Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hii aliyotupa Chama chetu cha Mapinduzi kushinda ushindi wa kishindo na baadhi yetu kuturejesha Bungeni. Nampongeza sana Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwani leo Chama cha Mapinduzi na wanachama wake kinatimiza miaka 44 tangu kuzaliwa kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli yake aliyoitoa ndani ya Bunge hili kwamba atashirikiana bega kwa bega na Rais wa Zanzibar pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kwamba Zanzibar inasonga mbele kiuchumi na wananchi wake wananyanyuka kiuchumi. Amedhihirisha hilo kwa kusema kwamba kwenye uvuvi wa bahari kuu anapeleka meli nne Zanzibar ambapo meli nne hizo zitasaidia Zanzibar katika dhana yake ile ya uchumi wa blue. Zanzibar sasa imejipanga kuingia kwenye uchumi wa blue na hapa Mheshimiwa Rais wa Muungano ameonesha dhamira yake ya dhati Zanzibar kuingia kwenye uchumi wa blue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najihusisha sasa kwenye sekta ya kilimo. Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake ameonesha dhamira ya dhati kwamba sasa anataka kumnyanyua mwananchi mdogo mdogo na mkulima mdogo mdogo, mvuvi pamoja na wafugaji ili waweze kupata tija ya kilimo chao, tija ya uvuvi wao na tija ya mifugo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali, Mheshimiwa Rais aliahidi kuwapunguzia kero wakulima na wavuvi na ameonesha kwamba tumepunguza tozo na kodi mbalimbali 114 ambazo zinamlenga mvuvi, mkulima na mfugaji na amesema wazi kwamba ataendelea kuangalia kero na tozo mbalimbali ambazo zinawagusa wakulima, wavuvi na wafugaji. Mheshimiwa Rais ameonesha dhamira ya dhati kuwasaidia wakulima wa bustani ambapo wakulima wa bustani walikuwa na changamoto kubwa sana katika usafirishaji wa mazao yao. Kwa hivyo sasa Serikali imepanga kununua ndege ambayo itasaidia kupunguza changamoto za kusafirisha mazao hayo ya bustani ambayo mazao ya bustani yana soko kubwa katika nchi za nje, tatizo ilikuwa jinsi ya kuyafikia masoko hayo. Mheshimiwa Rais ameonesha dhamira kwamba sasa masoko hayo yatafikiwa na wakulima watapata faida ya mazao yao wanaozalisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kwamba kilimo chetu kinakuwa bora na endelevu na chenye tija, lazima sasa tuwekeze kwenye mbegu bora, mbegu ambazo zitalingana na udongo wa nchi yetu na mazingira yake na maeneo husika, lakini mbegu ambazo zitaangalia mazingira yanayohusika linapolimwa zao husika. Ni vema sasa tukaziimarisha taasisi zetu zinazohusiana na uzalishaji wa mbegu pamoja na viuatilifu ili viweze kutatua changamoto ya mbegu na viuatilifu kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea katika kilimo, naunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais za kutaka sasa kilimo kiwe kilimo cha kisasa, kilimo chenye tija ambacho kitakuwa kilimo cha umwagiliaji. Sasa ili kuhakikisha kwamba kilimo cha umwagiliaji kinafanikiwa ni vyema sasa tukaimarisha pia kwenye sekta ya maji ambayo itasaidia kwenye viwanda, ukulima, uvuvi na ufugaji. Tukipata maji ya kutosha kwa wananchi lakini pia maji ya kuimarisha kilimo chetu, nashauri Serikali Mfuko wa Maji uongezewe fedha ili kukidhi mahitaji hayo ya wananchi. Nasema hivi kwa sababu fedha ambazo zimetumika kwenye Mfuko wa Maji zimeonesha kutoa mafanikio makubwa katika kutatua changamoto za maji na hivyo tukiongeze fedha kwenye mfuko wa maji, tutaisadia sasa TAWASA ili iweze kukabiliana na changamoto za maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, naomba nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano, wasaidizi wake wote, Mheshimiwa Spika, wewe mwenyewe kwa kulisimamia Bunge letu hili tukaweza kutekeleza yote ambayo tumefikia kwa sababu kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali na kuisimamia. Bunge hili Bunge hili lilifanya kazi hiyo na ndiyo maana maendeleo haya yakafikiwa na nategemea wataendelea kufanya hivyo na sisi Wabunge tuko pamoja na wao na Serikali yetu kuhakikisha tunafikia pale tulipokusudia, kumpa Rais wetu imani na kumpa Rais wetu hamu ya kututetea na kutuletea maendeleo. Ameonesha dhamira ya dhati kwamba yeye ni Rais wa wanyonge na anatetea wanyonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)