Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenisababisha mimi na wenzangu leo tukawa hai, tuko ndani ya Bunge hili Tukufu. Suala la nishati ya umeme, ukiangalia kwenye Mpango wa Pili, target ilikuwa kufikia megawatt 4,915 lakini zilizofikiwa mpaka sasa hivi 1,602.3. Maana yake lengo halijafakiwa, kwa hiyo kama Serikali inayokusanya kodi za wananchi ina wajibu wa kuhakikisha inafikisha malengo ambayo wameahidi kwenye Mpango.

Mheshmiwa Mwenyekiti, licha ya kutofikiwa hivyo, kuna suala lingine ambalo ni la muhimu sana nataka niliseme. Kumekuwa na kusema vijiji elfu kumi na ngapi vimefikiwa na umeme, lakini tuangalie katika katika vile vijiji ni nyumba ngapi zimeunganishwa na huduma ya umeme. Mpaka sasa hivi kwa mijini ni asilimia 39.9 ya nyumba ndiyo zimeunganishwa na umeme na kwa vijijini ni asilimia 24.3 ya nyumba ndiyo zimeunganishwa na umeme, maana yake una nyumba 100 kwa vijijini, ni nyumba 24 tu zilizounganishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali kwa umuhimu wa nishati ya umeme wanapopeleka umeme vijijini, basi wahakikishe wanapeleka nguzo karibu na maeneo ya wanaoishi watu ili iwe rahisi kwa wao kujiunganishia umeme kwenye nyumba zao.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tunza Malapo, kuna taarifa Mheshimiwa Hussein Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mchangiaji, vile vijiji ambavyo vimeshafikiwa na umeme ni vijiji zaidi ya elfu tisa na kitu, haya masuala ya kuunganisha ni kaya ngapi zimeunganisha ni yule mhusika, mwenye nyumba yake alipie na awashiwe umeme, siyo jukumu la Serikali. Nilikuwa nampa taarifa hiyo. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tunza Malapo, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei. Kazi ya Serikali ni kupeleka huduma karibu na wananchi. Kuna nguzo kumi ndiyo mtu umfikie kwenye nyumba yake, unamwambia ajiunganishie kwa nguzo kumi? Tuache bla bla bwana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mdau wa elimu sana, elimu ni uwezo, tunategemea mtu ambaye anapata elimu aelimike aweze kupambana na changamoto zilizoko katika maisha yake au maeneo yanayomzunguka. Tatizo kubwa ninaloliona kwenye elimu yetu ya Tanzania, tunaanza kufeli tangu mtoto anapoingia darasa la awali. Kimataifa ration inayokubalika ni Mwalimu mmoja wa awali kwa wanafunzi 25, lakini katika nchi yetu Mwalimu mmoja wa awali anafundisha watoto 104. Pata picha watoto wadogo, Mwalimu anahitajika kila mtoto amfuatilie, amejua kuandika, hiki ameelewa, una watoto 104 darasani, unawafuatilia vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tatizo linaanzia hapo. Ukienda shule za msingi mimi sisemi, kila mmoja wenu anajua hali ilivyo. Mwalimu unapita uandike ubaoni hata pakupita hakuna, tunataka watoto wakifika vyuo vya kati, wakifika vyuo vikuu wawe na ujuzi wawe na uwezo, wameutoa wapi wakati msingi huku chini ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, ione umuhimu wa kutafuta data zilizo sahihi ili kusudi madarasa ya kutosha yajengwe, madawati ya kutosha yapatikane, Walimu wa kutosha wapatikane; kwa sababu ndiyo maana tunaambiwa kuna projection una project kwamba leo wameingia watoto 2,000 maana yake mwakani wanaweza kuingia 2,500 au 3,000; unatakiwa ujiandae leo, usiwaache watoto nyumbani unasema mpaka madarasa, mpaka madawati yatengenezwe ndio watoto waende shule. Serikali isipende kuzima moto. Kuna sensa ya watu, kuna wataalam wa kuangalia population ya watu, watumie hizo data katika kuweka miundombinu ya elimu ili kusudi watoto wasome katika mazingira yaliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea bandari ya Mtwara; natokea Mtwara, Mbunge wa Mtwara. Wakati sisi hatujaingia Bungeni, mimi Tunza sijaingia Bunge mwaka 2015 kwenda huko nyuma, Bandari ya Mtwara ilikuwa inafanya kazi. Kipindi cha msimu wa korosho meli nyingi kubwa zilikuwa zinakuja katika Bandari ya Mtwara. Nini maana meli za korosho kuja katika msimu, maana yake watu wa Mtwara walikuwa wanapata shughuli za kufanya.

