Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na nianze kwa kukusahihisha naitwa Mtinga, sio Mtenga. Mtenga ni Wachaga, Mtinga ni Wanyiramba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara ya kwanza naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hai na leo hii nipo kwenye Bunge hili lakini pia niwashukuru wananchi wa Iramba Mashariki kwa kuniweka hapa na Chama changu kukubali wananchi wa Iramba Mashariki wanilete. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni dakika tano naomba niuelekeze mchango wangu kwenye kilimo. Sote tumesema hapa kwamba kilimo ndiyo ajira kuu kwa Watanzania, lakini kuna mambo mengi sana kwenye kilimo ila jambo ambalo limeonekana ni ufumbuzi na halijafanyika vizuri mpaka sasa, ni suala nzima la kilimo cha umwagiliaji. Mabonde tunayo mengi na mengi yameshawekewa miundombinu, lakini hata hayo yaliyowekewa miundombinu bado yanafanya kilimo kidogo sana na sehemu kubwa inabaki haitumiki na hayo mengine ambayo yanafaa pia bado hajawekewa miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri katika kilimo; rafiki yangu Mheshimiwa Bashe nimemwona mara nyingi sana anaongelea global family na nimpongeze amepita maeneo mengi na kuona jinsi ambavyo Serikali imeweka fedha na wananchi bado hawatumii vizuri; nchi yetu tuna hazina kubwa ya watu waliosoma mambo ya kilimo, lakini pia tuna hazina kubwa ya watu waliofanya kilimo pamoja na kuwa hawajasoma. Sasa ningeshauri kwamba katika maeneo haya ya umwagiliaji, Serikali iwekeze kila kitu kwenye maeneo hayo, kuanzia miundombinu, lakini vile vile na kuweka na viwanda vidogo kwa maana ya kuya-add value yale mazao katika maeneo yale. Baada ya kukamilisha, wawakopeshe vijana kuanzia wale wasomi wa chuo kikuu mpaka vijana wa mtaani wa darasa la saba kwa kuwakabidhi maeneo yale na kuwasimamia, walime warejeshe ule mkopo na baada ya hapo maeneo hale yabaki kuwa ya kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna maeneo mengi na kama Serikali itasimamia kwa kuwekeza namna hii, nina hakika tutazalisha na wale vijana watakuwa wamepata ajira. Hii itatuletea kipato, itatuletea uhakika wa chakula, uhakika wa mazao ya biashara kwa ajili ya viwanda, lakini vile vile itatibu suala nzima la ajira. Kwa hiyo nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Bashe hiyo kazi aliyoianza aifanye vizuri zaidi aiendeleze na ahakikishe kwamba maeneo yale ambayo yamewekezwa yanafanya kazi iwezekanavyo na haya mapya fanyeni utaratibu wa kuwakopesha vijana wa nchi hii, wasomi wapo na wasiosoma wapo na wanahitaji wakabidhiwe vitu hivi kama mkopo, wakimaliza wanaendeleza na maeneo mengine yanaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka niende kwenye eneo lingine la ukuaji wa miji. Ni kweli Serikali yetu inawekeza kwenye miundombinu, leo hii ukipita Dar es Salaam unaona barabara za juu, unaona hizo interchange, lakini cha kusikitisha miji yetu haikui, miji mpaka sasa ina vibanda mjini, nyumba za ajabu ajabu, sasa mji haupendezi, mji una barabara za juu, lakini nyumba ni vimakuti vimejaa mjini na vibati vya ovyo ovyo, wakati huo huo watu wanaendelea kuwekeza nyumba za maana mbali na watu hawaendi kuishi huko. Kwa mfano, Kigamboni, nyumba za NSSF hazina watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri kwamba wizara inayohusika katika miji yetu iwatambue wale watu wenye maeneo yale ya zile nyumba ndogo ndogo na vibanda. Ikishawatambua ifanye utaratibu wa kubomoa na kujenga upya mji, maghorofa ya kutosha, baada ya hapo wale watu wapate unit title. Kwa hiyo tutakuwa tumejenga mji na wale ambao maeneo yao walivunja watapata unit title kwenye yale maghorofa na watu wengine sasa watapata miji na hapo Serikali kwanza itapata kodi lakini mji utapendeza na miji yetu itaendana na miundombinu inayojengwa kwa sasa. Tukiendelea kuacha vibanda mijini tunakwenda kujenga mbali, matokeo yake tuna barabara nzuri lakini mtu akiangalia anaona vibanda viko mjini na miji yetu haiendelei kupendeza na tunazidi kukosa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwenye miundombinu, nchi hii sasa inaunganishwa na tunawaza kuunganisha barabara za wilaya na wilaya. Hata hivyo, katika Mkoa wangu wa Singida na hasa katika jimbo langu barabara inayounganisha Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Singida ambao unapita kwenye Jimbo langu la Mkalama ni muhimu sana ikaangaliwa. Tumejenga daraja kubwa la Mto Sibiti zaidi bilioni 28, sasa tulitumie daraja lile kwa kuweka barabara ya lami ili kuunganisha mikoa hii. Pamba yote sasa inayotoka kule inasafirishwa kupitia njia hii ya vumbi, naamini barabara hii ikijengwa kwa haraka na ipo kwenye Ilani, itasaidia sana kukuza uchumi na kuunganisha mikoa yetu na kuendeleza Mkoa wangu wa Singida na hasa Jimbo langu la Mkalama ambapo barabara hii inapita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele imelia, dakika tano ni chache, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)