Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia kwenye Bunge hili la Kumi na Mbili, nianze kwa kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo langu la Rufiji kwa kunichagua kwa kishindo na kukomboa Kata zote 13 na kupata ushindi ambao haujapata kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango tunaoujadili leo, una mambo makuu matatu. Jambo kubwa la kwanza ni utawala bora; ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu; na uchapa kazi kufikia malengo ya Mpango uliokusudiwa. Hizi siyo ndoto pekee za Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, hizi zilikuwa ni ndoto za Mwasisi wa Taifa hili, Rais wetu wa Awamu ya Kwanza, ambapo yeye katika fikra zake aliamua kuziweka fikra zake katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiisoma Ibara ya 9 ya Katiba, inazungumza misingi ya kwenda kuwasaidia Watanzania; kumsaidia mwananchi mmoja mmoja na kuondoa umasikini, ujinga na maradhi. Kwa hiyo, haya yote yanayozungumzwa leo na Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, yana msingi wake katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwasisi wetu wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ibara ya 9(e) inazungumzia Watanzania kwenda kufanya kazi. Hili ndiyo jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais analisisitiza leo kuwataka Watanzania kufanya kazi ili kwenda kutimiza ndoto za Mpango wa Maendeleo ambao tunaukusudia. Haya pia siyo mageni. Mambo haya tayari yana msingi wake, yalianzishwa na Mwalimu Baba wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Mpango wa Taifa wa Maendeleo baada ya uhuru uliotolewa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1964 mpaka mwaka 1969 na Mpango wa Pili wa Maendeleo uliosomwa mwaka 1969 mpaka mwaka 1974, haya yote yalidhamiria kwenda kukomboa Watanzania. Ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanda na mambo mengi makubwa, Mwalimu Nyerere dhamira yake ilikuwa ni kuhakikisha Tanzania yote inafikika. Wakati ule nchi yetu miundombinu ilikuwa ni square kilometa 86,000, wakati huo Tanzania ilikuwa na watu milioni 9 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujiulize, changamoto zilizopelekea ni kwa nini tulishindwa kufikia malengo ambayo Mwalimu aliyakusudia? Hapa tunajikita katika Watafiti wa kiuchumi wanavyosema. Tunaye mtafiti mmoja anaitwa Daron Acemoglu pamoja na James Robinson, katika kitabu chao cha tafiti kilichokuwa kinazungumza ni kwa nini mataifa yanashindwa kujiendeleza, waliwahi kusema: “Mataifa mengi yanashindwa kwa sababu hayana strong institutions and vigilance. Hayana taasisi zilizo imara, lakini siyo taasisi kuwa imara peke yake, taasisi ambazo zinaweza kujua changamoto tulizonazo na kesho tutafikia wapi? Kama tutashindwa katikati, ni jambo gani tutafanya ili tuweze kufika kule tunakotaka kufika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndipo tunapoiangalia bajeti ya Serikali na tunagundua kwamba Bajeti ya Serikali ya 2019/2020 tulikusanya asilimia 92.8, lakini mwaka 2020/2021 makusanyo ni asilimia 88. Ziko sababu nyingi ambazo wachumi wetu, tungekuwa na taasisi imara wangeweza kutuambia, ni kwa nini tumeshindwa kufikia malengo yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo lilijadiliwa na Bwana Acemoglu, alisema: “The quality of political and economic institutions.” Ni lazima tuwe na taasisi za kisiasa zinazozingatia uchumi, lakini pia tuwe na taasisi za kiuchumi ambazo ni imara, zinaweza ku-focus na kujua Tanzania tunataka kwenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote lazima tuangalie, bajeti yetu leo hii, dhamira yetu ni kukusanya shilingi trilioni 26, je, Taifa letu tutaweza kukusanya shilingi trilioni 13? Kwa sababu tayari tumepanga shilingi trilioni 10 itumike katika miradi ya maendeleo na fedha hizi lazima zitokane na makusanyo ya ndani, tunawezaje kufika huko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, zimekuwepo kelele nyingi sana kuhusu chombo chetu cha TRA namna kinavyokusanya na namna kinavyoshindwa kuwa imara na kutumia taasisi nyingine. Ili tuweze kufanikiwa yapo mambo mawili lazima tuyafanye. Jambo la kwanza, ni lazima tuzipe immunity institutions zetu ili ziweze kujitosheleza, ziwe imara na ziweze kufanya maamuzi kwa niaba ya Watanzania ili tuifikie Tanzania mpya tunayoitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo Bunge linaweza kufanya ni kuitaka Serikali kuleta mbele ya Bunge lako Tukufu vipaumbele vya Taifa vikionyesha flagship projects. Zile project zote ambazo ni kubwa na za kimkakati, basi Bunge liiagize Serikali na litoe Azimio la Kibunge ambapo hatatokea mtu yeyote kuweza kubadilisha Maazimio ya Bunge ili tuweze kuainisha miradi ya kimkakati, vipaumbele vya Taifa letu na ni wapi tunataka kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli amefanya vizuri sana, amekuwa na mpango mzuri sana wa kuipeleka Tanzania mbele, lakini hatujui kesho atakuja nani? Kama Bunge likitoa Azimio na likiungwa mkono na Wabunge zaidi ya robo tatu, kwamba tunataka miradi ya maji ikamilike, tunataka miradi ya mwendokasi wa treni ikamilike, hakuna kiongozi mwingine atakayeweza kuja kubadilisha haya kwa sababu tayari Bunge limeshatoa Azimio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono hoja hii, lakini tuiombe Serikali kama siyo Bunge hili, Bunge linalokuja, ilete ndani ya Bunge vipaumbele, miradi ya kimkakati ili Bunge tuamue robo tatu ya Wabunge kuikubali. Asije Kiongozi yeyote baada ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli kwenda kuipinga miradi hii ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)