Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza, naomba nianze kupongeza Serikali kwa kuleta Mpango huu mzuri, pamoja na mipango mingine yote iliyotangulia tuliona kwamba ina nia ya kuhakikisha tunafikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 sanjari na kukuza malengo endelevu ya SDGs. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu umekuwa na nguzo muhimu tatu, ikiwa ni utawala bora, maendeleo ya watu pamoja na kukuza uchumi. Kukuza uchumi ni kuwekeza katika sekta za kiuchumi na kiuzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa muda mrefu imeendelea kuingia katika mikataba na makubaliano mbalimbali aidha kupitia wahisani, mikopo, uwekezaji ambalo ni jambo jema sana, lakini tumeona mara nyingi Mheshimiwa Rais amekuwa akihoji, ndugu zangu hivi kweli huu uwekezaji una tija? Hivi hii miradi ina tija? Tija ni nini basi? Tija ni uwiano kati ya kitu unachowekeza na kile kinachopatikana, lakini kikionyesha mabadliko chanya katika mtu mmoja mmoja, katika taasisi na nchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tija ni nini ili kama mwekezaji anaweka mradi wake au analeta msaada wake au anaweka kampuni yake, mwisho wa siku anapoondoka aache ajira endelevu, aache ujuzi, akuze ujuzi kwa wale ambao wanahusika na pia kubwa kabisa waache teknolojia pamoja na ubunifu. Yaani mradi unapokwisha asiondoke yeye na vitu vyake akaacha vitu vitupu. Kwa mfano katika kuwekeza 100% kwa maana ya consultancy anaanzisha mradi yeye 100% mgeni anakuwepo pale pengine engineer wetu au mtaalam wetu anashuhudia tu msumari unavyopondwa pondwa kwenye shirika hilo au kwenye kampuni au mradi au mashine inavyofungwa, lakini ule ujuzi hashiriki moja kwa moja, anapoondoka anaondoka na ujuzi wake mwekezaji. Kwa hiyo ifikie sehemu, nashauri Serikali hii miradi safari hii, tunaona watu wengi wanalalamikia miradi ya maji, miradi mbalimbali ambayo tumeingia lakini kama nilivyofafanua nini maana ya tija. Je miradi hii inaacha tija kweli? Kwa nini? Sasa ifikie sehemu tutumie chombo kile kinaitwa chombo cha kukuza tija na ubunifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani liliitwa Shirika la Tija la Taifa, chombo hiki kipo na kipo vizuri chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu chombo hiki sasa kipewe meno kipewe uwezo ili kuondoa haya malalamiko yote ambayo yako kwenye miradi ambayo ina mambo mengi ambayo ni baadhi lakini kwa kweli ni mingi, miradi ambayo imekuwa ina-fail. Chombo hiki kabla miradi au mikataba haijaanza kutekelezwa, chombo kikaangalie kikapime hii miradi itakuwa na tija kama nilivyoeleza maana ya tija ili baadaye kusiwepo na malalamiko. Huu ni wakati wa kukipa chombo hiki meno na uwezo maana tunacho, tunacho kwenye Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia viwanda tulivyopata ni vingi sana kwenye nchi sasa hivi. Kweli ni vingi na ni vizuri, ni jambo jema, lakini chombo hiki bado kina uwezo wa kwenda kutathmini vile viwanda, kufanya analysis na kutoa ushauri ili mwisho wa siku viwanda visiwe vya kupotea, viwe vina-sustain vinakaa muda mrefu yaani vinaendeleza kuwa na tija, maana yake havikufanyiwa huu upekuzi mwanzo ndiyo maana tunaona kuna malalamiko mengi, kwenye viwanda hatujui itakuwaje baadaye na miradi imeshaonyesha jinsi ilivyokuwa kwenye Mipango iliyopita. Kwa hiyo, nashauri chombo hiki kitumike ili kilete tija katika miradi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nitoe mfano, wenzetu China wakati wanaandaa Olympic 2008 walikuwa wametoa nafasi kwa wawekezaji, lile ni jambo kubwa lilihitaji watu wawekeze kwa wingi, lakini walikuwa wakali, wakasema unakuja kuwekeza ndiyo, lakini kuanzia mwanzo wa mchakato wa kutaka kuwekeza, kama ni kujenga uwanja wewe mwekezaji utafanya kazi kwa asilimia 70 na sisi wazawa consultancy mzawa atafanya 70 ili pale wanapomaliza watapata faida ya 70% yes lakini 30% kutoka anapowekeza anajenga kiwanda au anajenga uwanja ile pesa inabaki ndani inazunguka kwa sababu yule mwekezaji wa ndani (consultancy) alikuwepo toka mwanzoni. Kwa hiyo inabidi kuangalia mfano wa wenzetu, wameendelea lakini wako makini sana na mali yao na mzunguko wa pesa yao ndani mwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwenye suala la afya, na-declare interest, suala zima la kada ya physiotherapy. Naipongeza Serikali sana imefanya bidii nyingi lakini taaluma hii ambayo ni matibabu kwa njia mbalimbali ikiwemo mazoezi tiba, wataalam ni wachache, wenye shahada hawazidi 100 kwenye nchi nzima, lakini pia chuo ambacho kinatoa shahada hii ya physiotherapy Kiswahili chake matibabu ya njia mbalimbali ambayo pia ni mazoezi tiba, ni KCMC peke yake. Niipongeze Wizara ya Afya sasa ina mpango wa kuanzisha hii kozi kwenye Chuo cha Muhimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado haitoshi, naomba niishauri Serikali ifanye uanzishaji wa kozi hii kwenye Chuo cha UDOM na Bugando. Hawa watu wanahitajika sana kwa sababu tunafungua hospitali nyingi za mikoa kwa bidii na pia hospitali za wilaya, pamoja na vituo vya afya. Pia nashauri kwa sasa kwenye vituo vya afya na hospitali za wilaya, hivi vitengo viwekwe, havipo, tufikirie viwekwe na wataalam waongezeke, wapelekwe kule kwa sababu ni idara muhimu sana, lakini ina watu wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia pawepo na wazo la kuongeza Shahada ya Uzamili na Uzamivu ikiwezekana ya kada hii ya physiotherapy hatuna kwenye nchi yetu. Ili upate Shahada ya Uzamivu lazima uende nje ya nchi. Kwa hiyo nilikuwa nashauri hili jambo litekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)