Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika hoja iliyoko mbele yetu kuhusiana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni kama desturi au taratibu zinatutaka tupitishe Mipango hii na mara nyingi imekuwa ni Mipango mizuri sana kwenye maandishi na imekuwa ni Mipango mingi kwa mara moja lakini ukija kwenye utekelezaji ndipo ambapo kunakuwa na changamoto kubwa. Utekelezaji umekuwa ni hafifu kwa sababu kwanza tumekuwa na mipango mingi ndani ya mwaka mmoja wakati tunaambiwa hako kasungura tunakokakusanya nako ni kadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bora tuwe na Mipango michache ambayo inahusiana moja kwa moja na maisha ya mwananchi wa kawaida, tukaitekeleza kwa ufanisi, tukamsaidia yule mwananchi wa chini kabisa maskini. Tukipitisha mipango tukaenda kupitisha na bajeti maana yake fedha zitolewe na bajeti hiyo iweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, tunapitisha mipango mbalimbali kwenye sekta zote muhimu zinazomgusa Mtanzania mfano ya kilimo, maji, viwanda, afya, yote kwa namna moja au nyingine inamgusa mtanania wa chini kabisa. Hata hivyo, tukipitisha Mipango hii ukija kwenye kuangalia namna gani bajeti zinapitishwa kwenye Wizara hizi haiendani kabisa na kile ambacho tumekipitisha. Fedha hazitolewi kwa wakati, wakati mwingine hata kikitolewa hicho kidogo kinafika kwa kuchelewa maana yake kile tulichokipitisha basi kinakuwa ni kama hakuna kwa sababu hakuna matokeo ambayo yanafikiwa kulingana na kile ambacho tumekipitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la mfumuko wa bei, ukisoma Mpango hapa unaeleza kabisa kwamba mfumuko wa bei Serikali imeendelea kudhibiti. Uhalisia sidhani kama iko hivyo, inawezekana imedhibitiwa kwenye makaratasi lakini tukitoka nje ya jengo hili huo mfumuko wa bei unaosemwa haujadhibitiwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Desemba mwaka jana mpaka leo hii January tunapoongea kuna mfumuko mkubwa sana wa bei ya bidhaa. Mfano, unga wa ngano wa kilo 50 ilikuwa inanunuliwa kwa Sh.60,000 leo unanunuliwa kwa shilingi 69,000. Unaenda kwenye mafuta ya kula ya lita 20, yalikuwa yananunuliwa kwa shilingi 52,000 leo yananunuliwa kwa shilingi 82,000. Ukienda kwenye bidhaa za ujenzi, vivyo hivyo, bati zimepanda bei, saruji ndiyo usiseme. Saruji sio tu kupanda bei, yaani saruji imekuwa bidhaa adimu ndani ya nchi hii na tuna viwanda. Saruji ilikuwa inanunuliwa kati ya shilingi 13,000 au shilingi 14,000 leo unaitafuta kwa shilingi 17,000 mpaka shilingi 28,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukisoma Mpango, Hali ya Uchumi wanakwambia mambo ni mazuri, Serikali ya wanyonge inasema hakuna mfumuko wa bei mambo yako sawasawa. Sasa, mambo kweli yako sawasawa kwenye makaratasi lakini hayako sawasawa tukitoka nje ya hapa. Bati za geji 8 zilikuwa zinanunuliwa kwa Sh.62,000 leo zinafika Sh.70,000 na zaidi. Nadhani yale mnayoyanena kwenye makaratasi basi yanenwe kwa vitendo huko nje tunakotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la mfumuko wa bei nadhani lipatiwe ufumbuzi sasa hivi halisubiri bajeti. Mtuambie, Watanzania huko nje wanataabika, mambo ni magumu, kila kitu kimepanda bei hatuelewi ni kwa nini kimepanda bei na bidhaa nyingine hazipatikani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ambayo napenda kuichangia ni kuhusu wafanyabiashara. Wafanyabiashara wa nchi hii imekuwa kama ni ule mchezo wa paka na panya. Ni mchezo wa kuviziana, wa kutafutana. Leo wafanyabiashara wa nchi hii wako wengine ambao wanaamua kufunga biashara kwa sababu mazingira ya ufanyaji wa biashara siyo rafiki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa Dodoma hivi tunavyoongea kuna wafanyabiashara wengi tu wameshaandikiwa barua na TRA; wengine wanataka kufungiwa akaunti na wengine wanaanza kufikiriwa kupelekewa hiyo task force ya kuangaliwa kodi ya miaka mitatu nyuma. Kuna wafanyabiashara kule Karatu wamepelekewa hizo task force zinawachunguza eti wanachunguzwa mapato yao kwa miaka mitatu nyuma yalikuwaje wakati huyu mtu analipa kodi yake kila mwaka hajawahi kukwepesha kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaambiwa mashamba hayatozwi kodi, Karatu kule kuna wafanyabishara kwenye Bonde la Eyasi wanalima vitunguu, wote wameambiwa wanapelekewa hiyo task force inachunguza kwa miaka mitatu namna gani wanalima, mapato yao ni nini, wana wafanyakazi kiasi gani, wanatakiwa kulipa nini na kwa nini hawajalipa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Cecilia Paresso.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wote wanalima mashamba ya vitunguu, lini tumeanza tena kutoza kodi mpaka mashamba? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ushauri wangu kwa Serikali.

SPIKA: Muda wako umeisha.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani kidogo tu nimalizie, ili uweze kuongeza mapato ni kuwatengenezea wafanyabiashara mazingira rafiki na unapunguza kodi, ndivyo ambavyo utapata kodi nyingi. Ukiongeza kodi unafukuza na kufunga biashara. Ahsante sana. (Makofi)