Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu Mpango wa Miaka Mitano na ule wa Mwaka Mmoja. Kwa hakika nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kutujalia uzima na kuweza kukutana leo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda basi niende moja kwa moja kwenye kuchangia Mpango ulioko mbele yetu. Kwanza nianze kwa kupongeza Mpango ule wa Pili wa Miaka Mitano ambao ulipita, tumeuona tathmini yake na katika muda huu tumeona maendeleo makubwa ya nchi yetu. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, pamoja na Serikali na watumishi wote ambao wameshirikiana katika kutekeleza Mpango ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapokuja kwenye Mpango huu wa Miaka Mitano na hasa ule wa Mwaka Mmoja tunaona namna ambavyo tumejipanga kwenda mbele na nitachangia sana leo kwenye eneo ambalo limesema kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Watanzania wengi wanafanya kilimo katika nchi yetu, zaidi ya 70% wanafanya kilimo na kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu. Naomba nikiri wazi kumekuwa na juhudi mbalimbali za kuhakikisha kilimo chetu kinabadilika na kama ambavyo Mheshimiwa Rais amesema katika hotuba yake, kwamba tutaongeza juhudi katika kuwekeza kwenye kilimo na kilimo chenyewe ni kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo tukikifanya vizuri pamoja kuwa kitatusaidia kwenye chakula lakini mapato mengi yanapatikana kwenye kilimo. Leo Halmashauri zetu nyingi zinategemea mapato makubwa kutoka kwenye mazao mbalimbali, kwa hiyo maana yake tukiwekeza kwenye kilimo kutakuwa na mapinduzi makubwa ya kiuchumi na itatusaidia sana kwenda mbele kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hoja yangu ni kwamba ni wazi tumefanya research nyingi, ni wazi tumepata maoni mengi, ni wajibu wa Serikali sasa kuyatendea kazi mawazo yale. Hatuwezi kuwa tunatoa ushauri na ushauri ule tunauacha kwenye makabati. Ombi langu nataka niiombe Wizara ije na mpango mahususi katika kukuza kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kwenye suala dogo sana la ambavyo tunasema Tanzania ya viwanda, lakini viwanda vyetu haviwezi kwenda mbali kama hatujawekeza kwenye kilimo kwa sababu tunahitaji malighafi kwenye viwanda vyetu. Kama leo hatujawekeza vizuri kwenye kilimo chenye pembejeo, mbolea, viatilifu na Maafisa Ugani ambao wanafanya wajibu wao. Naamini huko vijijini wote tunatoka hali ya Maafisa Ugani ni imechoka, hali ni mbaya idara ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii anaweza kwenda kiongozi yeyote ukakutana na Afisa Ugani, wewe unaweza kuwa na uelewa mkubwa kuliko Afisa Ugani maana yake Afisa Ugani huyu hawezi kumsaidia mkulima. Ombi langu nataka niiombe Serikali hasa Wizara ya Kilimo itusaidie kuongeza nguvu kwenye Maafisa Ugani. Naamini kabisa wao pia ni mashahidi kuna baadhi ya mazao ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo nitaongelea zao moja tu la alizeti, mafuta; leo hii sisi tunaagiza tunatakiwa kwa mwaka kutumia metric tons 570,000 za mafuta, lakini uwezo wetu ni 210,000 tu, maana yake ni karibu nusu tunaagiza nje ya nchi. Kwa hiyo maana yake ni kwamba tunatumia fedha za kigeni nyingi kuagiza mafuta ya kula, hili jambo ni vema tukabadilisha mwenendo wetu tuhakikishe kwamba zao la alizeti pamoja na mazao ya mbegu za mafuta, tuchukue hatua kubwa katika kuhakikisha tunawekeza vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatumia karibu bilioni 460 kwa mwaka kuagiza mafuta nje ya nchi, ndiyo maana leo tunakuta kuna upungufu wa mafuta ni kwa sababu hatujawekeza vizuri kwenye eneo hili. Niseme tu kwenye eneo hili tukija na mpango kweli unaosema kwamba wa block farming itakuwa ni jibu la tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kwamba inakuza kilimo cha umwagiliaji kutoka kwenye heka zile ambazo zimeelezwa 461,000 tutakwenda kuhakikisha kwamba tunaongeza zinakuwa 694,000, bado tuna safari ndefu. Lazima tuwe na mapinduzi ya kweli ya kuhakikisha kwamba tunawekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji, tusiendelee kusubiri mvua ambayo hatuna uhakika nazo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunavyoongea habari ya umwagiliaji, tunasemea habari ya kwamba uhakika wa kilimo chetu tusitegemee mvua, lakini wengine walisema hapa, maji yanayomwagika haya kwenye mito kila mwaka, tunayatumiaje ili kuweza kuhakikisha kilimo chetu kinakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hilo la alizeti, nadhani kuwe na mkakati au msukumo maalum, kama tunaweza kuwa na Bodi ya Korosho, kama tunaweza kuwa na Bodi ya Pamba, kwa nini tusiwe na Bodi ya Alizeti ili kuweza kuweka msukumo mkubwa zaidi. Tumeambiwa hapa kuna zaidi ya mikoa nane inayoweza kulima alizeti. Tukiwa na Bodi hii ya Alizeti tutaweka mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba tunalima alizeti kwa wingi, tunawezesha viwanda vyetu na mwisho wa siku tunakuwa na mafuta ya kula ya kutosha. Kwa hiyo ombi langu, naomba kama tunazo hizo nyingine, basi na hii Bodi ya Alizeti iwe ni jibu la kuhakikisha kwamba tunapata mafuta ya kula ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, naomba nichukue nafasi hii kuunga mkono hoja, naomba niwaachie changamoto hiyo Wizara ya Kilimo. Ahsante sana. (Makofi)