Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nashukuru sana kwa Mwenyezi Mungu kutupa uhai na uzima, lakini pili, nikishukuru wewe kwa kunipa hii nafasi kuweza kujadili Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda katika maoni yangu kwenye Mpango huu, kuna msemo mmoja wa kiarabu unasema lisanu-l-hali haswa umilisan-l-bakabi; lugha ya hali ilivyo ni fasaha zaidi kuliko lugha ya maneno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo mzungumzaji aliyepita anasema kwamba Serikali hii iliwadanganya watu katika umeme, umeme haukufika vizuri vijijini. Wewe tazama hali ya kura zilizokuwemo humu zilivyoenea, ni fasaha Zaidi, halafu tazama na zile zilizobakia, kwa hiyo hii lugha na hii hali ya humu ndani ni fasaha zaidi kuliko maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite moja kwa moja katika kuboresha mapendekezo ya huu Mpango. Wizara ya Fedha imetuletea Mpango. Katika Sura ya Sita, wameeleza ugharamiaji wa Mpango na wamesema kwamba Mpango huu utagharamiwa kwa jumla ya trilioni 114. Wakasema sekta ya umma trilioni 74 na sekta binafsi trilioni 40, lakini tukiangalia Mpango uliopita, Serikali ilisema kwamba sekta ya umma Mpango wote utagharimu trilioni 107, sekta ya umma itatumia trilioni 59 na sekta binafsi trilioni 48. Lakini matokeo baada ya miaka minne, sekta ya umma imetumia trilioni 34.9 ambayo ni sawa na asilimia 77 ya miaka minne; lakini sekta binafsi imetumia trilioni 32.6 ambayo ni sawasawa na asilimia 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye sekta binafsi, hizi trilioni 32, ni sawa kwa miaka minne, ina maana kwamba kwa miaka mitano sekta binafsi itafika trilioni 40.75. Sasa tumesema tutafanya maboresho kwenye sekta binafsi, huu Mpango umeeleza mambo ya blue Print, umeeleza mambo ya uwekezaji, umeeleza kuondosha vikwazo vingi. Sasa kwa nini tumeipa sekta binafsi trilioni 40, wakati mwaka huu bila marekebisho yoyote, tunaweza kufika trilioni 40 ndani ya miaka hii mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naiomba Serikali ikafikirie tena katika ugharamiaji wa Mpango huu kuwa sekta binafsi haitoshi kwa trilioni 40, tunao uwezo wa kufika zaidi ya trilioni 40 endapo yale maboresho katika Mpango huu kuhusiana na sekta binafsi yatafanyika. Hilo ndilo pendekezo langu la kwanza, kwa sababu tukifika miaka mitano kamili tutakuwa tumeshapita trilioni 40. Je haya maboresho plus tutapata ngapi? Naomba hilo wakalifanye kazi, watakapokuja na Mpango waje watueleze nini kinaweza kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nizungumzie katika Sekta ya Uvuvi. Tumepanga kukuza pato la Taifa kutoka asilimia 7 kwenda asilimia 8; pato la mtu mmoja mmoja dola 1,080 mpaka dola 3,000. Kwenye Sekta ya Uvuvi tumesema kwamba inachangia katika pato hili la Taifa kwa asilimia 1.8 tunataka ichangie asilimia tatu. Ukuaji wa sekta tutatoka kutoka asilimia 3.7 mpaka asilimia 3.9. Uzalishaji kutoka tani 497,000 mpaka tani 600,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa uvuvi huu wa bahari kuu hiki kiwango tulichokiweka ni kidogo kutokana na activities zinazotakiwa kufanyika katika uvuvi wa bahari kuu. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijaribu kuweka tena haya malengo kwa sababu ukuaji wa asilimia 3.9 tunaweza tukazidi endapo tutatumia fursa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja ambalo sikuliona katika Mpango huu. Katika Sura ya Tano Mpango huu umezungumzia mambo mawili; ununuzi wa meli na ujenzi wa Bandari ya Mbegani lakini uvuvi wa Bahari Kuu una mambo mengi ambapo tukitazama hotuba ya Rais imesema kwamba kutakuwepo na viwanda vya uchakataji wa samaki. Hili tungeliona pale katika ile item ya 13, katika lile jedwali ambalo limeeleza flagship project, lakini hapa tumekosea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu; sekta binafsi ili tuweze kuiwezesha kuingia katika uchumi huu wa uvuvi wa Bahari Kuu ina maana kwamba ni lazima tupime tuna samaki wa kiasi gani. Hata gesi, ili uchimbe gesi unatakiwa ujue kwamba ipo gesi kiasi gani. Tuna ukubwa wa bahari na tunajua ukubwa wa bahari, lakini wingi wa samaki tunauelewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta binafsi wanahitaji kuelewa wingi wa samaki halafu wao watakwenda kukopa. Wakiandika proposals zao za kutaka maombi ya kupewa fedha ni lazima waeleze viability ya mpango. Viability ya mpango, moja, ni lazima waoneshe cash flow ambayo itakuwa inapatikana kutokana na huo uvuvi wa samaki. Kwa hiyo, ni lazima wingi wa samaki nao utajwe ili kuwapa kigezo hawa wenzetu wa sekta binafsi waweze kukopa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imegonga Mheshimiwa.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)