Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika,hii ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako tukufu, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye imempendeza mimi kiumbe wake kuwa sehemu ya Bunge lako hili la Kumi na Mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa namna ya kipekee nikishukuru Chama changu chini ya uongozi wake Mwenyekiti wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kunipa imani, lakini kwa namna ya kipekee pia nishukuru familia yangu na wananchi wa Jimbo la Mikumi kwa imani yao juu yangu kuwakilisha katika Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge lako la Kumi na Moja lilifanyakazi kubwa, kazi ambayo imemsaidia Rais wetu na Serikali yetu kwenda kwenye uchumi wa kati. Jukumu la Bunge hili la Kumi na Mbili naamini ni kwenda kutoa tafsiri chanya ya uchumi wa kati katika maisha ya Mtanzania mmoja mmoja. Hotuba ya Mheshimiwa Rais inatupa dira na mwangaza wa nini ambacho anataka kutoka kwetu, lakini pia anatuonesha ni jinsi gani tunaweza kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda ili Mtanzania mmoja mmoja aone matunda ya nchi yake kuwa katika uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili tunapoenda kuzungumzia uchumi wa kiwanda sekta ya kilimo hatuwezi kuiacha nyuma kilimo ndiyo uti wa mgongo kilimo ndiyo kila kitu. Kuna mengi ambayo naamini yako nje ya uwezo wetu ambayo Serikali bado inayafanyia kazi. Lakini kuna mengi ambayo yako ndani ya uwezo wetu naamini tukisimama pamoja tunaweza kumkomboa mkulima na mkulima akawa sehemu ya uti wa mgongo katika Tanzania ya viwanda ambayo wengi tunaitarajia na wengi tuna matumaini nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna changamoto naomba nichukue kilimo cha miwa kama mfano. Jimbo la Mikumi wakulima wa miwa katika Bonde la Kilombero wanauwezo wa kuzalisha tani 900,000 za miwa, mnunuzi ni mmoja tu kiwanda cha sukari Kilombero ambaye uwezo wake kila mwaka ni kununua tani 600,000 tu. Maana yake tunaenda kupoteza tani 300,000 kila mwaka. Hakuna namna ambayo tunaweza kuelezea zaidi ya wananchi kukosa matumaini na hujuma kuwa sehemu ya maisha ya wakazi ama wakulima wa bonde lile.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mfano msimu huu zaidi ya ekari 1,300 ama zaidi ya tani 30,000 za miwa zimeteketea kwa moto, hasara hii kubwa ambayo wakulima hawa wa miwa wameipata inaelezea ndwele ambayo inaelezea changamoto wakulima wanaipitia. Katika hali hii mimi naamini Tanzania haipaswi kuwa na nakisi ya sukari ama kuagiza nje sukari kama tunaweza kujiweka vizuri na kujipanga pamoja na nakisi ya sukari ambayo tunayo viwanda hivi ambavyo kazi yake ni kuzalisha sukari vimekuwa na jukumu la kuagizia sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwanza jukumu la kuagiza sukari lisiachiwe wazalishaji wa sukari, kwa kuwafanyia hivyo maana yake wanakosa incentive ya kuhakikisha miwa ya wakulima inaenda kusangwa katika viwanda vyao. Jukumu hili libebwe na Bodi ya Sukari ama Serikali yenyewe na viwanda hivi vijikite katika suala zima la uzalishaji wa sukari ndani. Tukifanya hivi maana yake tunaondoa incentive kwao. Lakini la pili miwa ya wakulima isiuzwe kwa tani za miwa, tuuze kwa suclose, kwa kufanya hivi mkulima anaenda kupata thamani ya zao ambalo amelitolea jasho lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiondoka hapo kwa namna ya kipekee nilikuwa naomba kuzungumzia suala zima la utalii. Tunaambiwa watalii 20 kati ya 100 ndiyo ambao wanarudi Tanzania kwa ajili ya kutalii. Tuna swali la kujiuliza kwanini hawa 80 hawarudi? Wakati tunaendelea kutafakari hili naamini majibu mazuri ya Serikali yanaweza yakaboresha sekta ya utalii na kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya watalii kwa kuhoji maeneo ambayo tuna changamoto nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusiana na hii barabara ambayo inahudumia SGR…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)