Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii nami kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kwanza kabisa napenda kutoa pole kwa familia ya Mzee Waheke kwa kifo cha mzee Waheke, lakini pia kwa familia ya Mzee Mantago kwa kifo cha bibi yetu mpendwa Bhoke ambaye amefariki muda mchache katika hospitali ya Benjamin Mkapa. Mwenyezi Mungu azilaze roho hizi mahali pema peponi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza tu kwenye hotuba ya Rais ukurasa wa 66 ambao amezungumzia kuhusu elimu. Kama Taifa tunatakiwa kuwekeza kwenye elimu. Ukiangalia tulivyo sasa, elimu ya msingi, sekondari na hata vyuo vikuu bado tuna changamoto kubwa sana na ili tuweze kuwa na elimu bora na kupata wataalam wa fani mbalimbali ambao wamebobea na kuweza kupunguza umaskini katika Taifa letu na hapo kukuza uchumi, lazima Serikali itoe kipaumbele kwenye elimu. Leo ukiangalia miundombinu bado iko dhofli-hali. Tuna shule watoto wanakaa chini ya miti. Watoto wanakaa kwenye mawe, Walimu ofisi zao ni kwenye miti, leo hatuna madawati, vitabu vya kutosha; Walimu badala ya kupata motisha, wengi hawana mishahara wala hawana nyumba. Sasa haya yote tusipoyaboresha hatutakuwa na watu ambao wameelimika na Taifa lililoelimika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uchache sana hapo nashauri Serikali itatue tatizo la upungufu wa walimu mashuleni. Serikali iliondoa walimu wengi sana kupitia vyeti fake lakini haikuweza kufanya replacement na walikuwa tayari kwenye payroll.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kabla walimu wa vyeti fake hawajaondolewa tulikuwa tuna upungufu mkubwa sana wa walimu. Unakuta shule ina mwalimu mmoja au walimu wawili, unategemea watoto wafaulu katika shule hii? Nashauri kwanza Serikali iharakishe ku-replace wale wote ambao walitolewa kwa vyeti fake maana kuna Watanzania wengi mtaani ambao wana sifa za kuwa walimu wawaajiri lakini pia kuajiri walimu kwa ajili ya shule hizi ambazo hazina walimu wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye vyuo vikuu amesema anaongeza bajeti ya wanufaika wa mikopo ya vyuo vikuu, ni jambo jema sana. Hata kwenye kampeni yake 2015 alisema hatakubali kuona mtoto wa Kitanzania ambaye ana sifa za kwenda chuo kikuu anakaa bila kupata mkopo. Sasa kupata mikopo ni jambo moja na jema lakini hawa wanufaika wa mikopo hii badaye wanakuja kukaa kwenye kaa la moto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Sheria ile ya 2004 na marekebisho ya 2016 makato ni makubwa sana. Huyu Mtanzania unamkata asilimia 15 ya mshahara wake baada ya miaka miwili tu baada ya kuhitimu kama ameajiriwa na kama hajaajiriwa atatakiwa kulipa Sh.100,000/= bila kujali anazipata wapi; unamkata asilimia 6 ya kulinda thamani ya fedha; unakatwa asilimia 10 iwapo amechelewesha kama penalty; na anakatwa asilimia 1 ya kusimamia ule mkopo. Mtu huyu anakatwa makato mengine mengi; kuna NSSF hapo asilimia 10, bima, Pay As You Earn ambayo tunaipigia kelele, kodi ya wafanyakazi ni kubwa sana haijawahi kurudi hata kwenye single digit, huyu Mtanzania atabaki na shilingi ngapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, bado hapo mtu huyu anatakiwa akope, hata sisi Wabunge tumekuja hapa tumekopa yaani ule mshahara wetu sisi tumekopea. Sasa huyu mfanyakazi ambaye ana mlolongo mwingi wa makato naye atataka kukopa ili aweze kujinufaisha, atakuwa anabaki na shilingi ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliuliza swali hapa na Waziri hakunijibu kifasaha ingawa alisema tunaweka hivi ili makusanyo yawe mazuri, tumekusanya asilimia 46. I think tatizo ni recovery system ili hii mikopo iweze kurejeshwa na siyo kuongeza rate ambazo zinazababisha makato kuongezeka. Kama Taifa in fact ilitakiwa tuwekeze kupata wajuzi wa fani mbalimbali at the level of university. Tena tungekuwa tunawapa mikopo kwamba warejeshe tu bila hizo riba nyingine na tuwape muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi unakuta wengi, hasa ambao hawajaajiriwa, wanajificha, hawezi akafungua hata account, anaogopa. Sasa hivi mtu anajifanyia biashara zake au anaweza akaingia tu mkataba wa ajira siyo za Serikalini ili nisigundulike nisije kukatwa hayo makato ambayo mmeyaweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya kwanza yanasababisha moja, hata benki zetu zinashindwa kupata hawa wateja, kwa sababu, nikiamua kujificha hata akaunti sitafungua. Pili, hata nyie Serikali kwa kufanya hivyo mnakosa mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili marejesho ya-boost kutoka asilimia 46 tupunguze ije 8 hata tano, watakuwa wengi ambao wanaleta marejesho haya na watoto wetu wengine wengi wataweza kufaidika. Naomba sana Serikali mlichukue hili mlifanyie kazi, it is a burden to these people wanaokopa ambao ni watoto wa kimaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)