Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Furaha Ntengo Matondo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge lako tukufu ikiwa ni mara yangu ya kwanza, lakini pia nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kuweza kuwa hapa siku ya leo kwa ajili ya mchango wa hotuba ya Rais.

Mheshimiwa Spika, napenda kwanza kumshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa wananchi wetu wa Tanzania kwa kuonesha kwamba imani ya Tanzania inapatikana na mpaka leo hii tukiwa Bungeni tuna amani kubwa sana, lakini pia niwashukuru wanawake wa Mkoa wa Mwanza kwa kuniamini na kuweza kunichagua kuwa mwakilishi wao katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi kwa kunichaguwa na kunipa nafasi ya kuwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba moja kwa moja nijikite kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuona kwamba tuna haja ya Wizara hii kupata kipaumbele kikubwa ambavyo vimewapatia katika hotuba yake tumeisoma sote ni hotuba ambayo imelenga kujenga sana kwenye Kanda zetu za Ziwa na hata kwenye bahari.

Mheshimiwa Spika, ninaomba sasa kwa wale wavuvi wadogo wadogo ambao wao bado hawajatizamwa vizuri, waweze kuona ni jinsi gani wanaweza kupatiwa zana za kuweza kufanya kazi ili waweze kuondokana na changamoto za uvuvi harama. (Makofi)

Katika Kanda ya Ziwa hasa Mkoa wa Mwanza kuna akinamama ambao ni wafanyabiashara na wanafanyabiashara ndogo ndogo, lakini akinamama wale wanaitwa akinamama wachakataji, tunaomba sasa waweze kupatiwa vitendea kazi ili waweze kupata chanja za kuanika dagaa na hata kuanika samaki ili wasiweze kuanika chini na hata samaki wale na dagaa wakawa na mchanga kitu ambacho kinawanyima soko, lakini pia hatupati afya bora kwa sababu tunakula chakula siyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba kidogo niongelee suala la elimu; ninashukuru sana Serikali yetu imeweza kutoa vipaumbele kwa wanafunzi wetu ambao wanasoma bure mpaka form six, lakini pia wameweza kujenga majengo ya shule kila sehemu imeonekana. Niombe tu tunawanafunzi wetu watoto wa kike ambao ningeomba kila Wilaya basi angalau ipate shule ya bweni ya kuweza kuwawezesha mabinti zetu waweze kusoma wakiwa wametulia ili waweze kupata elimu bora tunapokwenda kusema hamsini kwa hamsini ili iweze kuwa ratio sawa na hata mabinti zetu waweze kuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongee kidogo kuhusu suala la afya, naishukuru sana Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kwa kuona kwamba hatuwezi kuenenda bila kuwa na afya njema, hilo ninamshikuru sana. Ameweza kujenga vituo vya afya, hospitali za kanda na kila kata kuna hospitali. Lakini niombe, naomba tuweze kupata matabibu katika vituo vya afya, lakini pia tuweze kupata madaktari watakaoweza kutoa dawa za usingizi kwa sababu majengo yamejengwa, lakini ni madaktari wetu kidogo wamekuwa ni wachache basi niombe Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli iweze kuona kuna haja sasa ya kuajiri madaktari na wanaotoa dawa za usingizi ili wananchi wetu wasiweze kuhangaika kwenda kupata huduma mbali wakati huduma wameshawekewa karibu.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa sababu Serikali yetu imeona ni jinsi gani akinamama tunahangaika ikaona kuna haja ya kuweza kupata mikopo ya asilimia kumi. Sasa niombe Wizara husika iweze kusimamia ili asilimia kumi iweze kutoka kwa wakati na wanufaika waweze kupata kile walichokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia naunga mkono hoja. (Makofi)