Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyeniwezesha kusimama katika Bunge hili la Kumi na Mbili. Pia nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo waliweza kupendekeza jina langu na kunisababisha nikawe Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa kura nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwape shukrani sana ndugu zangu wananchi wa Temeke, wenyewe tumezoea kujiita TMK Wanaume kwa kunipa kura nyingi za kishindo hata leo nimeweza kusimama hapa na kuitwa Mbunge wa Jimbo la Temeke kama mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuishukuru familia yangu pamoja na marafiki zangu. Pia nisiwasahau wanangu; Matrona Kilave pamoja na Samuel Kilave kwa sababu walinitia moyo sana katika kipindi kile kigumu, naamini sasa wanafurahia matunda ya maombi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niunge mkono hotuba ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa hapa Bungeni na kitabu cha miaka mitano ambacho nimeweza kukisoma. Namuunga mkono sana kwa jinsi ambavyo hakika mambo mengi ya miaka mitano iliyopita yameweza kufanyika na hata sasa naamini kwa miaka hii mitano mingine yote yaliyoandikwa katika kitabu kile pamoja na Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi yanakwenda kufanyika sawasawa na Ilani yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika elimu. Nishukuru sana Wizara ya Elimu kwa jinsi ambavyo Rais, Dkt. Magufuli, ameweza kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Hata hivyo, lipo moja ambalo napendekeza waweze kulisikia na kuweza kuliweka sawa, nashauri kwamba wajikite kuweka vifaa vya TEHAMA ili hata walimu wetu wanapofanya kazi zao wafanye kazi kwa bidii na tuweze kupata kwa wakati majibu yote ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie suala la afya. Nimpongeze sana Rais, Dkt. Magufuli, kwa jinsi ambavyo ameweza kuweka sekta ya afya kwa namna ya kipekee kabisa. Sasa akina mama tunajidai, tunajifungua bure pamoja na kwamba zipo changamoto chache ambazo naamini Serikali yetu ni sikivu na inakwenda kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika afya hakika mimi nishukuru sana katika kata zangu 13 ni kata chache tu ambazo hazina zahanati. Namshukuru sana Rais, Dkt. Magufuli, pamoja na Wizara husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika yote hayo niombe kusema kwamba ipo changamoto ndani ya jimbo langu, sina uhakika kwa wengine, lakini pale ambapo tunakuwa tunauguza na inapofikia yule mgonjwa amefariki, tunapokwenda kuchukua maiti tunadaiwa fedha. Niombe Wizara ya Afya suala hili kidogo linaleta utata ndani ya hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe basi kama Wizara ya Afya itaweza kutoa tamko kwamba tufanye nini pale ambapo tunakuwa tumefiwa tunapohitaji kwenda kuchukua maiti yetu. Labda kama inawezekana tupewe elimu wakati tunapouguza tufanye nini ili tusifikie kudaiwa fedha. Niombe sana Wizara ya Afya iliangalie hili na naamini Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake, wajina wangu Mheshimiwa Dkt. Dorothy ataliangalia hili na kuweza kuona tunapata majibu mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pia ni mhanga wa miundombinu katika Jimbo langu la Temeke. Kama nilivyosema tuna hospitali nyingi, tumejengewa na masoko mazuri lakini katika kupita kwenye barabara zile za ndani hakika TARURA sasa waweze kupewa angalau ongezeko la fedha ili tuweze kuona tunapita kwa usalama na kufikia zile sehemu ambapo Serikali yetu imeweza kujenga zahanati pamoja na masoko mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Rais na nimpongeze sana na Mungu ambariki kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya. Ahsante sana. (Makofi)