Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah-wataala aliyenipa uwezo na afya njema leo hii nikaweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani zangu za dhati ziende kwa Chama changu cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuridhia kwamba mimi Asha ambaye najulikana zaidi kama Mshua kuwa Mbunge wa Jimbo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Mjini Zanzibar kwa imani waliyonionyesha. Niwahakikishie mbele yako kwamba sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya iliyopelekea kupata ushindi wa kishindo wa uchaguzi uliopita. Hiyo ni kuonyesha kwamba utekelezaji ulikuwa wa kuridhisha katika awamu aliyohudumu. Ni matumaini yangu pia huko mbele tunakokwenda mambo yatakuwa mazuri zaidi kwa sababu yale mambo yetu muhimu; Standard Gauge, Stiegler’s Gorge na mengineyo yote yatakuwa in full operation. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. John Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nachukua nafasi hii adhimu sana kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuwa Rais wa Zanzibar na kuweza kuhudumu kwa style yake ya umahiri, umakini na uhodari na kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unapaa na neema tele kwa Wazanzibar. Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Mwinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia habari ya Mpango. Nimeusoma na nimeuelewa na watu wengi wameuchangia. Kwa kweli Mpango umepangika, hongera sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na timu nzima mlioandaa Mpango huu. Kwa ujumla wake mipango ya humu inaleta matumaini kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia sekta ya afya na hasa Mpango wa Bima kwa Watanzania wote. Taarifa ya Serikali ilionesha kwamba asilimia 33 tu ya Watanzania wanashiriki fursa za Bima ya Afya. Hadi kufikia 2019, Watanzania walionufaika na huduma hiyo ilikuwa 13,029,636 sawa na asilimia 25 ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iharakishe mchakato wa kuhakikisha kwamba Mfuko wa Bima kwa Watanzania wote unakuwa tayari na mchakato huo wa sheria ukamilike mapema iwezekanavyo. Hii itasaidia kuwa na mfuko mmoja wa Bima ya Afya ili kuwezesha Watanzania wengi kufaidika na huduma hiyo kwani wakiwa na afya njema, watachangia katika shughuli za maendeleo kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya pili ambayo nataka kuizungumzia ni hii ya Hifadhi ya Jamii. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria. Nimejengewa uelewa juu ya Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii inayochangia uchumi kwa kiasi kikubwa. Mifuko hii inachangia uchumi wa viwanda na nachukua nafasi hii kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa utaratibu wa Mifuko yetu NSSF, PSSSF na WSF. Nakupongeza sana Mheshimiwa Jenista, wewe na Kamanda wako Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa, mmejipanga kweli kweli kuchangia maendeleo na ustawi wa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu, tuongeze ubunifu wa maeneo ya uwekezaji kama vile viwanda vya kilimo vyenye uhakika wa soko, pamoja na kupanua huduma zake kwa Watanzania walio kwenye sekta isiyo rasmi kama vile wakulima, vikundi mbalimbali vya kijamii ambapo huko ndiko kuna Watanzania wengi Zaidi. Tukifanikiwa kuchangia mapato basi mifuko yetu hii itazidi kunona na Watanzania wetu watanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo, ahsante sana, nyote nawapongeza. (Makofi)