Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii adimu ambayo umenipatia ili niweze kusema machache kuhusiana na hotuba ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuchangia nitumie fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima, lakini pia kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili niweze kujadili masuala mazima yanayohusiana na hotuba hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa mambo mengi ambayo Mheshimiwa Rais alizungumza katika hotuba yake ni pamoja na nchi yetu kuingia katika uchumi wa kipato cha kati. Hii ni habari njema kwa Taifa na ni jambo la kujisifia kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa ni kweli Serikali yetu imetuingiza katika uchumi wa kipato cha kati, kuna mambo ya msingi sana ambayo yanapaswa au yalipaswa ku-reflect moja kwa moja kwamba sasa Tanzania tumeingia katika uchumi wa kipato cha kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mbele ya Bunge lako tukufu nijikite katika masuala makuu manne ambayo yanaashiria moja kwa moja kwamba ni ama tumedanganywa kama nchi kwamba tumeingia katika uchumi wa kipato cha kati au Serikali imedanganya kwamba sasa hivi imekuwa ikikusanya mapato makubwa sana ambacho ni kiashiria cha ukuaji wa uchumi wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, mosi, wewe ni shahidi kwamba Serikali imekopa pesa nyingi kutoka kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mfano NSSF; Serikali imechukua, au imekopa fedha ambazo Serikali ilitarajiwa irudishe ile mikopo ndani ya ule muda ambao masharti yanasema ili mwisho wa siku sasa wastaafu, mama zetu, mashangazi zetu, wajomba zetu ambao walitumikia nchi hii kwa uaminifu mkubwa sana na baadaye wakastaafu sasa waweze kupewa…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jenista.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge anayezungumza. Anataka kujenga hoja kwamba Serikali bado haijalipa fedha ambazo ilikuwa inadaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilipe taarifa Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeshafanya kazi hiyo na mpaka sasa zaidi ya trilioni 1.2 ambazo Mfuko wa PSSSF ulikuwa unaidai Serikali, fedha hizo zimekwisha kurudishwa na Mheshimiwa Mbunge ni shahidi wakati tulipokuwa kwenye kikao cha Kamati, mimi mwenyewe na watendaji wa Mfuko tulishatoa taarifa hiyo kwenye Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mengine ambayo Serikali bado inaendelea kufanya uhakiki. Utaratibu wa Serikali sasa hivi katika madeni yaliyobakia haiwezi kulipa bila kufanya uhakiki, kwa hiyo kila baada ya uhakiki Serikali imeendelea kuwa inalipa madeni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, labda nitakapokuja jioni ama wakati wa kuchangia Mpango tutatoa taarifa ya wastaafu wangapi wamekwishalipwa mafao yao na kwa nini labda kumekuwa na kuendelea kuwalipa wastaafu mafao kwa utaratibu mmoja na mwingine. Kwa hiyo maeneo haya tutayatolea maelezo lakini justification ya malipo ya Serikali tunayo na Serikali imelipa na tunaendelea kuhakiki na tunaendelea kulipa yale yaliyokwisha kuhakikiwa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nikiri kwamba mama yangu, dada yangu, rafiki yangu mpenzi, anafanya kazi nzuri sana, lakini itoshe kusema kwamba hayo aliyoyasema kwamba Serikali haijalipa ndiyo hayo ambayo nayaongelea mimi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasema tayari imetuingiza kwenye kipato cha kati. Kama tumeingia kwenye kipato cha kati na tayari kuna wastaafu ambao waliitumikia nchi hii kwa uaminifu mkubwa sana hawajalipwa, itoshe kusema kuna tatizo. Sasa nimshauri dada yangu na rafiki yangu achukue ushauri wangu huu, kwamba pamoja na kazi nzuri anayoifanya, hili linaitia doa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja katika ajenda yangu ya pili inayohusiana na Serikali kuchelewesha malipo kwa makandarasi. Ikiwa kweli Serikali hii imetuingiza katika kipato hiki cha kati, ilipaswa moja kwa moja kitu cha kwanza kabisa iwe inalipa on time fedha za makandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe umesikia jana, leo, juzi, wachangiaji wengi katika Bunge hili wamekuwa wakilalamika kuhusiana na ujenzi wa barabara. Kwa hiyo, unaposikia kuwa…

T A A R I F A

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, kuna taarifa.

Waheshimiwa Wabunge, hii itakuwa taarifa ya mwisho kwa sababu muda wetu ni mfupi. Mheshimiwa Charles Kimei.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimweleweshe msemaji kwamba hivyo vitu anavyovizungumza haviendani na hoja anayotaka kutoa ya kusema kwamba tuko kwenye kipato cha kati. Kipato cha kati hakiendani na mambo ya Serikali kukopa au Serikali kutokulipa, hayo ni mambo tofauti kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotumika ni wastani wa pato la mtu mmoja. Unachukua pato la Taifa unaligawanya kwa idadi ya watu, unapata huo wastani. Kwa hiyo, hiyo haihusiani na mambo ya Serikali kutokulipa au kufanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumwelekeza kwamba hilo analozungumza ana hoja nyingine pengine lakini siyo hiyo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, unaipokea taarifa hiyo?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza taarifa hiyo siipokei, lakini nakuomba wewe na Kiti chako unilindie muda wangu wa dakika tano vizuri sana, nakuomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anadai kwamba ninachokiongelea hapa siyo sehemu ya hiyo dhana nzima ambayo nimetoka kuisema. Hata hivyo, ikiwa pato la Taifa hali-reflect maisha ya wananchi ya kila siku, tusijidanganye kwamba tumeingia katika uchumi wa kati. Mfano, wakandarasi wanashindwa kwenda kulipa fedha kwenye…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, nilikupa sekunde 30 kwa sababu kengele ilishagonga. Ahsante sana. (Makofi)