Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Mussa Azzan Zungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, agizo la Chama cha Mapinduzi kwa Serikali kutaka uchumi uwe asilimia nane unaweza kufanikiwa katika Taifa letu ikiwa ni pamoja na asilimia za juu zaidi. Ili kufikia hapo ni lazima Benki Kuu ya Tanzania iwe ina-regulate (inasimamia) riba kwenye mabenki ya biashara nchini mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, riba za mabenki ni kubwa mno, ili kukuza uchumi ni lazima riba zishuke. Riba zikishuka zitafanya vilevile na kodi kwa upande wa TRA ambapo sasa hivi wanakusanya kodi vizuri, wanaweza kukusanya zaidi wakiwa na kodi rafiki. Kodi rafiki itamwezesha mlaji au private sector kuwa na mishahara mizuri kwa watumishi wao. Ukiwa na mishahara mizuri nominal wages ikiwa above inflation rate mlaji anakuwa na disposable economy. Disposable economy TRA watapata kodi kutoka kodi ya ulaji ambayo mteja wake atakuwa na uwezo wa kwenda kununua bidhaa katika soko ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe TRA pamoja na kazi nzuri wanayoifanya, wajaribu kuwa na kodi Rafiki. Kwa takwimu za TRA walipaji kodi Tanzania ni wachache sana, tuwe na wigo mkubwa wa walipaji kodi na kodi ikiwa rafiki lazima TRA watapata kiwango kikubwa sana cha ukusanyaji kodi na itaendana sawasawa na pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi rafiki inachangamsha biashara ndani ya nchi. Leo shughuli za za biashara Kariakoo asilimia kubwa zimelala kwa sababu ya kodi za TRA wanazoziweka siyo rafiki. Wakiweza kubadilika kuweka kodi rafiki wataweza kuwafikia wateja wengi na wateja wengi wakilipa volume ya kodi itakuwa kubwa na kuifanya TRA iweze kukusanya mapato kwa rekodi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inajenga barabara kwa pesa za ndani, ni jambo nzuri sana. Daraja la Kigamboni ni mfano mzuri wa PPP kati ya Serikali na private sector. Leo Daraja la Kigamboni linakusanya shilingi 1,100,000,000 kwa mwezi takribani shilingi 13,000,000,000 kwa mwaka. Kwa hiyo, inaelekea kwa miaka 15 ijayo deni la uwekezaji wa Daraja la Kigamboni litakuwa limekwisha. Maana yangu nini? Serikali na wataalam wa TRA wawe sasa na muono wa kutazama road toll kugharamia barabara ambazo zitakuwa zinatumika ili fedha hizi ziweze kutumika kujenga barabara zetu za ndani na za mikoani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mijini katikati barabara zinajengwa na TARURA lakini barabara hizi bado zinakuwa na msongamano kwenye barabara za TANROADS kwa sababu barabara za mijini hazina uwezo wa kubeba magari haya. Wakiweza kutengeneza barabara za ndani au za mitaani zitaweza kusaidia barabara zinazounganisha Mikoa na Wilaya kuweza kupitika kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali watizame namna gani road toll itakavyoweza kusaidia kujenga barabara ndani ya nchi yetu. Kwa kufanya hivyo, tutaipunguzia Serikali mzigo kwa sababu pesa nyingi za ndani zinaweza zikatumika kuwekeza kwenye kilimo, elimu na kwenye mambo mengine sana ya tafiti ambayo ni muhimu kwenye Taifa letu. Barabara za ndani ambazo ndiyo zinabeba mazao ya wakulima zitaweza kuwa zinapitika ikiwa barabara kubwa zitajengwa kwa njia ya road toll. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali pamoja na mikakati mizuri inayoendelea kufanywa tufungue wigo wa kuongeza walipa kodi. Walipa kodi waliokuwepo sasa hivi wanalipa kodi vizuri na sasa hivi kutokana mwamko wa Serikali yetu hii ya Awamu ya Tano wafanyabiashara wote wana- appetite ya kulipa kodi, wako tayari kulipa kodi, lakini kodi yenyewe walipe wengi wasilipe wachache ili kufikia target ya Serikali. Nina uhakika kama tukiwa na kodi rafiki, makusanyo ya Tanzania yatazidi asilimia 30 ya pato la Serikali na yakizidi maana yake Serikali itakuwa na uwezo wa kujiendesha na itajipa heshima kubwa sana ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa kununua ndege ya mizigo. Naiomba Serikali, ndege za mizigo ni jambo muhimu sana kwa ajili ya kusafirisha bidhaa zetu kuzitoa hapa na kuzipeleka kwenye masoko. Ndege hii isifanye kazi tu ya kupeleka bidhaa zetu kwenye masoko ya nje ifanye vilevile kazi ya kubeba mizigo yetu ndani ya soko la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo ndege itakayonunuliwa lazima iweze kukidhi malengo haya yaani iwe ndege kubwa lakini iweze vilevile kutua kwenye viwanja vidogo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Umeniwekea dakika kumi Mheshimiwa?

MWENYEKITI: Ahsante sana tayari.

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)