Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nikushukuru sana na nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyenijaalia afya njema nikaweza kuchangia katika hoja iliyokuwepo mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli kwa huruma na upendo mkubwa aliouonyesha na kuweza kunichagua kuwa Mbunge wa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais. Nasema Mwenyezi Mungu ambariki na sina la kusema zaidi ya kuendelea kumuombea Mwenyezi Mungu aweze kumtetea na aweze kumlinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa maombi yao na Watanzania kwa ujumla, nasema ahsante. Mwisho, nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa upendo walionionyesha na hata mimi kunipa moyo na kuniongoza na kunifikisha hapanilipofikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti,nina hoja ambayo ni ya muda mrefu, lakini Mheshimiwa Rais baada ya kunichagua nimeona nije na hoja yangu. Naomba Wabunge wenzangu mniunge mkono na muitambue kama hoja hii ni kwa maslahi mapana ya nchi yangu.Mwaka 1905 mpaka 1906 katika eneo la Tendeguru, Wilaya ya Lindi Vijijini, Mkoani Lindi walichukua mabaki ya mjusi kupeleka Ujerumani. Mwanzo nilikuwa nadhani ni mabaki yale ni ya mjusi mmoja, kumbe na mijusi sita, lakini nazungumza kwa uzalendo na uchungu wa kuhakikisha haya mapato ni lazima yawasaidie Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama mimi sitatumia lakini kuna watu wanahitaji mapato hayo kwaajili ya elimu, barabara, afya na kadhalika. Ujerumani wamepeleka lile jusi na Watanzania kutoka Lindi walilibeba kichwani jusi moja lilikuwa na uzito wa tani 250 kutoka Dendeguru mpaka kufika Kilwa tu kwenye Bandari, basi ujue wametembea kilomita 150, wametesekaje watu kama hawa, wengine wamepoteza maisha yao ukichukulia kipindi hicho kilikuwa ni kipindi cha wanyama wakali; je, wale wananchi wa kule wameangaliwaje, hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Tunaambiwa kuwa wao kwa mwaka wanakusanya Euro milioni 278, ukifanya calculation za haraka ni sawasawa na bilioni 834, sisi kama Tanzania hatujapata chochote. Ukiwauliza wanasema zile pesa zimejenga museum kule kwao, zinatumika kuwalipa mishahara watu wanaomtunza, zinalipa hela za tafiti mbalimbali, zinawawezesha wanafunzi wanaokwenda pale kujifunza wanatumia nafasi ile. Nasema haiwezekani na wanasema wameingia mkataba na Umoja wa Mataifa kuwa haiwezekani huyo mjusi kumrudishaTanzania, hakuna kisichowezekana katika ulimwengu huu wa Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabilioni yale 834 wanayoyavuna Wajerumani hata kule anapotoka mjusi yule hawapathamani. Sisi Tanzania ndio owner wa yule mjusi na Watanzania mfunguke na siyo kila wakati mnataka kubeza, mbona kama mngekuwa naye Tanzania msingeweza kumfanyia chochote, je, kama nao wangemwacha wangefaidika, wasingefaidika naye. Ina maana kuwepo kwa mjusi yule kwao ndiyo wamefaidika. Leo dunia unaisikia inavyozungumza wanaitegemea Afrika ife ili wachukue rasilimali zetu na walikwenda pale kuchimba madini. Hivyo Ulaya unayoiona, dunia ya kwanza unayoiona ilitajirika kwa kupitia Afrika. Wametegemea dhahabu, almasi, copper, zinc, shaba kutoka Afrika lakini sisi wenye Afrika hatujitambui na wala hatujielewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao, wanahitaji viwanda vyao vifanikiwe na ili vifanikiwe wanahitaji raw material kutoka Afrika. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais anasema tunahitaji viwanda kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya nchi yetu. Haya mazao yetu badala ya kupelekwa Ulaya yatafanya kazi hapa hapa tutawapelekea vitu ambavyo tumevi-process Tanzania. Tuangalie kipindi hiki tunachokizungumza cha Corona hatuwezi kuleta chochote kutoka nje lakini kama viwanda vyetu vingefanya kazi, nani angeagiza khanga kutoka India au China, tungekuwa na khanga zetu kutoka urafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya mjusi tumeunda Kamati, naomba uridhie na uingize ndani ya Hansard na uitambue kama Wabunge wako wamejitolea rasmi kuhakikisha haya mapato yanakuja Tanzania. Nataka niwatambue Wabunge ambao wako tayari akiwemo Mheshimiwa Kigua, Mheshimiwa Reuben Gwagilo, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Juma Hamad, Mheshimiwa Maimuna Patani na wengine watakaojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji mapato yaje Tanzania na siyo mapato tumekwenda kufanyiwa presentation Wizarani neno la kukatisha tamaa la kwanza wanasema haiwezekani hata mfanyaje mkafanikiwa. Mimi nasema inawezekana na tutafanikiwa. Lugha ya kukatishana tamaa Tanzania tuiache. Katika maisha yangu sina uwoga, nikipambana na kitu changu nasema hiki kitu kitafanikiwa na nasema nitafanikiwa. Ndiyo maana nakwenda sambamba na nyayo nafuatilia miguu step by step ya Mheshimiwa Rais kwa ajili ya mafanikio. Mheshimiwa Rais hana woga, ametishiwa sana, ameambiwa sana kuwa haiwezekani lakini yamewezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hoja ya madini imewezekana na hii hoja nahakikisha kuwa itawezekana. Nachoomba ni ushirikiano wa Wizara mbalimbali zinaguswa na hoja hii. Kama waliona mapambano haya hayawezekani hata kama mimi naondoka lakini bado kuna wanaharakati wako humu ndani ya Bunge ambao watakwenda sambamba na tutashinda vita hii na kuiletea mapato nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alinipigia simu Balozi akaniambia Mama Lulinda usirudi nyuma na mimi nimemwambia niko na wewe sirudi nyuma. Ananiambia panafanyika mafunzo mbalimbali ya watu duniani kwenda kusoma kwa nini mjusi ile mikubwa imetoka Tanzania, sisi wenyewe Tanzania tuko wapi? Hatupo! Tuna watoto wamesoma wanahitaji kwenda kufanya exchange program kwa nini wanawachukua watoto kutoka Marekani, watoto wa Tendeguru wako wapi? Kuna watoto wamemaliza shule tunataka Wajerumani wakawasomeshe watoto wale ili tukijenga Museum kule Tendeguru basi na wao wawaeleze hapa ndipo palitoka fossil za mjusi kutoka Tanzania. Hivyo exchange program ya elimu naomba iwepo katika mkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili, watu wa University of Dar es Salaam wanakwenda kuchukua fund kwa ajili ya kufanya research…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia ni dakika moja Mheshimiwa Lulida muda umeisha malizia.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Niendelee?

MWENYEKITI: Malizia maneno yako ya mwisho.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa research University of Dar es Salaam wanachukua pesa, watu wa Makumbusho wanachukua pesa lakini wanachukua fund zile bila kuwa na utaratibu. Nachoomba sasa hivi pawepo na utaratibu Wajerumani waje kukaa na Tanzania tuwe utaratibu maalum haya mapato yaweze kuisaidia nchi yetu. Kwa mwaka wanapata Euro milioni 278 sawasawa na bilioni 834 Tanzania tunapata nini? Tunaomba Wizara…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Riziki Lulida.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)