Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa wa Tatu. Kwanza naipongeza Wizara kwa Mpango tulioumaliza wa 2016 – 2021, pia kwa Mpango huu wa 2021 – 2026. Mpango ni mzuri, tunapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri tu kwenye sekta ya kilimo. Tumekuwa na kawaida ya kutoa fedha nyingi sana kwenye Wizara mbalimbali hasa za Ujenzi, Afya na Elimu. Naomba kama Taifa, katika kuelekea kukabiliana na Mpango huu wa Tatu, tuwekeze fedha nyingi sana kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu tumekuwa na uzalishaji wa mazao mbalimbali kama kahawa, korosho, mahindi, mpunga na mengineyo. Pamoja na mazao hayo yote, ukienda kuangalia katika Mataifa ndani ya Afrika yanayo-export huwezi kukuta nchi yetu katika nchi 10 bora zinazouza mazao yetu nje ya nchi. Sasa tuangalie jinsi gani tunaweza tukatengeneza Mpango ambao ukatufanya nchi ya Tanzania kuingia angalau hata kwenye kumi bora kwa nchi za Afrika zinazo-export mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na Mipango mingi sana. Toka mpango wa Kwanza, wa Pili na sasa tuko Mpango wa Tatu. Hata hivyo, katika Mipango yote hii hatujawekeza vya kutosha katika sekta ya kilimo. Tukichukua fedha zetu tukaenda kuwekeza kwenda uchimbaji wa mabwawa, kwenye maeneo yenye mvua za kutosha, tukakusanya maji, tusiruhusu maji yetu yakapotea; pia tukatengeneza skimu za umwagiliaji; tukatengeneza utaratibu wa kuzalisha mazao ya kutosheleza ndani ya nchi yetu; na tukatengeneza mazingira ya balozi zetu zikafanya kazi ya kutafuta masoko ya mazao ya wananchi wetu. Mheshimiwa Rais anasema anataka kuzalisha mabilionea Tanzania; mabilionea wako kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kule Ulaya wakati wanaendelea ilikuwa ni masuala ya kilimo. Hata biashara ya utumwa ilikuwa ni biashara ya kilimo. Tuwekeze kwenye kilimo, tutapata fedha; tutapata kilimo cha kutosheleza, tutauza nje, tutapata dola, tutatengeneza ajira ndani ya watu wetu, ajira zitaongezeka, tutapunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu na tutaongeza mzunguko wa fedha ndani ya uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia, kikifika kipindi cha masika hata mabasi hayana abiria, hata treni zinapungua abiria, hata ndege abiria wanapungua; watu wanawekeza kwenye kilimo. Mpango wetu huu ujielekeze kwenye kuwekeza angalau hata shilingi trilioni moja, tuombe tupeleke kwenye kilimo. Tuchukue trekta tuwapelekee wakulima wetu kwenye kila kijiji, tuhakikishe kuwa kuna trekta, kuna zana za kuwawezesha wakulima wetu wafanye kazi ya kilimo cha uhakika, sasa hivi wanatumia kilimo cha jembe la mkono, kilimo ambacho hawana uhakika nacho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kilimo tutajikomboa, tutapata utajiri, tutapata dola za kutosha, mzunguko wa fedha utakuwa mkubwa, umaskini utapungua na njaa tutakuwa hatuna. Nchi yetu kijiografia imebarikiwa na ardhi ya kutosha, ina mvua za kutosha, imebarikiwa kuwa na kila kitu, tumeshindwa kuwekeza kwenye kilimo, uwezesho ambao inatakiwa tuone matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo kwenye kilimo bado hatujayaona. Mheshimiwa Waziri, kama kweli tunataka tukomboe Taifa hili, tuwekeze kwenye kilimo. Tunatambua wananchi wetu wanavyohangaika, asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima. Sasa kama ni wakulima mbona hatupeleki fedha za kutosha kwenye kilimo? Kwa nini tusiende kujenga mabwawa? Kama tumefanya operesheni ya ujenzi wa shule, operesheni ya ujenzi wa vituo vya afya, tutafanya operesheni ya ujenzi wa mabwawa na ujenzi wa skimu za kumwagilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi uliyonipa. Ahsante sana. (Makofi)