Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kabla ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha kufika mahali hapa. Pili nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniamini na zaidi pia niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Busokelo kwa kunichagua kwa awamu nyingine tena ya pili, maana wanasema imani huzaa imani, nami nitawatumikia kwa moyo wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba zote mbili za Mheshimiwa Rais, ya kwanza nilishiriki 2015 na sasa ni 2020 na ndiyo maelekezo, ndiyo maagizo, ndiyo mtazamo wa nchi na hakuna ambaye anaweza kupinga hotuba hii kwamba ndiyo mwelekeo wetu wa nchi ya Tanzania kwa miaka mitano ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichangie hasa suala la ajira kwa vijana. Vijana wetu, wanafunzi wengi wanamaliza lakini ajira kwao ni changamoto. Ajira hizi zina uhusiano hasa hasa na sekta mbalimbali, si sekta tu ya kusoma, kama elimu ya Vyuo Vikuu, lakini na sekta zingine za kilimo, uvuvi, mifugo na sekta zingine mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na sekta ya uvuvi wa bahari Kuu; Bunge lako Tukufu mwaka 2018 lilitoa ripoti kuonyesha ni kwa namna gani ambavyo uvuvi wa Bahari Kuu hatuutumii vizuri, tunaita blue zone. Kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Rais ukisoma ukurasa 17, ameandika hivi: “Nchi yetu pia imebarikiwa kuwa na maeneo mengi yanayofaa kwa shughuli za uvuvi ikiwemo ukanda wa pwani, maziwa, mito na mabwawa. Hali hii inafanya sekta hii kuwa na nafasi ya kutoa mchango mkubwa kwenye kukuza pato la Taifa na pia kupambana na umaskini na tatizo la ajira. Hata hivyo kwa sasa mchango wake bado ni mdogo”.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yake ni nini? Bunge lako mwaka 2018 liliunda tume ambayo ilishughulikia masuala ya uvuvi wa Bahari Kuu na ikatoa ripoti kwamba hivi sana kwa miaka tisa Serikali imekusanya takriban bilioni 29.7, kwa wastani wa mwaka maana yake ni sawasawa na bilioni 3.3. Hotuba ile pamoja na ripoti ile imeonyesha Tanzania tukitumia vizuri kina kirefu cha bahari tuliyonayo, tuna uwezo wa kukusanya mapato kwa mwaka takriban bilioni 353. Hapa mimi nakuja na taarifa muhimu na natamani Waziri wa Mifugo pamoja na Uvuvi azisikilize takwimu hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kina cha Bahari ya Hindi kama tutakitumia vizuri kwanza kuna samaki wanaoitwa tuna ama jodari kwa wale ambao wanatoka maeneo hayo wanafahamu. Samaki huyu sasa hivi inakadiriwa kwamba kwa kina chetu cha bahari ya hindi wako samaki milioni 50. Katika hao samaki wanavuliwa na meli zinazotoka nje ya Tanzania na samaki hawa wana uwezo wa kutaga mayai mmoja mmoja milioni moja moja kila samaki huyu mmoja, tafsiri yake ukizidisha hesabu rahisi tu pale, maana yake ni milioni 50, ukizidisha kwa samaki hao milioni 50 na kwa mayai milioni moja moja unaweza ukapata zaidi ya trilioni 50 mayai ambayo yanaweza yakatagwa ama vifaranga katika huo uchumi wa bahari kuu. Tafsiri yake nyingine pia ni kwamba kwa miezi mitatu baada ya kutagwa mayai samaki huyu anakuwa na urefu na uzito wa takribani kilo 10 mpaka kilo 20 na akizidi zaidi ya miezi minne mpaka mitano anakuwa na uzito wa takriban kilo 80 na maximum kabisa ni kilo 95. Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuchukue tu hawa ambao wanakuwa na kilo 80; sasa kilo 80 kwa samaki mmoja ambaye anauzwa kwa dola za Kimarekani 18,000 kwa rate ya leo ya Kitanzania ya Sh.2,320, ni sawasawa na kusema samaki mmoja ana uwezo wa kuuzwa kwa Sh.41,760,000 za kitanzania. Huu ni uchumi mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukichukulia sasa hao samaki milioni 50 zidisha kwa samaki mmoja mwenye thamani ya Sh.41,760,000 ni zaidi ya trilioni mbili ambazo zilitakiwa ziingizwe kupitia uchumi wa bahari kuu. Hii hatuifanyi, hivyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi na Mifugo asimamie hili na nitampa taarifa zote na ripoti zote ambazo zinaonesha ni kwa kiwango gani Tanzania tunaweza kufikia trilioni mbili kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tumezungumza hapa habari za elimu yetu ya Tanzania…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, nitaleta maandiko lakini nitachangia zaidi kwa suala la elimu ili tuone namna gani wenzetu wa South Africa wameweza kuepukana na suala hili zima la ajira kutumia mfumo wao unaoitwa YES. YES maana yake Youth Employment Service.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)