Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kupata nafasi ya kuchangia Mpango huu wa Tatu tunaouendea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mpango unaandaliwa kulikuwa kuna malengo hasa waliyafikia. Kwanza kulikuwa na mambo kama manne kwa sababu ya muda nitayataja, viwango vya juu vya maendeleo ya viwanda lakini pia ushindani, maisha bora na utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uweze kutimiza haya malengo kulikuwa kuna viashiria, kwa mfano, walisema kuwekeza kimkakati katika viwanda vya nguo za pamba pamoja na mazao ya mbogamboga. Leo hii katika nchi hii ya Tanzania na hasa nikizungumzia Nyanda za Juu Kusini, wanalima mazao ya mboga mboga, wanalima mazao ya biashara lakini hatuna soko la uhakika. Ndugu zangu hapa wamezungumzia Maafisa Ugani. Leo hii ukienda Mkoa wa Mbeya, utakuta wakulima wanalima kutokana na wanavyosikia kwenye mikeka au kwenye vikao vya chini wanavyokaa na wala sio kwa utaalam. Leo wanakwambia zao la chai ni zao ambalo linauzika duniani na hatujawahi kusikia chai imeshuka katika soko la dunia, lakini hakuna Afisa Kilimo anayekwenda kuwasaidia wakulima wa chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo chai inauzwa Sh.200 kwa kilo wilaya ya Rungwe, lakini ukienda Njombe chai inauzwa Sh.500 kwa kilo. Ukienda Lushoto, chai ni Sh.500 kwa kilo. Ni nchi moja, Serikali moja, bei tofauti. Tumelilalamikia hilo na tunaendelea kuuliza kwa nini tuna Bodi ya Chai inayofanana bei zinaenda tofauti, uchumi unakua hauendi sawa, watu wa Mbeya wanapata kidogo, watu wa Lushoto wanapata zaidi. Tunaomba Serikali na hasa Wizara ya Kilimo isimamie suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna mazao ya vanilla. Mkulima anaamua kulima vanilla kwa sababu jirani yake kalima vanilla. Anaambiwa kilo moja ni 400,000 sasa tunataka Maafisa Kilimo waende wawaambie wananchi kama ni kweli hiyo bei iko kwenye soko badala ya watu kuambiana na kuwa na vikundi vya kuambiana zao hili linalipa, lakini mwisho wa siku akilima vanilla kwa miaka miwili anakuta soko Sh.50,000 na ametumia gharama kubwa. Tunaomba Wizara ya Kilimo isimamie suala hilo lisaidie wananchi wasifanye kilimo cha makundi au kusikia kwenye redio mbao, ifuate mfumo wa Serikali kwa kupitia Maafisa wetu wa Kilimo kwenye halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia biashara ya ushindani, leo hii tuna Bandari ya Dar es Salaam, ni bandari ambayo Mungu ametupa wala hatujaitengeneza, ipo. Leo Bandari ya Dar es Salaam kama tusipofanya kwa umakini kama wananchi wa Tanzania Beira inachukua wateja wetu wote wanapeleka Bandari ya Beira, watapeleka Bandari ya Afrika Kusini. Hivyo tunaomba viongozi wetu ambao wamesomea mambo ya marketing wajitahidi kusimamia biashara yetu ili Bandari yetu ya Dar es Salaam iendelee kupata wateja na wateja wasitukimbie kwa sababu ya vile viwango vinavyowekwa. Mtu akienda Beira anapewa labda siku 21 ndipo anaanza kulipia mzigo wake. Ukija kwetu mnawapa siku 14. Ni lazima tuwe wajanja na kufikiria kwamba wanaotuzunguka Mombasa na wengine hawapendi maendeleo ya Tanzania, hivyo basi viongozi wajifikirie kujiongeza, wahakikishe wale wateja ambao walikuwa wanapitia bandari yetu, hatuwapotezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda, huwezi kuzungumzia viwanda ukaacha kilimo. Leo hii tunahitaji kupata malighafi kutoka kwenye kilimo ili viwanda vyetu viweze kupata malighafi hapa hapa nchini. Naomba sana tuhakikishe kwamba kilimo hasa mbolea na pembejeo zinafika kwa wakati kwa wakulima. Nilizungumza hata hotuba iliyopita, bila utafiti hatuwezi kufanikiwa, tuwekeze kwenye utafiti. Nilisema last time kwamba tuna Chuo cha Uyole ambao wao ni wenzetu wamesomea mambo hayo, tuna SUA na asubuhi umezungumza hawa watu wa SUA wajikite kwenye utafiti ili kusaidia watu wetu na kilimo chetu tupate mazao ya kutosha ili yaweze kusaidia kwenye viwanda na tuweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utalii; leo hii tuna majirani zetu wa Kenya, sisi tuna vitu vingi sana vya utalii lakini kuvitangaza tumeweka bajeti ndogo sana. Leo hii mikoa mingi sana ina vivutio lakini Kaskazini ndiyo inaonekana ina vivutio vingi kwa sababu Serikali imewekeza huko zaidi. Kuna vivutio vingine ni vidogo. Ukienda sehemu za Njombe unakutana na bustani ya Mungu, unakutana na maua mazuri, tujitahidi kueleza watalii wetu kwamba hata huko pia wanaweza wakaja na uchumi ukaongezeka. Tuna daraja la Mungu sisi kwetu Rungwe, je, watu wetu wanafikaje? Ukienda kwenye daraja la Mungu miundombinu kufikia ni kilometa tano kutoka barabara kuu lakini mpaka ufike barabara ilijengwa na Mjerumani mpaka leo hakufikiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango vya kutoza watalii. Nimerudia mwanzo nimesema viongozi wetu na wataalam waende hata kwa upelelezi wajue Kenya wanafanyaje na nchi zingine wanafanyaje na sisi tuone kama tunapunguza au tunaongeza kwa faida ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ulisema uchumi utakua mpaka asilimia 10, ule ulikuwa ni Mpango, lakini mpaka sasa bado hatujafikia, tunahitaji kukaa na kujipima ni wapi tumekosea, ni wapi tuongeze nguvu ili tuweze kuhakikisha tunasonga mbele kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi sana ambayo sisi kama Taifa tunafikiri tukisimamia tunaweza tukasonga mbele. Tunazungumzia maisha bora, ili Mtanzania wa kawaida asilalamike kusema mnasema uchumi umekua, mfuko wangu hauna pesa, ni lazima mzunguko wa fedha uachiliwe kwa wananchi. Unapomlipa mkandarasi kwa wakati, mamantilie atawauzia wale wafanyakazi kwenye barabara, mamantilie yeye akishauza chakula atalipa ada ya mtoto, pesa zitakuwa mfukoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kulipa madeni kwenye Halmashauri zetu, tunahitaji kuwekeza zaidi kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia utawala bora msipokuwa na amani, nakumbuka kuna Waziri mmoja alijibu hapa akasema utawala bora hapa pana amani. Sote tunafahamu unapozungumzia amani lazima uzungumzie na haki. Tulikuwa na uchaguzi uliopita, uchaguzi uligubikwa na mambo yasiyokwenda sawa kuanzia kwenye wakati wa kujiandikisha, wakati wa kutangazwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sophia, naona kengele kama vile.

Unasikia, imeshaita tayari. (Kicheko)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)