pia. Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha taratibu masuala ya uvuvi na tutawashirikisha Waheshimiwa Wabunge; na baada ya Bunge pia tutafika kwenye maeneo yenu ili pasiwepo na matatizo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwa upande wa mifugo. Kwa upande wa mifugo, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia kwa upana wake, suala la Serikali kuwekeza katika mifugo. Tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge katika maoni yao tuliyoyapokea wamehitaji Serikali iwekeze katika ujenzi wa miundombinu ya mifugo kote nchini. Sisi kama Serikali, tumejipanga, kwa kuanzia tu, tumeita kikao cha wadau wote ambao wanajihusisha na uzalishaji na uchakataji wa nyama. Tuna viwanda kama tisa katika nchi yetu. Nafahamu kwamba hoja kubwa ni kuangalia hizi tozo ambazo zinasababisha viwanda vyetu vinashindwa ku- perform waki-compete na nchi za wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeshapitia hizo tozo na katika Bunge lijalo la Bajeti, tutapendekeza mabadiliko mbalimbali ili kuhakikisha mifugo yetu inachakatwa ndani ya nchi. Haturidhishwi ng’ombe, mbuzi na kondoo kutoroshwa. Mwaka 2019/2020 tulikuwa na ng’ombe milioni 1.4 wanatoroshwa au wanasafirishwa wakiwa wazima kwenye nchi za wenzetu, halafu wao wanachakata, wanauza hizo nyama wakati ng’ombe wametoka kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi tozo tutazipitia kwa upya tuone kiasi gani tunaweza kuzirekebisha ili viwanda vyetu vya ndani viweze kufanya kazi sawa na viwanda vya nchi za wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwa upande wa mifugo ni suala la kuongeza malisho. Wizara katika kuhakikisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.