Sasa kwa masikitiko makubwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani meli Bandari ya Mtwara hakuna. Ukiuliza unaambiwa meli zina kuja Dar es Salaam, korosho zisafirishwe kwa barabara mpaka Dar es Salaam, kwa sababu kuzileta Mtwara meli ni gharama hakuna mizigo ya kupakia kutoka Dar es Salaam kuja Mtwara. Naomba niulize, kipindi kile meli zilipokuwa zinakuja Mtwara mizigo ilikuwa inapatikana wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, kama wanaona hakuna mizigo ya kuja Mtwara, wajitahidini kukaa na wafanyabiashara wapunguze kodi ili na Bandari ya Mtwara itumike, mtu aone nikienda kupakia korosho Mtwara kuna ahueni fulani kwa sababu uchumi wa kwetu sisi watu wa Mtwara tunategemea asilimia kubwa korosho. Korosho ukienda kupakia Dar es Salaam tunawaacha vijana na wanawake wa Mtwara hawana kazi. Sasa hivi Mtwara ukienda kuko kama msibani, korosho haieleweki, zinapakiliwa Bandari ya Dar es Salaam, watu wa Mtwara wanafanya shughuli gani? Hapa wanasema wamewekeza bilioni mia moja hamsini na ngapi sijui, zinakwenda kufanya nini wakati hakuna mkakati thabiti wa kuhakikisha bandari ile inatumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huo uwekezaji unaofanywa uendane sambamba na kuchochea meli zije Mtwara ili kusudi zifanye kazi katika Bandari ya Mtwara. Kama ni issue ya tozo ya kodi, Waziri wa Viwanda akae na wafanyabiasha aone ni kwa namna gani anakwenda kuiboresha bandari ile iweze kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la muhimu kwenye zao la korosho bado kuna malalamiko mengi, wakulima wa korosho wanalalamika, wanadai, ili kuepusha malalamiko hayo na watu wapate haki zao, naishauri Serikali imwombe CAG, akafanye ukaguzi maalum, wale watu wote wanaodai walipwe madai yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo kidogo; kuna siku nilikuwa kwenye semina iliyoandaliwa na Wizara ya Kilimo, naambiwa nyanya za kwetu zinaoza, zinatupwa kwa sababu hazina fibber zinazotesheleza kutengeneza tomato source, mananasi ya kule Mkuranga na kwingine, yanaoza yanatupwa kwa sababu hayana ubora, maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiniambia mimi Serikali imeshindwa kupeleka pesa, wataalam wetu wakatafiti, wajue hitaji la soko ni nini. Mkulima akiletewa mbegu bora atalima. Leo mkulima analima, anavuna nyanya zinaishia kuliwa na mbuzi, lakini leo tunamwambia akalime. Hivi nyie mnaijua kazi ya kulima, ilivyo ngumu. Kwa hiyo tunataka wakulima walime, wazalishe kwa tija na mazao wanayopata yaweze kutumika katika viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba hayo niliyoyaongea yafanyiwe kazi kwa maendeleo ya watu wa Kusini na kwa Taifa kwa ujumla. (Makofi)