Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Wiki iliyopita kwa sisi Wabunge wengi tulioingia Bungeni kwa mara ya kwanza tulitumia nafasi hii pia kushukuru Mungu kwa kuandika historia, lakini pia leo tunaingia katika historia nyingine ya kutoa mawazo kwa ajili ya ujenzi wa Taifa letu kwa sababu tunakwenda kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie eneo moja tu, nafasi ya utumishi wa umma katika kufanikisha Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa. Nimeusoma Mpango vizuri kuanzia ukurasa wa 111 mpaka ukurasa wa 120, umeelezea kuhusu maendeleo ya watu na eneo moja kubwa ambalo limekuwa interesting kwangu ni suala la ujuzi. Hotuba ya Waziri na Mpango umeelezea vizuri sana kuhusu ujuzi katika ngazi mbalimbali ambazo namna itakavyotusaidia katika kulisogeza Taifa letu mbele. Hata hivyo, kuna changamoto kubwa sana ambayo Serikali naomba msi-compromise na hili ni suala la utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002; tuna Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za 2003 na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za 2009; vyote katika muundo wake na maelezo yake havitoi nafasi katika suala la ujuzi. Sasa huu Mpango tunaoujadili leo Wabunge, wanaoenda kutekeleza, wanaoenda kusimamia na wanaotakiwa kubuni vyanzo vya mapato ni hao hao watumishi wa umma ambao Mpango haujawatambua vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapolipitisha hili jambo litakwenda na Serikali wasipoliona, matokeo yake baada ya miaka mitano, Waziri ataleta Mpango mwingine utakuja na utakuwa na table inayoandika vikwazo na moja ya kikwazo itakuja ni hili suala. Sasa ushauri wangu ni nini? Sisi kama Taifa linaloendelea tunachukulia mfano wa Malaysia, Malaysia walipofanya mabadiliko yote kwenye kilimo na viwanda walikuja na kitu wanakiita re-energizing civil service; waliamua kuweka nguvu kwenye kubadilisha mfumo wa utumishi wa umma wakaja na mfumo ambao wanaangalia knowledge, skills na ability kwa maana ya kwamba maarifa, uwezo na ubunifu ndiyo vikawa vinampa mtu nafasi ya kufanya maamuzi katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwetu bado tuna mfumo wakwetu tunaita meritocracy na ni mfumo wa kizamani na ndiyo maana mfumo wetu wa utumishi wa umma umejengwa vizuri sana, lakini unafanya kazi kizamani, bado tunatumia model za akina Max Weber za seniority, unapotumia mifumo ya seniority maana yake watu wenye uwezo wenye ubunifu wanakosa nafasi za kufanya maamuzi, michango yao inaishia chini, unakuta maamuzi yanaishia kufanywa na Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na Wakuu wa Vitengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kukupa mfano hata huu Mpango tunaoujadili, unaweza kwenda Wizara ya Fedha ukaulizia, ukakuta wanaoufahamu huu Mpango hawafiki watumishi 30, Wizara nzima hawaufahamu. Tuunde mfumo sheria hizi zibadilishwe, kuwe na mfumo wa kubadilisha vikao vya maamuzi vijumuishe na watumishi wa kawaida ambao wengi wanakuwa na uwelewa mpana.

Kwa hiyo tutapokuwa na mawazo ya wachache matokeo yake kwenye utekelezaji tunakwama na ndiyo maana tunatolea mfano suala la ubunifu wa vyanzo vya mapato, kila siku vyanzo vinarudi vilevile, utaishia vichungi vya sigara, utaishia sijui pombe zenye vileo vikali, ukiwaambia watumishi kubuni vyanzo vipya wale wanaobuni miaka yote ni wale wale, ni level ya juu cluster watumishi wa chini hawashirikishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya wazo ambalo ninalo hata kwa watumishi wa umma, inabidi taasisi na idara zote zinazohusika na makusanyo ya maduhuli na mapato waambiwe ili tuwaongezee mishahara na motisha watumishi wenu wabuni vyanzo vipya vya mapato. Tukifanya hivyo tutakusanya trilioni 40 kwa mwaka hili Taifa, lakini sasa hivi mtu anajua ikifika tarehe 23 tarehe ya Baba Jesca imefika nitapata mshahara, hata nisipofanya kazi hamna litakapofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli tumefanikiwa kujenga nidhamu kwenye utumishi wa umma, lakini nidhamu tuliyonayo ni ya watumishi kuingia saa 1.30 anasaini, anasubiri kutoka saa 9.30, hawana ubunifu, wanaishia kuanza kuzunguka maofisini wanauza vocha, wanauza mabuyu kwa sababu kutokana na mfumo huu hauwasaidii. Ofisi zinabebwa na watu wachache na mtu anajua kwamba mimi sasa hivi nimeshaajiriwa ni permanent and pensionable, nisipokifanya leo na mimi labda siku moja nitakuwa Mkurugenzi nitafanya. Tunataka kila mtu atimize wajibu wake. Namna ya kutimiza wajibu wake ni kubadilisha mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningeshauri Serikali, Wakuu wa Idara kwa maana ya Wakuu wa Taasisi za Umma Wakurugenzi wapewe mamlaka ya kuweza kuteua na kupendekeza watu kwa Katibu Mkuu wa Utumishi wanaoweza kufanya nao kazi kwenye menejimenti. Menejimenti nyingi hazitoi ushirikiano kwa Wakurugenzi walioteuliwa na Mheshimiwa Rais, unakuta Menejimenti ina watu tisa wanaounga mkono Mkurugenzi aliyeteuliwa na Rais ni wanne au watano anashindwa kufanya kazi na wale watu matokeo yake wanabaki wanamkwamisha, ndiyo ile bureaucracy, unakuta dokezo linahitaji laki mbili, maamuzi yanatumia tisa kuamuliwa, hatuwezi kusogea kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tubadilishe huo mfumo Mkurugenzi anapopewa taasisi ya Serikali anapoona kuna watu anashindwa kufanya nao kazi, apendekeze watu kwa Katibu Mkuu wa Utumishi apeleke majina matatu akiletewa moja naye atakuwa hana sababu ya kusema kwa nini nimekwamishwa, lakini atakwamishwa na mwisho wa siku anajua huyu kapewa, baadaye atatumbuliwa atatuacha, ndiyo kauli zinazoendelea kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo lingine ambalo ningependa kupendekeza ni kwenye suala la ubunifu wa vyanzo vya mapato kama nilivyosema. Tunahitaji fedha za kuweza kusaidia huu Mpango; huu Mpango ni wa miaka mitano na Taifa letu tunahitaji lisogee mbele na tuna miradi mikubwa ambayo inahitajika ikamilike tunahitaji fedha. Wapewe nafasi watumishi wabuni vyanzo vipya vya mapato ili kuweza kusaidia Taifa letu kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)